Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi
Maryprisca Mahundi akizungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa
Idris Kikula pamoja na timu yake (hawapo pichani) ofisini kwake mara
baada ya kuwasili wilayani Chunya kwa ajili ya ukaguzi wa shughuli za
madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 13
Februari, 2019.
Kutoka kulia waliosimama
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na Mkuu wa Wilaya ya
Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi wakiangalia namna uchenjuaji wa
dhahabu unavyofanyika katika Kiwanda cha Uchenjuaji Dhahabu cha PM
kilichopo katika eneo la Makongolosi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula (kushoto) akitoa maelekezo kwa Afisa Madini Mkazi
wa Chunya, Mhandisi Godson Kamihanda (wa pili kulia) katika Kiwanda cha
Uchenjuaji Dhahabu cha PM kilichopo katika eneo la Makongolosi Wilayani
Chunya Mkoani Mbeya. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi
Maryprisca Mahundi.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula (kushoto) akiangalia namna upimaji wa madini ya
dhahabu unavyofanyika katika kituo cha ununuzi wa madini cha
Makongolosi kilichopo Wilayani Chunya Mkoani Mbeya. Kulia ni mmoja wa
wauzaji katika duka linalomilikiwa na Sitta Malase, Philemon Boniphace.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi
Maryprisca Mahundi (mbele) akimwongoza Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula ( wa pili) kwenye ziara katika Kampuni ya
Uchenjuaji wa Dhahabu ya Otter iliyopo katika eneo la Makongolosi
Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi
……………………………………………………………………………………………..
Na Greyson Mwase, Chunya
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Chunya, Godson Kamihanda ameeleza kuwa kuanzia
kipindi cha mwaka wa
fedha 2019/2020 kilichoanza Julai, 2019 hadi Januari 31, 2020, ofisi
yake imefanikiwa kukusanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 24.173
ikiwa ni sawa na asilimia 128 ya lengo la ofisi kwa mwaka wa fedha
2019/2020 ambalo lilikuwa ni shilingi bilioni 18.861.
Kamihanda ameeleza hayo leo
tarehe 13 Februari, 2020 kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula Wilayani Chunya mkoani Mbeya yenye lengo la
kufuatilia maelekezo aliyoyatoa katika ziara yake aliyoifanya awali
nchini kati ya tarehe 29 Oktoba, 2019 na tarehe 03 Novemba, 2019,
kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero
mbalimbali za wachimbaji wa madini.
Alisema kuwa maduhuli
yamechangiwa na uanzishwaji wa Soko la Madini Chunya pamoja na vituo
vidogo tisa vya ununuzi mdogo wa madini vilivyopo katika maeneo ya
Makongolosi, Matundasi, Itumbi, Chunya Mjini, Sangambi, Godima, Igundu
na Shoga na vituo vingine vilivyopo katika maeneo ya Mkwajuni na Saza
katika Wilaya ya Songwe.
Aliongeza kuwa ili
kuhakikisha biashara ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye
makusanyo ya maduhuli Chunya, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ofisi yake
ilitoa leseni 105 za ununuzi mdogo wa madini ya dhahabu kwa wale ambao
walikubali kukaa katika vituo vidogo vya ununuzi wa madini.
Alisema pia ofisi yake ilitoa
leseni 34 za ununuzi mkubwa wa madini katika kipindi cha kuanzia mwezi
Julai, 2019 hadi Januari, 2020 tofauti na mwaka 2018/2019 ambapo ni
leseni tisa tu zilitolewa.
Alisema kuwa, kukua kwa
biashara ya madini Chunya kumetokana na elimu ya uhamasishaji ambayo
imekuwa ikifanywa na Ofisi yake tangu kuzinduliwa kwa Soko la Madini
Chunya mnamo tarehe 02 Mei, 2019 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,
Profesa Simon Msanjila ikiwa ni siku tano baada ya Rais John Magufuli
kutoa siku saba za kuhakikisha soko husika limefunguliwa.
Katika hatua nyingine,
Kamihanda aliongeza kuwa ili kuhakikisha usimamizi unaimarishwa kwenye
vituo vya ununuzi wa madini, ofisi yake ilishirikisha viongozi wa kata
ambao wamekuwa mstari wa mbele kusimamia biashara ikiwa ni pamoja na
kuwasilisha taarifa zote kwa maafisa wa Tume ya Madini ambao wamekuwepo
kwenye soko kuu la madini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya,
Mhandisi Maryprisca Mahundi alisema kuwa Ofisi yake imekuwa ikisimamia
kwa karibu sana suala la usalama kwenye biashara ya madini ikiwa ni
pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa madini.
Alisema kuwa, wananchi
wameanza kuwa na uelewa mkubwa wa umuhimu wa kutumia masoko ya madini na
kuwa walinzi wa rasilimali za madini huku wakilipa kodi mbalimbali
Serikalini.
Mbali na kupongeza juhudi
zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John
Magufuli kwenye Sekta ya Madini, alisema kuwa kabla ya maboresho kwenye
Sekta ya Madini wachimbaji wa madini wasio waaminifu walikuwa
wakitorosha madini hali iliyoikosesha Serikali mapato yake.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa
Tume ya Madini alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhandisi Maryprisca
Mahundi na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Chunya, Mhandisi Godson
Kamihanda kwa usimamizi mzuri wa masoko ya madini hali iliyopelekea
maduhuli ya Serikali kupaa.
Akielezea mikakati ya Tume ya
Madini katika kuboresha huduma kwenye Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa
Mikoa, Profesa Kikula alisema Serikali imeongeza wataalam kwenye Ofisi
za Madini, vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari na mashine za kupima
madini kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa.
Aidha, Profesa Kikula alifanya
ziara katika vituo vya ununuzi wa madini vilivyopo katika eneo la
Makongolosi na kuwataka wafanyabiashara wadogo kuwa wazalendo na
waaminifu kwenye biashara ya madini huku wakilipa kodi mbalimbali
Serikalini.
Pia Profesa Kikula alitembelea
Kampuni za Uchenjuaji wa Dhahabu za PM na Otta Mining Limited
zilizopo katika eneo la Makongolosi na Kampuni ya Uchimbaji na
Uchenjuaji wa Dhahabu ya Sunshine iliyopo katika eneo la Matundasi
Wilayani Chunya Mkoani Mbeya
No comments :
Post a Comment