Thursday, March 5, 2020

MTATURU ARIDHISHWA NA KASI YA UCHIMBAJI VISIMA JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI



…………………………………………………………………………………………………..
Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekagua shughuli ya uchimbaji kisima katika kijiji cha Unyaghumpi na kushauri Meneja Wakala wa Umeme Vijijini(REA) na wa Shirika la Umeme Nchini(TANESCO)Mkoa wa Singida kufika na kufanya tathmini ili miundombinu ya
maji itapokamilika waweze kufikisha umeme na maji yaweze kwenda kwa wananchi.
Kisima hicho ni miongoni mwa visima 15 vinavyochimbwa na serikali jimboni humo kupitia Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) kwa gharama ya shilingi milioni 505.6.
Akizungumza machi 4 mwaka huu akiwa katika ziara yake kijijini hapo Mtaturu amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kukubali kuchimbwa kisima kwa ajili ya wananchi wote.
“Niwashukuru wananchi kwa moyo wenu huu, na niwaombe Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)kuweka kituo cha kuchotea maji(DP)karibu na familia iliyotoa eneo lililochimbwa kisima,
“Nimshukuru mhe Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli kwa kukubali kutuletea miradi hii ikiwemo kukubali maombi yangu,mara nilipoapishwa Septemba 3 mwaka jana nilioomba shilingi bilioni 2 za kujenga miundombinu ya maji kwa wananchi wetu,nashukuru ombi hilo lilikubaliwa na kazi hivi sasa inaendelea vizuri,”alisema Mtaturu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Musa Mkanga amemshukuru Mbunge kwa kuwapigania wananchi hatimaye sasa visima vinachimbwa ili maji yapatikane.
“Mhe mbunge tunakushukuru sana,ukiacha suala la maji pia usambazaji umeme unaendelea kwenye Kijiji chetu,kwa kweli unatuwakilisha vizuri na kubeba shida zetu na hatimaye matokeo tunayaona,tunamshukuru Rais wetu mpendwa Magufuli kwa kusikia kilio chetu na kutuletea maendeleo” alisema mwenyekiti huyo.
Kwa sasa upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ikungi ni asilimia 41 ambapo baada ya miradi hiyo kukamilika inatarajiwa itaongeza upatikanaji wa maji hadi kufikia asilimia 71 na hivyo kukaribia lengo lililowekwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) la kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa Maji Safi na salama vijijini.

No comments :

Post a Comment