Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Serikali
imeanza kuchukua hatua za haraka kuumaliza mgogoro wa eneo lililo ndani
ya Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI UYOLE) lililopo kata ya Ilomba
mkoani Mbeya.
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 9 Aprili 2020 ametangaza
hatua za serikali katika kutatua mgogoro huo mara baada ya kufanya ziara
ya kikazi ya siku moja mkoani Mbeya akiwa ameambatana na Kamati ya
ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe
Albert Chalamila na kulikagua eneo hilo na kuzungumza na wananchi
husika.
Waziri
Hasunga ameiagiza Taasisi ya TARI Uyole kutoendelea na shughuli za
utafiti mpaka hapo kesi ya mgogoro huo iliyopo mahakamani itakapotolewa
uamuzi.
Kwa
upande wa wananchi, Waziri Hasunga amewataka kusitisha shughuli zote za
kilimo ili kusubiri maamuzi ya mahakama. Kuhusu mazao ambayo
yalishalimwa na wananchi hao amesema kuwa wataruhusiwa kuvuna lakini
hawataruhusiwa kuendelea na kilimo.
Wananchi
hao wapatao 200 kwa mujibu wa orodha waliyoiandika na kusaini kwa ajili
ya kuwasilisha malalamiko yao kwa katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo
Januari 1, 2020 wanailalamikia serikali kwa kutowalipa fidia kwa wakati
hivyo kuiomba kuwalipa fidia ama kuwarudishia eneo hilo.
Eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta 8.52 limekuwa likitumiwa na wananchi hao kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na ufugaji.
Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila amewasihi wananchi hao kadhalika
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Uyole kuitikia maelekezo ya Waziri wa
Kilimo kwani serikali itafanya maamuzi ya busara na kila mtu atapata
haki yake inayostahili.
Na
endapo mahakama itabaini kuwa wanastahili kurudishwa eneo hilo
watapatiwa kwa mujibu wa sheria na kama itabaini hawana haki kadhalika
itafanya maamuzi.
MWISHO
No comments :
Post a Comment