Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John
Mbungo, wakati alipozindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akiweka jiwe la msingi, wakati alipozindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, kulia
ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John Mbungo,
Januari 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akikata utepe, wakati alipozindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari
13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John
Mbungo, wakati alipozindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya ruangwa, wakati wa uzinduzi wa jengo
la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), lililopo katika
Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari 13, 2020.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Brig. Jenerali John Mbungo, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya
ruangwa, wakati wa uzinduzi wa jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), lililopo katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi,
Januari 13, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akipanda mti, baada ya kuzindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari 13, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) ukamilishe mapema uchunguzi dhidi ya madudu
yaliyoibuliwa katika
mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na wizi uliofanywa na
viongozi wa AMCOS kwa wakulima wa ufuta na korosho ikiwemo wilaya ya
Ruangwa.
Ameyasema hayo
leo wakati akizindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) wilaya ya Ruangwa lililogharimu zaidi ya sh. milioni 142.
Ametoa wito kwa TAKUKURU kuwa imara na kuweza kutembea kifua mbele
katika mapambano hayo.
Waziri Mkuu
amesema pamoja na TAKUKURU kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya
kila siku pia ameuagiza uongozi wa taasisi hiyo ukamilishe mapema
utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli
aliyoyatoa kwao kwa nyakati tofauti.
Amesema
ameshuhudia kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya kupitia
uchunguzi na ufuatiliaji wa madai ya malipo ya wakulima wa zao la ufuta
na korosho.“Kamilisheni chunguzi hizi zote kwa wakati ili hatua stahiki
za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliopatikana na
hatia.”
Amesema rushwa
huathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. “Kutokana na
ukweli huo, Serikali imetoa msukumo wa pekee katika kushughulikia
vitendo vya rushwa na ufisadi. Msukumo huo, umechangia kwa kiasi kikubwa
hususan katika kipindi hiki, utekelezaji wa miradi mikubwa na ya
kimkakati kwa ufanisi na kwa wakati.”
Amesema wananchi
wanatakiwa wafahamu kwamba kwamba nchi yoyote ambayo rushwa imetamalaki
siyo rahisi kuwa na uwezo wa kiuchumi utakaoiwezesha nchi hiyo kumudu
kulipa madeni ya ndani na ya nje. “Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania
tunashuhudia jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyolipa madeni.”
Kwa mfano, kati
ya Julai na Septemba, 2019, sh. bilioni 85.72 zimetolewa ikiwemo bilioni
50 za madai ya pensheni; bilioni 22 za madai ya watumishi wa umma
ikiwemo kiinua mgongo kwa wastaafu 3,019 na malimbikizo ya mishahara kwa
watumishi 1,435; bilioni 10.24 zimelipa watoa huduma na zaidi ya
bilioni 2 kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi washauri. Hayo ni
matokeo ya jitihada za kupambana na rushwa zinazofanywa na Serikali.
Amesema tangu
Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa ikijipambanua na
vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Hivyo, kitendo hicho cha kuendelea
kulipa madeni ni ishara ya mafanikio ya Serikali katika jitihada zake za
kuzuia na kupambana na rushwa nchini. Serikali itaendelea kudhibiti
mianya yote ya rushwa katika utendaji mzima wa Serikali.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amesema tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na wadau wa
mapambano dhidi ya rushwa na Utawala Bora kama vile Transparency
International (TI), MO Ibrahim na Afrobarometer zinaonesha kuwa kwa
miaka mitatu mfululizo, yaani 2016 hadi 2018 Tanzania imeendelea kufanya
vyema katika mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora.
Amesema mafanikio
hayo ya kujivunia ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kusimamia kwa dhati mapambano dhidi
ya rushwa kwa usimamizi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) ambayo ndicho chombo kilichopewa dhamana kisheria.
“Tambueni kwamba
uongozi mzima wa juu kabisa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa
Waziri Mkuu) uko pamoja nanyi katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
Pia ameagiza
kuanzishwa kwa vilabu vya kupambana na rushwa katika shule ili wanafunzi
waweze kuwa na uelewa na kuweza kutoa taarifa za rushwa.
Akizungumzia
kuhusu jengo alilolizindia amesema muhimu sana kwa taasisi nyeti kama ya
TAKUKURU kumiliki majengo yake yenyewe. Kuhusu hali ya majengo ya ofisi
za TAKUKURU katika ngazi ya mikoa na hata wilaya, amemwagiza Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Dkt Mary Mwanjelwa alishughulikie suala hilo.
Kwa upande
wake,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo
amesema jengo hilolimejengwa kwa muda wa miezi saba kuanzia tarehe
11/06/2018 na kukamilika tarehe 25/01/2019.“Hadi kufikia hatua hii ya
uzinduzi, jengo hili limegharimu jumla ya Sh. 142,857,142.86.”
Akizungumzia
kuhusu uchunguzi kiongozi huyo amesema kwa kipindi cha mwaka 2019
TAKUKURU imefanya uchunguzi kwenye tuhuma kubwa ikiwemo ya utekelezaji
wa maagizo ya Rais Dkt. Magufuli aliyoyatoa Jumanne Oktoba 15, 2019
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ruangwa.
“Kupitia
uchunguzi ule, tumebaini kwamba zaidi ya vyama 30 vya Msingi vya
Ushirika (AMCOS) vya Mkoani Lindiviliwadhulumu wakulima wa zao la ufuta
kiasi cha zaidi ya sh.Bilioni sh. 1.23. Kupitia uchunguzi huo
tuliwakamata na kuwahoji zaidi ya viongozi 300 wa
AMCOS zilizokuwa zinahusika katika dhuluma hii. Tulifanikiwa
kuokoa zaidi ya sh. bilioni 1.042. Fedha hizi zilikuwa ni mali ya
wakulima wa ufuta ambao walidhulumiwa fedha hiyo na Viongozi wa Vyama
vya AMCOS.”
Kadhalika
Brigedia Jenerali Mbungoamesema pamoja na kufanikiwa kujenga majengo ya
ofisi za TAKUKURU katika wilaya saba bado inakabiliwa na uhaba wa
majengo ya kudumu ya ofisi. Amesema TAKUKURU ina jumla ya ofisi 28 za
mikoa na ofisi 117 za wilaya huku mahitaji halisi ni majengo 28 kwa
ofisi za Mikoa na majengo 117 kwa ofisi za wilaya.
Naye, Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Dkt Mary Mwanjelwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria
kuendeleza mapambazo dhidi ya rushwa, hivyo uzinduzi wa jengo hilo ni
miongozi mwa harakati hizo.
No comments :
Post a Comment