Tuesday, May 12, 2020

MUHIMBILI KUENDELEA KUTAMBUA MCHANGO WA WAUGUZI



Mkurugenzi wa Uuguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili Bi Zuhura Mawona akiongea na waandishi wa habari.
Muuguzi wa Hospitali ya Taiga Muhimbili Bi. Sophia Sanga akiongea na waandishi wa habari.
Baadhi ya wauguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili wakila kiapo cha maadili ikiwa ni kumbukumbu ya siku ya wauguzi duniani .
………………………………………………………………………………..
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeendelea kutambua mchango mkubwa unaofanywa na wauguzi katika sekta ya afya kwa kuendelea kufadhili masomo kwa wauguzi mbalimbali wanaojiendeleza ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za kibingwa zinazotolewa katika
Hospitali hii kubwa nchini.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Uuguzi Bi. Zuhura Mawona katika mkutano wake na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya wauguzi duniani iliyobeba kauli mbiu isemayo Wauguzi; Sauti inayoongoza Uuguzi kwa Dunia yenye Afya.
Aidha Bi Mawona amesema kuwa Katika kuhakikisha usalama wa watoa huduma hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu COVID19 Kurugenzi ya Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia kitengo cha ushonaji hivi karibuni imebuni na kushona mavazi ya watoa huduma kujikinga na maambuzi (PPE)
“Kurugenzi ya Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kupitia kitengo chake cha ushonaji, imeendelea kutengeneza vifaa kinga (MNH PPE GOWN) kwa ajili ya kuwakinga watoa huduma wanao hudumia wagonjwa walioambukizwa COVID 19, ambapo awali mavazi hayo upatikanaji wake ulikuwa adimu.” Amesema Bi Mawona
Bi Mawona alisema kuwa kwa kuzingatia kuwa asilimia kubwa ya watumishi wa sekta ya afya nchini ni wauguzi, Hospitali Taifa Muhimbili itaendelea kuwajengea uwezo wauguzi tarajari pamoja na wauguzi kutoka sehemu mbalimbali nchini ili kufanya huduma za kibingwa ziweze kupatikana nchini.
“Hospitali ya Taifa Muhimbili inapokea na itaendelea kupokea wauguzi tarajari na kuwawekea mazingira mazuri sana ya mafunzo ili waje kuwa wanataaluma bora katika kutoa huduma kwa watanzania lakini pia tunaahidi kuendelea kuwajengea uwezo Wauguzi na Wakunga wanaokuja kwa kupata uzoefu wa utoaji wa huduma katika vitengo vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum, Kitengo cha kusafisafisha figo, pamoja na vitengo vingine vinavyotoa huduma za kibingwa ili kuhakikisha wanapata uzoefu wa kuweza kutoa huduma hizo kwa watanzania mahali pao pa kazi.” Amesema Bi Mawona
Aidha Bi Mawoma amewataka wauguzi wote nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia viapo kwani wauguzi ndio humpokea mwanadamu anapokuja duniani na ndio pia humuhifadhi na kumsitiri pale mauti yanapomkuta.
Katika mkutano huo baadhi ya wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili walikula kiapo cha maadili ikiwa ni kumbumbu ya siku hiyo muhimu katika taaluma ya uuguzi.

No comments :

Post a Comment