*******************************
Na Daudi Manongi, MAELEZO
Mkutano wa
kwanza wa kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
utafanyika tarehe 18-21 Februari visiwani Zanzibar, 2020 ukiwa na lengo
la kuchochea juhudi zilizopo katika kupunguza madhara ya maafa ambapo
mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar, Mhe.Dkt. Ali Mohamed Shein.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera,Bunge,Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati
akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.
“Katika
mkutano huu wa SADC tutajadiliana namna ya
kuwekeza katika kupunguza
madhara ya maafa kwa kuwa gharama za usimamizi wa maafa kama ya mafuriko
huzilazimu nchi wanachama kuelekeze rasilimali zilizotengwa kwa ajili
ya shughuli za maendeleo na badala yake huelekezwa katika shughuli za
kurejesha hali”, aliongeza Waziri Mhagama
Ameongeza
kuwa nchi wanachama ikiwemo Comoro, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kwa
mwaka 2019 zilipata mafuriko yaliyosababishwa na vimbunga Idai na Keneth
na gharama zake misaada na madhara zilikuwa kubwa sana zikikadiriwa
kuwa dola bilioni 10.
Ili kwenda
sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa , Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli itaendelea kuimarisha uwezo wake
wa usimamizi wa maafa katika Nyanja zote, aliongeza Mhagama.
“Tayari
Serikali ya Awamu ya Tano imetunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya
Kitaifa na.7 ya 2015 na kanuni zake, tunao wasifu wa janga la mafuriko
na ukame wa kitaifa na mkakati wa Taifa kupunguza madhara ya maafa”,
aliongeza Waziri Mhagama.
Itakumbukwa
kuwa Tanzania ilichukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya kuanzia
mwezi Agosti, 2019 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, 2020.
Mkutano huo unafanyika kwa mara ya kwanza visiwani Zaznibar huku ukiwa
na fursa kubwa kwa wananchi kwani utasaidia kukuza biashara na utalii na
kujitangaza kimataifa.
Kauli
mbiu ya Mkutano huu:Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya
maafa ni njia bora ya kuimraisha ustamilivu katika ukanda wa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini wa Afrika (SADC).”
Kamati ya
Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa imeanzishwa kwa lengo la
kulishauri Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC kuhusu masuala ya
upunguzaji wa madhara ya maafa kikanda huku lengo mahususi likiwa ni
kuwa na jukwaa la kubadilishana taarifa na uzoefu wa kiutendaji.
No comments :
Post a Comment