Friday, February 7, 2020

MILIONI 22 ZAPUNGUZA UHABA WA MADARASA, MADWATI SHULE YA MABATINI A



Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Sibtain Meghjee, akiwa ameketi na wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Mabatini A baada ya kukabidhi madawati na chumba kimoja cha darasa kwa ufadhili wa  taasisi hiyo.
………………………………………………………………………………………………………….
NA  BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation (TD & CF) Tawi la Tanzania imekabidhi jengo la
chumba kimoja cha darasa na madawati 20 kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mabatini A, wilayani Nyamagana.
Jengo hilo limejengwa na taasisi hiyo kwa gharama ya sh. milioni 20 ufadhili wa Walfare Aid International Organasation kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto za elimu ambapo madawati, vifaa vya kufundishia, meza na kiti cha mwalimu vikigharimu sh. milioni 2.2.
Akikabidhi jengo hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi, jana Mwenyekiti wa TD & CF Sibtain Meghjee alisema msaada huo umelenga kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa inayoikabili Shule ya Msingi Mabatini A.
Alisema wanafunzi wa shule hiyo ambao ni viongozi wa kesho watanufaika na  darasa hilo kielimu kwa miaka mingi ijayo kutokana na kusoma kwenye mazingira bora na rafiki na kuishukuru taasisi ya Walfare Intenrational Organasation kwa ufadhili wa fedha za mradi huo unaolenga kuinua na kuboresha elimu nchini.
“Tunaishukuru serikali ya mkoa na watendaji wake kwa ushirikiano wa dhati kwetu The Desk & Chair Foundation kuweza kutekeleza miradi na  shughuli mbalimbali za kijamii.Tutaendelea kutekeleza miradi ya kijamii ili kuunga mkono jitihada za serikali kwenye sekta ya afya, elimu na maji,”alisema Meghjee.
Alisema TD & CF baada ya kukabidhi darasa hilo kwa uongozi wa serikali na shule, itaanza mchakato wa kujenga chumba kingine mara baada ya wafadhili kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande wao Wendo Meshack na mwenzake aliyefahamika kwa jina moja la Christopher kwa niaba ya wanafunzi wa darasa la saba  wa shule ya Msingi Mabatini A, waliishukuru TD & CF waliahidi kusoma kwa bidii na watafaulu wote ili kurudisha fadhila kwa taasisi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk. Nyimbi alisema wananchi na wazazi wanapaswa kushiriki maendeleo ya elimu na kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili kuunga mkono serikali  na kuwafanya watoto kufanya vizuri na kufaulu masomo.
Alisema shule za Wilaya ya  Nyamagana zimekuwa zikifanya vizuri kitaifa kwenye mitihani ya darasa la saba n kuifanya kushika nafasi nne kitaifa,hivyo inahitaji kufanya mabadiliko makubwa ya elimu kwa kuondoa changamoto mbalimbali.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mabatini A George Kadago aliishukuru The Desk & Chair kwa msaada huo wa chumba kimoja cha darasa kwa kuwa kitapunguza uhitaji mkubwa wa shule hiyo na kuomba wadau wengine kuiga ili kusaidia sekta ya elimu.
Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 1,680 ina upungufu mkubwa wa  vyumba vya madarasa,mahitaji yakiwa ni vyumba 38 lakini vilivyopo  ni tisa  ukiongeza kilichojengwa na TD & CF, pungufu itakuwa vyumba 28 hali inayosababisha wanafunzi 150 kutumia chumba kimoja badala ya wanafunzi 45 .
Hata hivyo Halmashauri ya Jiji la  Mwanza inajenga vyumba 6 vya madarasa ili kupunguza changamoto ya uhaba wa madarasa shuleni hapo na yatakapokamilika mahitaji yatakuwa ni vyumba 22

No comments :

Post a Comment