Mkuu wa Takukuru Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
…………………………………………………………………………………………
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) Mkoani Manyara, inawashikilia mawakala watatu wa
ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kudaiwa kupokea
rushwa.
Mkuu wa Takukuru wa mkoa wa
Manyara, Holle Makungu akizungumza jana alisema mawakala hao walikamatwa
juzi wakiwa wanajipongeza kwa kunywa vinywaji kwenye bar ya Mandosi
iliyopo Dareda kati.
Makungu aliwataja mawakala hao
kuwa ni Idd Sulle na Ezekiel Samwel wa kituo cha kazi cha kizuizi cha
Kampala na Basil Aloyce wa kizuizi cha Sinai.
Alisema mawakala hao wanadaiwa
kuomba na kupokea rushwa ya sh120,000 ili kutoa kibali cha kusafirisha
mazao yao kutoka mkoani Singida kwenda jijini Arusha.
Alisema mawakala hao wa kituo cha
Kampala walimsimamisha mfanyabiashara huyo akiwa na mazao yake kituo cha
Sinai mjini Babati na kuchukua nyaraka zake.
“Mfanyabiashara huyo alikuwa na
mazao ya mchele, vitunguu na viazi mviringo akisafrisha kwenda kuuza
jijini Arusha, alitii agizo hilo kisha kesho yake akafuata nyaraka
zake,” alisema Makungu.
Alisema baada ya kufuata nyaraka
hizo aliambiwa awapatie rushwa ya sh120,000 ili watie saini nyaraka hizo
na yeye aendelee na safari yake akiwa na mazao hayo ndipo akatoa
taarifa Takukuru nasi tukaweka mtego.
“Ukiacha kucheleweshwa kwa sababu
za rushwa kwa mfanyabiashara huyo, baadhi ya mazao kama vitunguu na
viazi vimeharibika hivyo watuhumiwa pamoja na kufikishwa mahakamani
watawajibika kwa kulipia hasara hiyo,” alisema.
Alitoa rai kwa wakurugenzi wa
Halmashauri zote za mkoa wa Manyara, kuweka mawakala waadilifu kwenye
vizuizi ili kuondoa usumbufu na kudhibiti upotevu wa mapato unaofanywa
na mawakala wasio waadilifu.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa
Babati, walidai kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu kwani baadhi ya
mawakala wanakusanya ushuru wamekuwa wakipata rushwa kwa kutumia mtindo
huo.
Mfanyabiashara wa mazao Elias Umbu
alisema mawakala hao wanapaswa kubadilika na kutambua kuwa nyakati za
kuchukua rushwa kwenye mazao zimepita waridhike na wanachokipata.
No comments :
Post a Comment