Waziri wa Katiba na
Sheria Zanzibar, Khamis Juma Maalim
katika Mkutano Mkuu wa Tano wa Wanachama na Wadau wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
ya Zanzibar (ZSSF)
Na Christian Gaya: Majira Ijumaa 06.Machi.2020
HIFADHI ya Jamii ni haki
ya msingi ya kila mwananchi awe mtu mzima au mtoto mdogo popote awapo katika
ulimwengu huu. Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 linasisitiza hayo.
Utekelezaji wa agizo hilo ulitokana na...
Azimio la Shirika la Kazi Duniani
nambari 102 la Hifadhi ya Jamii la mwaka 1952.
“Hifadhi ya Jamii inaweza
kutafsiriwa kwa ujumla kama ni maandalizi au kinga ya kiuchumi na kijamii dhidi
ya dhiki inayosababishwa na kupoteza uwezo au kipato kutokana na umri, maradhi,
kuumia, kazini au kufariki dunia,” anasema Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Khamis Juma Maalim alipokuwa mgeni rasmi siku ya Mkutano Mkuu wa Tano wa Wanachama na
Wadau wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Zanzibar (ZSSF) uliofanyika Februari 26,
2020 kwenye ukumbi wa Uhuru Kariakoo Zanzibar.
Anasema kutokana na
athari kubwa ambazo mwanachama anaweza kuzipata kwa kupoteza kipato, uendeshaji
wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni jukumu la Serikali zote duniani.
“Sekta ya Hifadhi ya
Jamii kwa Zanzibar inayo historia ndefu sana. Sekta hii ilikuwepo kabla ya
Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 lakini
walionufaika wakati huo walikuwa ni wachache tu wale ambao waliobahatika
kufanyakazi za ukarani katika Serikali ya Kikoloni na pia kulikuwa na Hifadhi
ya Jamii za kikabila au madhehebu,” Waziri anazidi anafafanua zaidi.
Anasema tangu 1964
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya jitihada kubwa katika kuendeleza
Hifadhi ya Jamii kwa wananchi wake kupitia mfuko mkuu wa Serikali. Mfumo huu
ulikuwa ndiyo njia kuu ya Hifadhi ya Jamii Zanzibar mpaka mwanzoni mwa miaka ya
1990 wakati Serikali ilipoanza kupambana na hali ngumu ya uchumi. Pia
ilichangiwa na ongezeko maradufu la watu kutoka 300,000 mwaka 1967 hadi 750,000
mwaka 1997.
“Ambapo Mfuko wa Hifadhi
ya Jamii Zanzibar umeanzishwa kwa Sheria Na.2 ya mwaka 1998 ambayo
ilirekebishwa na Sheria Na 9 ya mwaka 2000, pia ilirekebishwa kwa notisi ya
Serikali ya 2004 na kuanzishwa upya kwa Sheria Na 2 ya mwaka 2005 baada ya
kufanyiwa mapitio makubwa. Aidha kwa marekebisho ya karibuni yalikuwa ni mwaka
2016 na utekelezaji ukaanza 2017,”Waziri wa Katiba na Sheria anasema.
Aidha anasema marekebisho
yote hayo yalikuwa na dhamira mbili kuu: Kwanza ni kuendana na mahitaji ya
watumiaji wa sheria kulingana na wakati husika ikizingatiwa sekta hii bado
haijakomaa vizuri. Lakini pili ni kuufanya Mfuko huu kuwa na afya njema ya
uendelevu wake ili wachangiaji na wasimamizi wa mfuko waweze kunufaika.
Pia anasema matukio makubwa
yaliyofanyika ni uzinduzi wa mfumo wa kujichangia katika mfumo wa hifadhi ya
jamii kwa hiari kupitia Benki moja kwa moja. “Hili ni jambo jema ambalo kwa
ulimwengu wa kileo mwananchi hatumii muda mwingi katika foleni au kufuatia
huduma ya fedha eneo la mbali na anapoishi, bali huduma nyingi zinafanywa
kupitia kiganjani au katika meza yako ya nyumbani au afisini. Naamini huduma
hii itawarahisishia wanachama wengi kuweza kuwasilisha michango yao kama
ambavyo tumeona,”anasema.
