…………………………………………………………………………………….
Na ASP Lucas Mboje, DSM
KAMISHNA Jenerali mpya wa Magereza
nchini, Suleiman Mzee(pichani) amewataka Maofisa na askari wote wa
Jeshi la Magereza kumpa ushirikiano katika uongozi wake ili aweze
kusimamia vyema maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kwa Jeshi hilo ikiwemo jukukumu la kujitegemea kwa
chakula cha wafungwa magerezani.
Akizungumza na Maofisa, askari na
watumishi raia wa Jeshi hilo katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya
Magereza, jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema
kuwa anayomatarajio makubwa ya kuhakikisha kuwa Jeshi la Magereza
linakuwa na miradi mingi ya uzalishaji mali ili kuwezesha kujitegemea
badala ya kutegemea bajeti kuu ya Serikali.
“Ni lazima tuzalishe kwa wingi na
kila gereza lizalishe kulingana na fursa zilizopo ikiwa tunataka
kujiwekea mazingira ya kuaminika. Pia, tuhakikishe kuwa utaalam wetu
katika nyanja mbalimbali lazima uwe na manufaa Jeshini”, amesisitiza
Jenerali Mzee.
Aidha, Kamishna Jenerali Mzee
ameongeza kuwa ni vyema maofisa na askari wa Jeshi hilo wakazingatia
utii, uaminifu pamoja na uhodari katika kazi ili kuyafikia matarajio
hayo makubwa ndani ya Jeshi.
“Mkizingatia utii, uaminifu pamoja
na uhadari katika kazi naamini matokeo chanya yataonekana katika muda
mfupi kwani upo uwezekano wa kufanya mambo makubwa ambayo yataliletea
heshima na sifa Jeshi letu la Magereza”, amesema Jenerali Mzee.
Kuhusu mafunzo mbalimbali kwa
maafisa na askari, amesema kuwa atapitia mitaala ya mafunzo ili kuona
kama inaendana na mazingira yaliyopo pamoja na kuifanyia maboresho
mbalimbali kwani mafunzo ni nguzo muhimu katika kujenga nidhamu kwa
maafisa na askari.
Kwa upande wake aliyekuwa Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(sasa Balozi Mteule)
alimpongeza Jenerali Mzee kwa kuteuliwa na Rais kushika nafasi hiyo na
alibainisha baadhi ya changamoto ambazo zinalikabili Jeshi hilo ikiwemo
uchakavu wa makazi ya askari.
“Nafurahi kuwa naliacha Jeshi la
Magereza likiwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na kuwa na baadhi ya
changamoto mbalimbali ikiwemo makazi duni ya askari, naamini changamoto
hizo utazifanyia kazi kwani tayari tulikwishaanza kuchukua hatua”,
amesema Mhe. Balozi Kasike.
Jeshi la Magereza linamiliki ardhi
yenye ukubwa wa ekari 326,205 Tanzania Bara, kati ya hizo ekari 151,350
zinafaa kwa shughuli za kilimo na mifugo. Eneo linalotumika kwa
shughuli za kilimo kwa sasa ni ekari 20,580 pekee sawa na asilimia 13.60
ya eneo linalofaa kwa shughuli za kilimo. Jeshi hilo likijipanga
kimkakati linaweza kujilisha, kuongeza pato serikalini pamoja na kufanya
mapinduzi makubwa ya kilimo hapa nchini.
No comments :
Post a Comment