*************************
NA EMMANUEL MBATILO
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa TAKUKURU imekamilisha Uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na
aliyekuwa
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ,Thobias Andengenye.
Uchunguzi huo kwa watuhumiwa hao
ulihusu kusainiwa kwa mkataba wa ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto
na Uokoaji wenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni moja kinyume cha
sheria.
Akizungumza na Wanahabari Jijini
Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo , Brig.Jen.John
Mbungo amesema kuwa baada ya maelekezo ya Mhe.Rais, TAKUKURU ilianzisha
uchunguzi kwa kukusanya vielelezo na kufanya mahojiano na watu
mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la zimamoto na
Uokoaji, Watumishi wa Serikali pamoja na makampuni husika katika MoU
hiyo.
“Uchunguzi huu ulilenga
kuthibitisha iwapo kuna uwezekano wa baadhi ya watumishi kufanya uzembe
kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutozishauri Mamlaka zao
kuhusu taratibu mbalimbali za usajili wa makampuni pamoja na
uzingatiwaji wa sheria ya Ununuzi wa Umma?”. Amesema Brig.Jen.Mbungo.
Aidha Brig.Jen.Mbungo amesema kuwa
katika makosa hayo yanaangukia katika makosa ya ujumu uchumi ambayo
kisheria TAKUKURU haitakuwa na mamlaka ya kuyafikisha mahakamani
.Kitakachofanyika ni kuwasilisha jalada la uchunguzi katika ofisi ya
Taifa ya Mashitaka ili kwa kibali chake watuhumiwa waweze kufikishwa
mahakamani.
Pamoja na hayo Brig.Jen.Mbungo
amesema kuwa wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha uchunguzi huo
ambapo baada ya wiki moja watakuwa tayari kwa kukabidhi jalada hilo
katika ofisi ya Taifa ya Mashitaka.
No comments :
Post a Comment