Friday, April 3, 2020

KLABU YA MBIO ZA MAGARI WAJIPANGA KUFANYA VYEMA

Timu ya mbio za magari kutoka Mkwawa chini ya Ahmed Huwel wakionyesha vikombe vya ubingwa walivyobeba katika moja ya mashindano ya magari .
Mkuu wa mkoa wa Iringa akimpongeza Ahmed Huwel ‘Simba’ katika moja ya mashindano aliyochukua ubingwa wa kukimbiza magari.
…………………………………………………………………
NA DENIS MLOWE,IRINGA
KLABU    ya Mbio za  Magari mkoa wa Iringa(Iringa Motorsport  Club Tanzania)imejipanga kurudi vyema msimu mpya unaotarajiwa kuanza hivi karibuni katika kuinua mchezo wa
kukimbiza magari nchini na kutoa bingwa wan chi kutoka ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza na mwanahabari hizi,Mwenyekiti wa Klabu hiyo mkoa wa Iringa, Hamid Mbata alisema kuwa wamejipanga vyema kuweza kuinua mchezo huo kwa mkoa wa Iringa na nchini kwa ujumla kwa kuwa wana wanachama wenye moyo na nia ya kufanya hivyo kwenye mchezo huo.
Mbata alisema kuwa kwa wanachama wa Klabu hiyo mkoa wa Iringa wamekuwa mstari wa mbele katika kulipia ada ya mwaka ya uanachama hali ambayo itawezesha kushiriki mashindano mbalimbali na kuendelea kuifanya klabu kuwa hai zaidi.
Klabu hiyo yenye wanachama mbalimbali akiwemo bingwa wa magari nchini Ahmed Huwel na mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ndio klabu ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuandaa mashindano ya magari nchini yakiwemo ya Mkwawa Rally ambayo yamejizolea umaarufu nchini kwa sasa na kudhaminiwa na maji ya Mkwawa.
Aliwataka wanachama kuendelea kulipia ada za klabu kama ambavyo wengine wametoa ada zao kwa mwaka mzima na wanaruhusiwa kulipia kipindi cha nusu mwaka ambapo kwa miezi 6 wanalipia sh. 30000 ambacho kinaishia mwezi Juni mwaka huu na ada ya mwaka mzima ni 60000 na kulipia 10000 ya kitambulisho.
Alisema kuwa kwa sasa chama hicho kimeweka mikakati ya kufanya vyema mkoani hapa na nchini kwa ujumla hali ambayo inatokana na ushirikiano mzuri na wanachama wa klabu hiyo ambayo wengi wamekwa wakishiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yanayojitokeza.
Mbata ambaye ni mshiriki wa mashindano yanayofanyika nchini akiwa chini ya msoma ramani wake Sultan Chana amewashukuru wanachama wa Iringa Motorsports Club kwa michango yao mbalimbali ndani ya klabu hiyo  na kuwataka kuungana katika kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.
Klabu hiyo yenye wanachama 34 baadhi yao wakiwa ni wafanyabiashara wakubwa mkoani hapa, na wanachama wa kada mbalimbali akiwemo mwanasheria maarufu mkoani hapa Barnabas Nyalusi, Mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni ya Asasa Ahmed Salim na mchezaji wa zamani wa Yanga Ally Msigwa.

No comments :

Post a Comment