Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini, Wang Ke,
Ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 10, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini, Wang Ke, Ofisini
kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 10, 2020. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amekutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa
Wang Ke na ameishukuru Serikali ya nchi hiyo kwa misaada ambayo imetoa
katika kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaotokana na maambukizi
ya virusi vya corona (COVID-19).
“Tunaishukuru Serikali
ya China kwa misaada ambayo imetupatia hadi sasa vikiwemo dawa na vifaa
tiba. Na leo umesema kwamba kuna asasi za kiraia na wafanyabiashara
bado wanakusanya vifaa vingine ili viletwe hapa nchini vitusadie kuzuia
maambukizi, tunawashukuru sana.”
Waziri Mkuu
ametoa shukrani hizo leo (Ijumaa, Aprili 10, 2020) ofisini kwake Mlimwa,
jijini Dodoma alipokutana na Balozi huyo. “Mchango wenu ni muhimu sana
kwetu, kwa sababu tunaanza kupata uzoefu wa namna ya kupambana na
ugonjwa huu,” amesema.
Amesema
Tanzania Bara na Zanzibar zinapata wagonjwa kwa sababu ni vituo vya
biashara lakini wageni wote wanaoingia nchini kwa sasa wanawekwa sehemu
maalumu ambako wanapatiwa huduma zote wakiwa hukohuko.
“Tunashukuru
Watanzania wa pande zote mbili wanaendelea kupokea maelekezo wanayopewa,
wanaendelea kujikinga na kuchukua tahadhari za kutozunguka ovyo ili
wasisambaze maambukizi,” amesema.
Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa China kwa niaba ya Serikali ya
nchi hiyo kwa jinsi ambavyo waliwahudumia wanafunzi wa Kitanzania zaidi
ya 500 wanaosoma China katika kipindi chote cha kupambana na ugonjwa
huo.
“Balozi
Mbelwa Kairuki amekuwa akitupa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na
jinsi mlivyowasaidia wanafunzi wetu walioko huko na kuhakikisha wanakuwa
salama tangu maambukizi yasambae nchini China.”
“Leo hii
Tanzania tumeanza kupitia tatizo lile lile ambalo liliwapata ninyi. Tuna
wagonjwa wachache lakini tuna kundi kubwa la wale waliokutana na
wagonjwa na bado tunaendelea kuwafuatilia na kuwapima kila siku.”
“Tunaendelea
na jitihada za kuzuia maambukizi mapya, tunatoa elimu kwa wananchi wetu
na kuwaelimisha kuhusu kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono.
Tunaendelea kufanya tathmini kila siku ya watu wanaopimwa. Tumezuia
mikutano na mikusanyiko yote, tumefunga shule na vyuo, tumezuia michezo
ili tusisambaze maambukizi.”
Waziri Mkuu
amemweleza Balozi huyo kwamba kwa sasa Tanzania imefunga mipaka yake kwa
sababu hata nchi jirani zimefunga mipaka yao na endapo kuna wageni
wanaingia nchini, ni lazima waende kwenye isolation centres ambako wanalazimika kukaa kwa siku 14.
Kwa upande
wake, Balozi Wang Ke alimfikishia salamu za shukrani Mheshimiwa Waziri
Mkuu kutoka kwa Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang. “Waziri Mkuu wetu
anashukuru kwa barua ya pole uliyomtumia wakati nchi yetu inapitia
janga kubwa la ugonjwa wa virusi vya corona,” alisema.
Alimweleza
Waziri Mkuu Majaliwa kwamba nchi yake sasa hivi haina maambukizi na
kwamba hivi sasa wamelenga kuzuia maambukizi mapya kutoka nje ya nchi
yasiingie nchini mwao.
“Kwenye
baadhi ya miji tumefungua viwanda na vimeshaanza uzalishaji wa bidhaa
ili kufufua uchumi wetu. Mwaka huu ni muhimu sana kwetu kwa sababu nchi
yetu ilijipangia kuwa uwe ni mwaka wa kuhakikisha kuwa hakuna kabisa
umaskini (zero poverty). Kwa hiyo, tunapambana kurejesha shughuli za
kiuchumi zilizoathirika kutokana na ugonjwa huu,” alisema.
Balozi Wang
Ke alisema nchi yake imechagua baadhi ya nchi za Afrika ambazo
inazisaidia kwa kubadilishana nazo uzoefu kupitia mikutano kwa njia ya
video (video conferencing) ili ziweze kukabiliana na ugonjwa huo.
“Zaidi ya
hayo, kuna misaada ya vifaa tiba kwa ajili ya Serikali ya Zanzibar na
Tanzania Bara ambayo inakusanywa na asasi za kiraia na wafanyabiashara.
Hii iko njiani, na ile ya Tanzania Bara itawasili wiki ijayo.”
No comments :
Post a Comment