…………………………………………………………………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma.
Katika hali ya kawaida herufi
huunda neno na maneno huunda sentensi nayo sentensi huunda kikundi cha
maneno. Kwa kawaida neno ni tamko mojawapo miongoni mwa mengi ambalo
mtu
hulitamka katika mchakato wa mazungumzo unaopelekea iwepo misemo ambayo
ni fungu la maneno yenye maana mahususi ili kutoa fundisho kwa jamii.
Kwa mantiki hiyo, semi ni maneno
yanayozungumzwa na watu yanayoleta maana mahususi katika lugha
inayozungumzwa katika eneo fulani. Kiswahili ikiwa lugha ya Taifa la
Tanzania kimekuwa pia lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya
nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na lugha ya Umoja wa Afrika (AU). Bila
kusahau kuwa ni lugha ya kufundisha katika shule, taasisi na vyuo vikuu
katika mataifa mbalimbali duniani.
Watafiti wa mbalimbali duniani
katika tafiti zao wanabainisha kuwa lugha ya Kiswahili inashika nafasi
ya kumi katika lugha elfu sita zinazozungumzwa na watu wengi duniani
ambapo kwa nchi za Afrika kinashika nafasi ya pili kwa kuongelewa na
watu wengi Barani humu.
Tafiti wa wataalamu wa lugha
kutoka Umoja wa Nchi za Afrika unabainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2063
lugha ya Kiswahili ndiyo itakuwa lugha kuu ya mawasiliano katika nchi
zote za Afrika.
Ukuaji na utambuzi huu wa
Kiswahili katika Afrika na duniani kote unaipa heshima Tanzania ikiwa
ndio kitovu cha Kiswahili kuwa lugha maridhawa, adhimu na yenye ubora wa
kipekee yenye msamiati unaofaa kufundishia mataifa mbalimbali duniani.
Tanzania ikiwa nchi Mama kwa lugha
hiyo, haina budi kuwa mstari wa mbele katika kutumia maneno ya
Kiswahili sahihi na fasaha. Kutokana na sababu hiyo, Serikali imeamua
kusisitiza matumizi sahihi ya Kiswahili haswa katika misamiati yake.
“Kumekuwa na matumizi mabaya ya
maneno ‘Kisimbuzi’ na ‘King’amuzi’ Serikali haiwezi kufumbia macho watu
au taasisi ambazo zinaharibu matumizi sahihi ya maneno haya ama kwa
makusudi ama kwa kutofahamu.”Anasema Dkt Harrison Mwakyembe, Waziri
Mwenye dhamana ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Dkt. Mwakyembe ameendelea
kulipigia chapuo suala hili kwenye ziara zake za kikazi katika mikoa
Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mwanza, Singida na Tanga ambapo alipata
fursa ya kuzungumza na wadau wa habari pamoja na wa utamaduni.
“Watanzania tuwe mfano kwa kutumia
Kiswahili fasaha ili kuudhihirisha ulimwengu kuwa Kiswahili kitovu
chake ni Tanzania.” Aliongeza Waziri Mwakyembe katika ziara zake
alizozifanya hivi karibuni.
Aidha, akiwa katika kongamano la
Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Wanafunzi na Wahitimu wa Kiswahili
Vyuo Vikuu na vya Kati Tanzania (CHAWAKITA) Januari 4, 2020 katika Chuo
Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) cha jijini Mwanza, Dkt.
Mwakyembe alibainisha umuhimu wa vyombo vya habari vya Tanzania kuwa
mstari wa mbele katika kusimamia matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Kwa umahiri wa hali ya juu Waziri
Mwakyembe alitoa somo la Kiswahili kwa matumizi sahihi ya maneno haya
huku washiriki wakimsikiliza kwa umakini na shabaha ya Serikali ni kuwa
baada ya ufafanuzi huo makosa yaliyokuwa yakifanyika awali kutojirudia.
Alisema kuwa kwa mujibu wa Kamusi
Kuu ya Kiswahili neno “Kisimbuzi” lina maana ya kifaa kinachotumika
kufichua alama za kielektroniki zilizofichwa ili ziweze kusikika na
kuonekana kupitia kwenye simu, televisheni, faksi na intaneti kwa
kutumia mfumo wa dijiti.
