Mmoja wa wapiga debe kwenye stendi
kuu ya Igumbilo akifurahia msaada wa mtambo wa kisasa wa kunawia mikono
uliotolewa na kampuni ya Asas kwa ajili ya abiria na wafanyabiashara
kwenye stendi hiyo unaoweza hudumia watu zaidi ya watano kwa wakati
mmoja
Afisa Usalama, Afya Mazingira na
Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles akitoa elimu jinsi ya kutumia
mashine hiyo kwa baadhi ya wananchi wanaotumia stendi hiyo kwa shughuli
za kila siku.
Abiria na wananchi wakinawa mikono mara baada ya kupatiwa msaada wa mashine kutoka kampuni ya Asas (picha na Denis Mlowe)
………………………………………………………………………………………
NA DENIS MLOWE,IRINGA
STENDI kuu ya Igumbilo na stendi
ya zamani zimekabidhiwa msaada wa mashine ya kunawia mikono ya kisasa
kutoka kwa kampuni ya Asas ya mjini Iringa ikiwa ni mwendelezo wa
kampuni hiyo kusaidia jamii kupambana na kuenea kwa virusi vya coroni
mkoani hapa.
Msaada huo wa mashine mbili za
kisasa ambazo zinazinatumia miguu kuweza kutoa maji na vitakasa mikono
ni kubwa zinazoweza kuhudumia watu zaidi ya watano kwa wakati mmoja
zimekabidhiwa na mwakilishi wa kampuni hiyo, Afisa Usalama, Afya
Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles kwa niaba ya
mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri kwa wenyeviti
wa stendi hizo.
Cosmas alisema kuwa kutokana
na wanafunzi wa vyuo na kidato cha sita wakitarajiwa kuendelea na masomo
yao Juni 1 kampuni ya Asas Group imehimarisha huduma ya kujikinga na
maambukizi ya virusi vya Corona kwa abiria wanaotumia stendi kuu za
mjini Iringa kuongeza mashine za kisasa za kunawia mikono kwa lengo la
kuhudumia wananchi wengi zaidi.
Alisema kuwa kampuni imetoa
mashine hizo zenye uwezo wa kuhudumia watu sita kwa mara moja kwa kila
moja zimetolewa katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya
Igumbilo, mjini Iringa na stendi kuu ya daladala zinazotoa huduma katika
maeneo mbalimbali ya mjini huo.
“ Kama kampuni tumelenga
maeneo yenye mikusanyiko mikubwa, tukianzia na stendi kuu za mjini
Iringa na baadae tutaenda kwenye maeneo mengine ambayo pia yana
mikusanyiko mikubwa ya watu ndani na nje ya mkoa kwa lengo la kusaidia
jamii kuweza kupambana na maambukizi ya virusi vya corona
vinavyosababisha ugonjwa Covid 19,” alisema.
Aidha alisema kuwa kampuni
hiyo imekwishatoa msaada wa ndoo maalumu za kunawia mikono, barakoa na
vitakasa mikono kwa makundi mbalimbali ya jamii mjini Iringa, wakiwemo
madereva wa daladala, bajaji na bodaboda.
Akizungumza mara baada ya
kupokea msaada huo, Mwenyikiti wa Stendi ya Igumbilo, Mwinyi Mwaugali
alisema kuwa wanakumbana na changamoto kubwa ya uhaba wa vifaa vya
kunawihia kwenye stendi hiyo kutokana na kuwa kubwa hivyo msaada huo
umekuwa muhimu sana kwa wanaotumia stendi hiyo.
Mwaugali aliishukuru kampuni
ya Asas na kutoa wito kwa kampuni ya hiyo kuangalia uwezekano wa
kuongeza mashine zingine kama hii kwasababu katika stendi hii kuna
maeneo saba ya kushusha na kupakia abiria hivyo zitasaidia kwa kiasi
kikubwa
Kwa upande wake askari wa
usalama barabara wa kituo kikuu cha daladala cha mjini Iringa, Koplo
Rashid aliwataka abiria na watu wengine wanaotumia kituo hicho cha
daladala kuitumia mashine hiyo ili kujinusuru na janga hilo.
“Asas ametoa msaada huu
kwasababu anawapenda watu, ombi langu kwa watu wote wanaotumia stendi
hii tusiigeuze mashine hii kuwa pambo, ifanye kazi iliyokusudiwa ili
kutunusuru na maambukizi ya virusi hivyo,” alisema
No comments :
Post a Comment