“Napenda kusema kuwa moja
kati ya kilio cha ulimwengu ni kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii duniani
inawahifadhi wale tu walio katika sekta rasmi na inawatenga wale ambao wamo
katika sekta isiyorasmi,” Waziri anasema.
Anakumbusha ya kuwa uzinduzi
wa Mfumo wa kujichangia kwa hiari (ZVSSS) uliofanyika miaka mitano iliyopita ni
hatua muhimu sana ya kutekeleza kwa vitendo agizo la Shirika la Kazi Duniani-ILO
linalosema “Hifadhi ya Jamii kwa wote”.
“Kuanzishwa kwa Mfumo huu
kunatoa fursa kwa wale wote ambao kwa namna moja au nyengine hawakuweza
kusajiliwa katika mfumo wa sekta rasmi ili kuweza kunufaika kama wanavyonufaika
wenzao katika sekta iliyo rasmi,”anasema.
Anasema mbali na mafao ya
uzeeni pia katika mfuko wa kujichangia kwa Hiari kuna fursa kwa mwanachama
kunufaisha mtoto wake kwa mafao ya elimu. Mwanachama anapata fursa ya kumsajili
mtoto na kumchangia mafao ya elimu kwani elimu ni hazina njema na uwekezaji
mwema kwa mtoto.
“Hivyo basi natoa wito
kwa wananchi wote ambao hawakusajiliwa katika mfumo mkuu, kuitumia fursa hii ya
kujisajili katika Mfumo wa kujichangia kwa hiari ili waweze kunufaika na mafao
kama yale ya uzeeni ambayo wafanyakazi walioajiriwa wananufaika nayo,”waziri wa
katiba na sheria anasisitiza.
Anasema kuanzisha
michuano ya soka ya ZVSSS ni jambo jema ambalo mumeamua kulitumia kama ni nyenzo
ya kutafuta wanachama katika maeneo ambayo michezo inafanyika. Kwangu mie pia
naangalia kwa jicho jengine ambalo bila shaka ni kuendeleza juhudi za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya DK. Ali Mohamed Shein ambayo imekuwa
ikisisitiza suala la mazoezi na michezo kwa jumla.
Anasema tumeona kuna
jitihada ya kuanzisha viwanja vya michezo kila Wilaya, kuwepo na programu
maalum ya kuhuisha michezo nchini, lakini pia hata kuwepo siku maalum kila
mwaka ya kuvikutanisha vikundi vya mazoezi na wanamichezo ili kushirikiana
katika mazoezi ya pamoja na kujadiliana kuendeleza sekata hiyo.
“Hivyo basi ninawapongeza
ZSSF kuanzisha michuano hiyo ikiwa ni miongoni mwa jitihada za kuunga mkono
serikali yenu. Wito wangu kwenu ni kuyaendeleza michuano hiyo lakini pia
kuangalia katika mikoa mengine Unguja na Pemba,” Waziri anasema.
“Napenda kuwakumbusha
waajiri wajibu wao wa kujisajili kuwa mwanachama mchangiaji na kuwasajili
wafanyakazi wao kuwa wanachama wanufaika wa ZSSF na wito huu unawahusu wenyeji
na wageni,” anasema.
Anawakumbusha waajiri wa
sekta binafsi walitekeleze hilo na kuwasilisha michango kwa wakati ili walengwa
wasipate usumbufu unapofika wakati wa kustaafu. Anasema jumuiya ya Waajiri
Zanzibar (ZANEMA) ambao nao ni wadau wakubwa wa mkutano huu hawana budi
kuwakumbusha waajiri juu ya jukumu hili la kisheria ili kujenga mustakbala
mzuri baina ya waajiriwa, ZSSF na waajiri.
“Lakini pia hata Jumuiya
za Wafanyakazi kupitia vikao vyao baina ya Wafanyakazi na waajiri wao, ni
wajibu kuwakumbusha kutekeleza sheria hii ya ZSSF ambayo ni miongoni mwa sheria
za kazi lakini kuwapatia elimu hii ya Hifadhi ya Jamii kwa manufaa yao kwa sasa
wawapo kazini na pia wakati wa kustaafu,”Waziri amesisitiza.
No comments :
Post a Comment