****************************
Nteghenjwa Hosseah – OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya
Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo
amelitaka Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA) na Taasisi ya Elimu
Tanzania(TET), kuhakikisha utaratibu wa kufanya marejeo ya mitihani
ulioanza kwa kidato cha sita uhusishe
madarasa yote yanayotarajia
kufanya mitihani ya Taifa.
Aidha, amewataka wanafunzi
kuzingatia ratiba ya masomo inayotolewa ili wasikose vipindi
vinavyorushwa kwenye redio,runinga na mitandao ya kijamii.
Jafo alitoa kauli hiyo alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa masomo kwa njia
ya runinga,redio na mitandao ya kijamii.
Alitaka taassi hizo kuangalia
utaratibu huo wa marejeo kwa madarsa mengine kama kidato cha pili,cha
nne,darasa la saba na la nne ili nao wawe na umahiri katika kujibu
mitihani yao.
Alisema Serikali kupitia wadau
mbalimbali imetoa fursa hiyo muhimu ambayo inapaswa kuzingatiwa na watu
wote wakiwemo wazazi,walimu na wanafunzi wenyewe.
“Niwatake wanafunzi wote hasa wa
kidato cha sita ambao sasa maandalizi ya kufanya marejeo
yanafanyika,tutumie fursa hii vizuri ya kujiandaa kwa utaratibu mpya
utakaotumika kuanzia mwaka huu wa kupima umahiri tofauti na ule wa awali
wa kuulizana maswali tuliouzoea,”alisema Jafo.
Aliongeza kuwa “Wanafunzi tumieni
fursa hii iliyoletwa kwenu,zingatia ratiba,jipimeni uwezo wenu ili
wenzio wasikuache nyuma pindi mkirudi shuleni,someni kwa bidii kwa maana
tunataka kuelekea kwenye Taifa lenye uchumi imara.”
Aliwataka walimu kutumia fursa
hiyo kujijengea uwezo wao wenyewe pia lakini kuwawezesha kuwa na uelewa
zaidi ili wanafunzi wao watakapohitaji msaada pale watakapokwama wawe
wanajua nini kinachoendelea.
“Walimu wetu najua mtu huwezi kuwa
mkamilifu kwenye maeneo yote,kwa upande wenu hii pia ni fursa ya
kujijengea uwezo kupitia walimu waliopo kwenye program hii ili ukirudi
shuleni unakuwa umeongeza kitu kipya,lakini mwanafunzi wako anaweza
kukupigia simu ameshindwa kuelewa sehemu Fulani hivyo inakuwa rahisi
kumuelewesha,”alisema Jafo.
Waziri Jafo alisema kama Waziri
anayesimamia elimu ya awali,msingi na sekondari amefarijika kuanza kwa
utaratibu huo na ni imani yake kuwa pengo la vijana waliokuwa wanakaa
nyumba bila ya msaada wowote wa kimasomo linaenda kuzibika.
“Wazazi wapeni nafasi watoto wenu
ya kushiriki vipindi vyote vinavyotolewa, inawezekana vipindi
vinaendelea wewe mzazi umempa mtoto wako kazi nyingine anafanya hilo sio
sahihi, toa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha watoto wanasoma na
kufanya mazoezi yote yanayotolewa na walimu,”alisisitiza Jafo.
Jafo alivitaja vyombo vya habari
ambavyo vinashiriki kikamilifu katika mpango huu wa ufundishaji wa
vipindi kwa njia ya Televisheni na Radio kuwa ni TBC, ZBC, Azam Tv,
Channel Ten, Clouds Fm, Global Tv, Gel Tv na Radio mbalimbali.
Pia aliwakumbusha wazazi na
wanafunzi wote kuwa vipindi hivyo vitakua vinarushwa kupitia mtandao wa
Youtube kwa ajili ya marudio ili kujenga uelewa zaidi.
“Mitandao ya Youtube itakayokuwa
inarusha vipindi hivyo ni ya Baraza la Mitihani – NECTA, Taasisi ya
Elimu Tanzania – TEA, Global Education Link – GEL, Global Tv, Azam Tv,
ZBC TV na EATV” alisisitiza Jafo.
Alizipongeza taasisi zote binafsi
zilizoshirikiana na Serikali kuhakikisha lengo lake linatimia katika
kipindi hiki cha mpito cha ugonjwa wa Corona unaosababisha homa kali ya
mapafu(COVID 19).
Alizataja Taasisi hizo kuwa ni
Mawakala wa Vyuo Vikuu Nje ya Nchi yaan Global Education Link (GEL),
UNESCO na Taasisi ya Elimu Solution.
No comments :
Post a Comment