Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga
Mhe. Azza Hilal Hamad ( CCM) amekabidhi gari la kubebea Wagonjwa ‘
Ambulance’ lililotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia,Wazee na Watoto katika Kituo cha Afya Tinde kilichopo katika
halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mhe. Azza Hilal Hamad amekabidhi gari
hilo leo Ijumaa Mei 8,2020 kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta
Mboneko katika Kituo cha Afya Tinde kilichokuwa kinakabiliwa na ubovu wa
gari ambalo lilikuwa linagharimu shilingi milioni 5 kila mwezi kwa
ajili ya matengenezo.
Akizungumza wakati kukabidhi gari
hilo,Mhe. Azza aliishukuru Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuboresha huduma za afya ili
wananchi wapate huduma bora za afya.
“Mwezi Julai mwaka 2018 Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akiwa katika ziara yake mkoani Shinyanga alitembelea
kituo cha afya Tinde akajionea hali yake. Tukiwa tunaendelea na Ziara
katika Halmashauri nilimuomba atusaidie gari la wagonjwa kwa ajili ya
Ushetu lakini katika kujibu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliahidi
serikali italeta magari kwa ajili ya Ushetu na Tinde na leo ninakabidhi
gari hili katika kituo hiki cha Tinde”,alieleza Mhe. Azza.
Mbunge huyo pia ametoa shilingi Milioni 1
kwa ajili kuchangia ujenzi wa Uzio wa Kituo cha Afya Tinde pamoja
shilingi 2,500,000/= kusaidia ujenzi wa wodi ya wazazi katika Zahanati
Lyabukande pamoja shilingi 2500,000/= kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya
wazazi zahanati ya Mwamanyuda.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Tinde,
Dkt. Greyson Matogo alisema kituo hicho kinakabiliwa na upungufu wa
watumishi wa afya na kwamba gari la wagonjwa lililopo ni bovu na mara
kwa mara limekuwa likiharibika na kujikuta wakitumia shilingi milioni 5
kwa ajili ya matengenezo kila mwezi.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko alimshukuru Mbunge Azza Hilal kwa namna
anavyotolea kusaidia wananchi ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi.
Kuhusu changamoto ya upungufu wa
watumishi wa afya, Mkuu huyo wa wilaya alisema serikali italeta
watumishi wawili katika kituo cha afya Tinde, Samuye wawili na Kambarage
mmoja.
No comments :
Post a Comment