Friday, February 21, 2020

MGALU AITAKA EWURA KUHARAKISHA UANDAAJI KANUNI KWA WAWEKEZAJI BINAFSI WA UMEME



Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu akiwasikiliza wananchi wa kijiji cha Matipwili kata ya Mkange, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa pwani alikuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme.
Mwanakijiji wa kijiji cha Matipwila kilichopo kata ya Mkange, Wilaya ya bagamoyo, Mkoa wa Pwani akiuliza mwaswali kwa Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.
Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu akiongea na wananchi wa kijiji cha Matipwila kilichopo kata ya Mkange, Wilaya ya bagamoyo, Mkoa wa Pwani alipokuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme.
………………………………………………………………………………………………………
Hafsa Omar-Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, imeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma  ya
Nishati na Maji(EWURA) kuharakisha uandaaji wa kanuni ambazo zitatumika kudhibiti bei za umeme ambazo zitatumiwa na wawekezaji binafsi wa umeme nchini.
Ameyasema hayo, Februari 20,2020 wakati alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya wananchi ambao walikuwa wakilalamikia bei kubwa ya umeme wanaotozwa na Mkandarasi wa kampuni ya Husk Power iliyopo katika kijiji cha Matipwili kata Mkange, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Alisema, Ewura inatakiwa kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwa haraka ili wawekezaji hao wadogo, wapate muongozo huo ambao utawasaidia kufanya kazi kwa kufuata sharia za nchi bila ya kujichukulia maamuzi ya kujiwekea bei za juu ambazo zinawaumiza Watanzania wa kipato cha chini.
Alifafanua kuwa, Serikali ilitoa fursa kwa wawekezaji hao kuwapelekea umeme Watanzania ambao wapo katika maeneo ambayo yapo mbali na gridi ya Taifa na Serikali iliamua kutoa ruzuku ili wawekezaji hao watoe bei nafuu ya umeme kwa Watanzania wa kipato cha chini.
“Ni kweli wao wamewekeza miundombinu yao hapo lakini haiwezekani 5000 itumike kwa siku, haiwezekani kabisa, pia haiwezekani laki tatu na nusu iwe bei ya mtumiaji wa kioski kweli hiyo hapana, laki tatu na nusu ni umeme unaotumika kwenye kiwanda cha saizi ya kati lakini sio kioski” alisema Mgalu 
Alieleza kuwa, Serikali inajukumu la kuwalinda watumiaji wa Nishati nchini, kwa kuzingatia jukumu hilo, inawakumbusha wawekezaji nchini kuwa bei ya kunganisha umeme vijijini ni 27000 na kuwataka wawekezaji hao kupunguza gharama za undeshaji wa kampuni zao ili waweze kujiendeshe kwa kupata faida kwenye kampuni zao.
“Tunataka wapunguze gharama za uendeshaji watumie wataalamu wa ndani, watumie vifaa vya ndani ili gharama za uendeshaji zishuke ili watanzania hawa wapate nafuu vyenginevyo  gharama za umeme zisiposhuka sisi tutakwenda hata maeneo ambayo tulisema waende wao watakosa hii fursa kwasababu sisi hatutakubali bei kama hizo”alisema Aidha,alimtaka mkandarasi huyo kukutana na Meneja wa TANESCO mkoa wa Pwani ili kujadiliana na kuzipitia tena bei za umeme  ambazo zinatumiwa na mkandarasi huyo, ili kupatikane uwiano wa bei  za umeme vijijini  ambazo zinatawanufaisha Watanzani wote ili waweze kujiletea maendeleo.

No comments :

Post a Comment