Saturday, February 1, 2020

MBUNGE CHIKOTA ATAKA SERIKALI KUMALIZIA UJENZI WA BARABARA YA MTWARA-NEWALA-MASASI KWA LAMI


Na Alex Sonna, DODOMA
MBUNGE wa Nanyamba, Abdallah Chikota(CCM), amehoji serikali lini itajenga kwa kiwango cha lami kilometa 160 zilizobaki katika barabara ya Mtwara – Newala – Masasi.
Akiuliza swali bungeni leo, Chikota amesema barabara hiyo yenye
urefu wa kilometa 210 ujenzi wake umeanza kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara hadi Mnivata  yenye kilometa 50.
“Je, Serikali ina mpango gani kwa kilometa 160 zilizobaki?,”amehoji
Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo pia amesema katika bajeti ya mwaka 2019/20 na ujenzi wa barabara umeishia Mnivata na kwamba Mnivata hadi Nanyamba ni kilometa 20.
“Na kwa kuwa mkandarasi yupo pale kwanini bila kuathiri taratibu za manunuzi kwanini mkandarasi aliyepo asijenge kwa kiwango cha lami hadi Nanyamba mjini,lakini pia barabara Mtwara-Nanyamba-Masasi kuna barabara pacha ambayo ni ya ulinzi inakwenda hadi Michenjele, serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami,”amehoji
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Elias Kwandikwa, amesema ujenzi wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi kwa kiwango cha lami kwenye kilometa 160 zilizobaki pamoja na daraja la Mwiti utaanza katika mwaka wa fedha 2020/21.
Kwandikwa amefafanua upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi yenye kilometa 210 pamoja na daraja la Mwiti ulikamilika mwaka 2015.
“Mpango wa Serikali ni kujenga barabara yote kwa kiwango cha lami kwa awamu na awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa kilometa 50 ambayo utekelezaji wake hadi kufikia Desemba, 2019 ulikuwa asilimia 76, Jumla ya Sh.Bilioni 3.40 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2019/20 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi,”amesema
Hata hivyo, amemuomba Mbunge kuvuta subira kwa kuwa serikali imedhamiria kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Zipo taratibu za manunuzi zinafuatwa mkandarasi kama atakuwa na sifa basi ataomba ili aweze kukamilisha kipande hicho,”amesema
Naibu Waziri huyo amesema mara baada ya kukamilisha barabara inayojengwa sasa watajenga barabara ya hiyo pacha ya kiulinzi.

No comments :

Post a Comment