Aliongeza kuwa kamusi hiyo hiyo
neno “King’amuzi” maana yake ni kifaa kinachotumika kufichua vitu
vilivyofichwa au kupotea aghalabu mabomu yaliyofukiwa ardhini, madini na
vito vya thamani au ni kitu kinachotambua vitu au hali ya hatari kama
vile moshi, moto na mazingira mengine ya hatari.
Waziri Mwakyembe alisisitiza kuwa
imezuka kasumba ambayo imejengeka miongoni mwa watumiaji wa lugha ya
Kiswahili vikiwemo vyombo vya habari ambavyo vinatumia vibaya lugha ya
Kiswahili ama kwa makusudi ama kwa kutokujua kutumia.
“Kupitia kongamano hili, naliagiza
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuvionya mara moja baadhi ya
vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vinara wa matumizi mabaya ya neno
‘king’amuzi’ badala ya neno ‘kisimbuzi’.” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Ni ukweli usiopingika ukisikiliza
vyombo vya habari vya redio, televisheni na magazeti pamoja na mitandao
ya kijamii ikiwemo Face Book, Twitter, Instagram na mitandao mingine ya
kijamii. Maneno haya ‘Kisimbuzi’ na ‘King’amuzi’yanatumika ndivyo sivyo,
ni vema vyombo vya habari vichukue nafasi yake ya msingi ya kuelimisha
jamii juu ya matumizi sahihi ya maneno hayo.
Katika kongamano hilo, Waziri
Mwakyembe alikuwa Mgeni Rasmi ambapo alisisitiza kuwa nafasi ya Lugha ya
Kiswahili kuwa kati ya Lugha kumi bora duniani, kuna haja kubwa ya
kuithamini, kutunza na kuiendeleza ili ikue zaidi.
Kutokana na uhitaji wa lugha ya
Kiswahili kwa mataifa mengine, Watanzania wanafursa ya kusoma lugha hiyo
ili kupata wataalamu wa kukifundisha Kiswahili sanifu na fasaha,
uhariri na ukalimani. Hii ni fursa kwa wakufunzi, wahadhiri, wataalamu
waliopo katika sekta ya Kiswahili ama wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma
somo la Kiswahili kuchukua hatua za makusudi ili waweze kuingia kwenye
kada mbalimbali zilizopo kwenye ya lugha ya Kiswahili.
Pia alitilia mkazo juu ya umuhimu
wa wajuzi wa lugha yetu kujua kutumia vyombo vya kisasa vya kufundishia
lugha ya Kiswahili katika muktadha mbalimbali iwe vyuoni, kwenye
ukalimali na maeneo mengine.
Miongoni mwa washiriki wa
kongamano hilo ni Mwakilishi wa BAKITA ambaye pia ni Mhadhiri Chuo Kikuu
cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Dkt. Nestory Ligembe alimshukuru
na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli na Waziri mwenye dhamana na Lugha ya Kiswahili Dkt.
Harrison Mwakyembe kwa uongozi wao thabiti ambao umeleta mafanikio
makubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya
nchi.
Akisoma risala kwa niaba ya Chama
cha Wanafunzi na Wahitimu wa Kiswahili Vyuo Vikuu na Vya Kati Tanzania
(CHAWAKITA) tawi la SAUT Mwenyekiti wa chama hicho Tumaini Masanja
amesema kuwa wanawajibu wa kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ngazi ya
Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, kukuza vipaji vya wanafunzi katika lugha
ya Kiswahili, kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati katika
suala la kuithamini na kuendeleza lugha ya Kiswahili na kuitangaza ndani
na nje ya nchi.
Kongamano liliongozwa na kauli
mbiu “Kiswahili Urithi wetu kwa maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania
kwa kuwa chimbuko lake ni Tanzania” kwa lengo la kuendeleza kampeni ya
kukuza na kuendeleza Kiswahili.
Ni muda muafaka sasa kila mwenye
taaluma ya Kiswahili aone ana mchango katika kukuza, kuhifadhi na
kuendeleza lugha ya Kiswahili. Soko la lugha hii adhimu sasa limevuka
mipaka ya nchi za SADC zikiongozwa na Afrika Kusini iliyoonesha uhitaji
wa walimu wa Kiswahili.
Rais Dkt. Magufuli ameonesha njia,
ni wakati sasa wa kutumia fursa hiyo, wakati ndio huu, tumia Kiswahili
katika kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na hatimaye uchumi wa
taifa.
No comments :
Post a Comment