Na Englibert Kayombo, WAMJW, Arusha.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewahakikisha
Watanzania kuwa nchi bado iko salama na hakuna mgonwjwa yeyote mwenye
ugonjwa wa Virusi vya Corona.
Dkt Ndugulile ametoa kauli hiyo
akiwa Jijini arusha katika Ziara zake za kikazi ambapo
waandishi wa
habari walimuuliza juu ya tetesi za uwepo wa ugonjwa huo nchini, pamoja
na kutaka kufahamu ukweli wa taarifa za mtu anayedai kuwa na dawa za
ugonjwa huo.
“Niseme tuu kuwa Tanzania mpaka
sasa hivi bado tuko salama na hakuna mgonjwa yeyoteambaye ameripotiwa na
amethibitika kuwa na ugonjwa” amesema Dkt Ndugulile.
Amesema kuwa Serikali imekuwa
ikifuatilia taarifa mbalimbali za washukiwa na watu wote ambao
tunawahisi kuwa na ugonjwa huo na tumeweza kuwapima na kubaini kuwa
hawana ugonjwa.
“Sambamba na hilo tumeendelea
kuchukua tahadhari mbalimbali na mimi niko katika Mkoa huu wa Arusha na
nitaenda Kilimanjaro kwenda kuangalia utayari” amesmea Dkt. Ndugulile na
kuendelea kusema “ Nimepita hapa leo nimeongea na uongozi na
nimeridhika na maandalizi ambayo tunayo hapa katika Mkoa huu wa Arusha
katika kudhibiti ugonjwa huo” Ameeleza Dkt. Ndugulile
Akijibu kuhusu mtu ambaye anasema
kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa huo ambaye anajulikana kwa jina la
Mosses Mollel maarufu kwa jina la “Nabii namba saba” aliyetoa taarifa za
kuwa na dawa yenye uwezo wa kutibu virusi vya corona, Dkt Ndugulile
amesema kuwa anazo taarifa za mtu huyo ambazo zimesambaa kwenye mitandao
ya kijamii na vyombo vya habari akijitangaza kuwa anayodawa ya kutibu
ugonjwa huo na kumtaka athibitishe kauli yake.
“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya
huyo mtu anayejiita Nabii Saba kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa wa
Corona ,ila hapa kwetu Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huyo
,tunachotaka huyo mtu atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa
wa Corona” Amesema Ndugulile
Ameongeza kuwa iwapo atashindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua Kali za kisheria.
Amesema hadi sasa Serikali imetuma
wataalamu wake kwenda kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali Vya kutoa
huduma ya Tiba na kujitangaza kuwa anatoa Huduma ya kutibu ugonjwa huo
hatari ambao hadi sasa mataifa bado yanahaha kusaka Tiba ya ugonjwa
huo.
Nabii Namba Saba ambaye ni mkazi
wa Ngaramtoni Wilayani Arumeru,Mkoani Arusha amekuwa akijitangaza kuwa
anayo dawa ya kutibu ugonjwa huo wa virusi vya corona na kuweka
mawasiliano yake kwenye mitandao .
Dkt. Ndugulile amesema kuwa mtu
yeyote anayetoa tiba asili na mbadala kwanza ni lazima asajiliwe na
mamlaka husika ambayo ni Wizara ya Afya, pili lazima dawa zake ziwe
zimesajiliwa na Wizara ya Afya na kusisitiza kuwa nabii huyo pia
anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.
“Tuepuke kutoa kauli ambazo
zinakwenda kuchanganya jamii, na endapo tutabaini mtu huyu hana sifa
ambazo anasema kuwa nazo tutamchukulia hatua za kisheria” Amesema Dkt.
Ndugulile.
No comments :
Post a Comment