
Naibu Waziri wa
Kilimo Mhe Hussein Bashe (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo
tarehe 3 Februari 2020 wakati wa mkutano wa kumi na nane.
Na Mathias Canal, Wizara ya kilimo-Dodoma
Serikali
imewahakikishia wakulima wa Pamba nchini kuwa
itaendelea kufuatilia
upatikanaji wa viuadudu vya zao la pamba na kuhakikisha vinawafikia
wakulima kwa wakati.
Naibu Waziri wa
Kilimo Mhe Hussein Bashe ameyasema hayo tarehe 3 Februari 2020 wakati
akijibu swali la swali la Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mhe Joseph
Kasheku Msukuma aliyetaka kufahamu serikali inampango gani kupeleka dawa
za kuuwa wadudu wa Pamba kwani zinazopatikana huwa ni chache.
Bashe amesema
kuwa kama sehemu ya utekelezaji wa hamasa za kilimo cha Pamba, katika
msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 eneo la ekari 1,488,406 lililimwa na
kuzalisha kiasi cha tani 132,961. Chupa milioni 4.6 za viuadudu zenye
thamani ya shilingi bilioni 16.8 na vinyunyizi 15,300 vyenye thamni ya
shillingi milioni 462 vilinunuliwa na kusambazwa mwaka huo.
Aidha, katika
msimu wa 2018/2019 eneo la ekari 1,865,000 lililimwa na kuzalisha kiasi
cha tani 222,725 ambapo chupa milioni 6 za viuadudu vyenye thamani ya
shilingi bilioni 29 na vinyunyizi 23,000 vyenye thamani ya shilling
bilioni 1.8 vilinunuliwa.
Vilevile, katika
msimu wa 2019/2020 eneo la ekari 1,786,890 lililimwa na kuzalisha kiasi
cha tani 350,473 ambapo chupa milioni 8.2 zenye thamani ya shilingi
bilioni 41 na vinyunyizi 20,000 vyenye thamani ya shillingi bilioni 1.6
vilinunuliwa.
Mhe Bashe amesema
kuwa katika msimu wa 2017/2018 jumla ya ekapaki 965,300 na vinyunyizi
3,302 vilisambazwa katika Mkoa wa Geita. Aidha, jumla ya ekapaki 736,345
na vinyunyizi 3,020 vilisambazwa katika mkoa huo katika msimu wa
2018/2019. Kwa msimu wa 2019/2020 Mkoa wa Geita umekwisha kusambaziwa
kiasi cha ekapaki 8,748 na usambazaji bado unaendelea.
Bashe amesema, si
sahihi kusema kuwa Serikali inahamasisha kilimo cha pamba ikiwa haina
uwezo wa kupeleka sumu za kuulia wadudu na hata zinapopatikana huwa ni
chache. Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao likiwemo zao la
pamba ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali.
Akizungumzia
uchache wa viuadudu vya zao la pamba Mhe Bashe amesema kuwa umechangiwa
na baadhi ya wakulima kutumia viuadudu katika kupulizia mazao mengine
kama vile mahindi na viazi vitamu ili kudhibiti viwavijeshi vamizi.
Vilevile, amesema
kuwa kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji katika
baadhi ya maeneo ukiwemo Mkoa wa Geita ambapo viuadudu havikupelekwa kwa
wakulima na badala yake kuuzwa katika maduka ya pembejeo kinyume na
taratibu za usambazaji wa viuadudu vya zao la pamba.
Ameongeza kuwa
Watu zaidi ya 12 walikamatwa na kati yao 9 walifunguliwa mashtaka ambapo
watu nane (8) walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja.
No comments :
Post a Comment