Saturday, February 1, 2020

NDUGAI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI MAHAKAMA IWE NA RASILI MALI ZA KUTOSHA



…………………………………………………………………………………….
Na Magreth Kinabo- Mahakama
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job  Ndugai amesema  Bunge litashirikiana na Serikali  kuhakikisha Mahakama ya Tanzania inapate rasilimali za kutosha ili
iweze kutekeleza  majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati.
 Akizungumza leo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika  uzinduzi wa Wiki ya  Utoaji  Elimu ya Sheria iliyoambatana na   matembezi  maalum ya kilomita tano yaliyoanza kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu  Dodoma hadi kwenye maonesho, ambayo yanaendelea katika   Viwanya vya Nyerere Square, aliipongeza Mahakama kwa maonesho mazuri.
‘’Bunge litashirikiana na Serikali, kuhakikisha  Mahakama inapata rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati,’’ alisema Spika.
Aidha Spika huyo    alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma,  wafike katika viwanja   hivyo ili wajue  haki zao na kupata elimu ya sheria kwa kuwa Mahakama si sehemu ya kuogopwa.‘ wananchi wakielewa haki zao hawatadanganywa,’ alisisitiza.  
Spika huyo, aliipongeza Mahakama kwa kauli mbiu yake ya mwaka huu inayosema ‘Uwekezaji  na Biashara: Wajibu   wa Mahakama na Wadau  kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’ Kwa kuwa inasaidia kufikisha dhamira ya Serikali  ya Awamu ya Tano kujenga uchumi imara  na viwanda.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa  Dodoma, Dkt. Bilinith  Mahenge alitoa shukrani kwa Mahakama  kujenga majengo ya   Mahakama Jumuishi na  Ofisi za Makao Makuu jijini Dodoma.
Katika  maonesho hayo, Spika pia alizindua Vitabu Vitatu vya Muongozo wa Kusikiliza Mashauri  Mahakamani vinatumika  Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mkoa na Mahakama Kuu ( A hand book for Magistartes in Primary Courts, A guick reference for Magistrates in the District Court and Courts of Resident Magistrtes in Tanzania and  Bench Book for Judges in Tanzania).
Akizungumzia kuhusu vitabu hivyo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer  Feleshi,  alisema vitabu vimeshawekwa kwenye Tovuti ya Mahakama ya Tanzania.
Wiki ya hiyo imeanza Januari 31, mwaka huu na inatarajia kumalizika Februari 5, mwaka huu, ambapo kilele chake cha Siku ya Sheria nchini kitafanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu J. K. Nyerere.
Mgeni rasmi katika kilele hicho, anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

No comments :

Post a Comment