
Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiongozana na Wakuu wa
Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwenda kukagua maeneo mbalimbali
yanayosemekana yanatumika kupitisha wahamiaji haramu,ambapo serikali
imetangaza kuanza operesheni maalumu kudhibiti wahamiaji hao kipindi
hiki nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Afisa Uhamiaji Mkoa Kigoma,
Kamishna Msaidizi, Remigius Pesambili akisoma taarifa ya Utendaji kazi
kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni
(hayupo pichani), wakati wa kikao cha ndani kilichohusiana na utendaji
kazi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi
***************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali
imetangaza kuanza operesheni, doria na misako maalumu ya kuwasaka na
kuwakamata wahamiaji haramu katika sehemu mbalimbali
ikiwemo katika nyumba za kulala wageni, stesheni za mabasi, stesheni
za reli, mahoteli, mialo ya uvuvi pamoja na maeneo yenye muingiliano wa
shughuli za kibiashara hasa vijiji vinavyojishughulisha na shughuli za
kilimo,makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Hayo yamesemwa na
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, mkoani
Kigoma baada ya kikao cha ndani na Wakuu wa Vyombo vilivyopo chini ya
wizara yake ikiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji,
Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) na Idara ya Wakimbizi.
“Nchi yetu
inaelekea katika Uchaguzi Mkuu,kama vyombo vya ulinzi na usalama lazima
tutimize majukumu yetu na sasa tunaanza msako nchi nzima hasa katika
mikoa iliyopo mipakani,tutaimarisha vizuizi vyetu vya barabarani nchi
nzima,tutatoa elimu kwa wananchi wetu jinsi ya kuwatambua watu wasio
raia ambao wameingia nchini bila kufuata utaratibu na kubwa zaidi
tutafanya ukaguzi katika makampuni binafsi na mashirika yasiyo ya
kiserikali” alisema Masauni
“kumekuwepo na
wimbi kubwa la watu kuingia nchini bila kufuata utaratibu,sisi kama
serikali hatukatazi mtu kuingia nchini basi wafuate utaratibu,kila mtu
kwa kada yake anaetaka kuingia nchini kuna utaratibu wake wa kufuata na
serikali haijawahi kumnyima raia yoyote yule wa kigeni fursa ya kuingia
nchini.
Masauni pia
aliwataka wananchi kutowahifadhi au kuwasafirisha watu wasio raia kwani
ni kinyume na sheria na adhabu yake ni kifungo cha muda wa miaka
ishirini au faini ya milioni ishirini au vyote kwa pamoja ikienda
sambamba na kutaifishwa kwa chombo cha usafiri kilichohusika
kuwasafirisha washtakiwa na kwa mwananchi atakaekutwa akimhifadhi au
kumsafirisha mhamiaji haramu adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka
mitatu na faini isiyozidi laki tano au vyote kwa pamoja.
Akizungumza
katika kikao hicho Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma,Kamishna Msaidizi
Remigius Pesambili alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi
Disemba,2019 wamekamata wahamiaji haramu 3.992 na kuchukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria”
“Idara ya
Uhamiaji hapa Kigoma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na
Usalama tumefanikiwa katika mwaka uliopita kuanzia Januari hadi Disemba
kukamata wahamiaji haramu kama ifuatavyo; raia wa Burundi 3,293, Kongo
631, Kenya 12, Uganda 28, Rwanda 16, China 9, Somalia 2 na Msumbiji ,
ambapo jumla yake ni wahamiaji haramu 3,992 na tayari washachukuliwa
hatua na wengine wako magerezani tayari wakitumikia adhabu” alisema DCI
Pesambili
Aliongeza pia
katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2019 raia wa kigeni 1,544
waliondoshwa nchini,815 walipewa amri ya kuondoka,534 walifikishwa
mahakamani,231 waliachiwa huru baada ya kubainika kuwa hawana makosa ya
kuwafikisha mahakamani na 868 walikabidhiwa Idara ya Wakimbizi.
Kuwepo kwa
wahamiaji haramu nchini kunatajwa kushamiri sana katika mikoa iliyopo
mipakani huku upatikanaji wa nyenzo za kutosha ikiwemo magari,elimu kwa
wananchi juu ya kutoa taarifa za wahamiaji katika eneo lao,utoaji wa
vitambulisho vya taifa uelekezewe nguvu hasa zaidi katika mikoa ya
mipakani,vikao vya ujirani mwema baina ya Tanzania na nchi tunazopakana
nazo na utolewaji wa vibali vya wakimbizi ikiwemo kufanyika upewaji wa
uraia vikitajwa uenda vikawa suluhisho la kupunguza uhamiaji haramu.
No comments :
Post a Comment