
Naibu Waziri wa
Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo
tarehe 3 Februari 2020 wakati wa mkutano wa kumi na nane.
……………………………………………………………………………………….
Na Mathias Canal, Wizara ya kilimo-Dodoma
Kutokana na
kuwepo kwa upungufu wa pembejeo nchini, Serikali imechukua hatua
mbalimbali za
kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wingi ili
kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi.
Hatua hizo ni
pamoja na; kutoa vibali kwa wasambazaji wakubwa wa mbolea kuagiza nje ya
mfumo wa BPS kutokana na mahitaji ya wakulima na soko ambapo tani
200,000 zimeagizwa na hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020; Kutoa kibali
cha kuagiza tani 45,000 kwa Umoja wa wasambazaji na wauzaji wa pembejeo
za kilimo; na kuagiza mbolea tani 43,000 kwa kutumia mfumo wa BPS
ambapo mbolea hiyo imeanza kusambaza nchini tangu tarehe 28 Januari,
2020.
Naibu Waziri wa
Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo tarehe 3 Januari 2020
bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kavuu
Mhe Dkt. Pudeciana Wilfred Kikwembe aliyetaka kufahamu serikali ina
mpango gani juu ya ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu na
mbolea ambazo huwasababishia wakulima hasara.
Mhe Mgumba
amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha
mifumo ya uzalishaji, udhibiti na usambazaji wa pembejeo nchini ambapo
sekta ya Umma na binafsi zitashirikishwa na kuhamasishwa kuzalisha
pembejeo nchini ili kukidhi mahitaji.
Kuhusu upungufu
wa mbolea nchini Mhe Mgumba amesema kuwa umechangiwa na sababu
mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupatikana kwa mahitaji kutoka kwa
Makampuni ya mbolea hapa nchini, kuongezeka kwa matumizi ya mbolea
kutokana na bei nzuri ya mazao kwa msimu wa 2018/2019; kuongezeka kwa
kilimo cha kibiashara baada ya Serikali kuwahakikishia wakulima kuwa
haitafunga mipaka na kuingilia upangaji wa bei za mazao ya kilimo na
kuwepo kwa mvua nyingi ambazo zimesababisha kuongezeka kwa viwango vya
matumizi ya mbolea kwa wakulima.
Katika msimu wa
2019/2020 upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbegu bora hadi kufikia
Desemba, 2019 ni tani 71,155.13. Kati ya hizo,
tani 58,509.9 zimezalishwa nchini, tani 5,175.79 zimeingizwa kutoka nje
ya nchi na tani 7,469.44 ni bakaa ya msimu 2018/2019.
Aidha,
upatikanaji wa mbolea hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020 ni tani
410,499 zikijumuisha tani 92,328 za UREA na tani 84,311 za DAP. Kati ya
hizo tani 225,417 zimeingizwa kutoka nje ya nchi, tani 16,685
zimezalishwa ndani ya nchi na tani 168,397 ni bakaa ya msimu wa
2018/2019.
No comments :
Post a Comment