Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (aliyeshika kipaza sauti ) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha
Kisaki baada ya kusikiliza malalamiko yao mbalimbali ikiwepo fursa za
upatikanaji ajira katika mradi wa JNHPP.
uonekano wa baadhi ya nyumba za wafanyakazi wanaotekeleza mradi wa JNHPP zilizokamilika kujengwa katika eneo la mradi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (pili kulia) akikagua ubora wa kitasa cha mlango wa moja ya
nyumba za kuishi wafanyakazi zilizokamilika kujengwa katika mradi wa
JNHPP.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (katikati) akizungumza mara baada ya kutembelea daraja la muda
lililojengwa katika bonde la mto Rufiji kurahisisha usafirishaji wa
vifaa na mahitaji mbalimbali ng’ambo ya mto ili kutekeleza shughuli za
ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme.
Muonekano wa mtambo wa kusaga
mawe ili kupata kokoto za ukubwa wa aina tofauti kulingana na mahitaji
zitakazotumika katika shughuli za ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (wa pili kushoto) akikagua sehemu ya eneo litakapojengwa bwawa
la kuzalisha umeme katika bonde la mto Rufiji.
Vibarua wakiendelea na shughuli
mbalimbali za ujenzi kulingana na Mpangokazi wa utekelezaji wa ujenzi
wa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme
Daraja la muda lililojengwa
kurahisha usafiishaji wa vifaa na mahitaji mbalimbali katika upande wa
pili wa mto katika eneo litakapojengwa bwawa la kuzalisha umeme.
Kazi ya kupasua miamba na kuondoa
vifusi ikiendelea kulingana na mpangokazi wa utekelezaji wa ujenzi wa
mradi wa bwawa la kuzalisha umeme.
………………………………………………….
Na Zuena Msuya, Morogoro
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani amewataka wakandarasi na wahandisi wanaotekeleza ujenzi wa
Mradi Bwawa la kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya
maji ya Bonde
la Mto Rufiji wa Julius Nyerere (JNHPP) kuhamia na kuishi katika eneo la
mradi kuanzia Januari 13,2020, baada ujenzi wa nyumba za wafanyakazi
kukamilika.
Aidha aliwataka wafanyakazi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wale Wahandisi washauri wa
mradi (TECU) kuhamia katika eneo la mradi kuanzia mwezi ujao baada ya
nyumba zao kukamilika pia.
Dkt.Kalemani alitoa agizo hilo,
Januari 12, 2020, alipofanya ziara ya kumi ya kukagua maendeleo na hatua
iliyofikiwa katika ujenzi wa mradi huo, tangu kusainiwa kwa mkataba na
mkandarasi kuanza kufanya kazi wa mradi huo uliopo Rufiji.
Dkt. Kalemani alisema kuwa,
kuanzia sasa hakuna sababu ya wafanyakazi wakandarasi wanaotekeleza
mradi wa JNHPP, kuishi mbali na eneo la mradi kwa kuwa tayari ujenzi wa
nyumba za wafanyakazi umekamilika.
“Hatupendi kuona wafanyakazi wa
mkandarasi wanaishi Dar Es Salaam, wakati kazi inafanyika Rufiji,
kuanzia kesho (Januari 13,2020) wakandarasi wote wahamie eneo la mradi,
na wale wafanyakazi wa TANESCO na TECU wao watahamia kuanzia mwezi ujao
baada ya nyumba zao kukamilika,” alisema Dkt.Kalemani.
Alisema tayari nyumba 8
zimekamilika zenye uwezo wa kubeba wafanyakazi 192, lengo la nyumba
zinazojengwa ni kubeba zaidi ya wafanyakazi mia nne watakaokuwa wakiishi
katika eneo la mradi.
Katika ziara hiyo pia, alimtaka
mkandarasi wa mradi huo kuanza kupeleka mitambo tisa ya kufua umeme
(Turbine) pamoja na vipuri vingine vinavyohitajika katika eneo la mradi
kwa kuzingatia makubaliano ya mkataba, pia aliwataka TANESCO pamoja na
TECU kuwa wazalendo katika kuhakiki ubora wa mitambo hiyo kwa manufaa ya
Taifa na kuhakikisha inafika eneo la mradi kwa wakati uliopangwa.
Vilevile aliendelea kupiga
marufuku wafanyakazi wageni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na
watanzania zikiwemo za vibarua, ulinzi, wauza vyakula na kadhalika na
kwamba yeyote atakayekaidi maagizo hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa
makubaliano ya mkataba.
“Tunataka kuona walinzi ni
SUMAJKT au Jeshi la Wanyapori, sitegemei kuona mlinzi kutoka nje ya
Tanzania akiwa pale getini,na endapo atakuwepo basi achukuliwe hatua,
nawaagiza Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa simamieni hili,”
alisisitiza Dkt. Kalemani.
Akizungumzia usafishaji wa eneo
la mradi, Dkt. Kalemani alitoa miezi miwili kwa Wakala wa Misitu
Tanzania(TFS), Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), TECU na wote
wanaohusika katika kusafisha eneo la mradi lenye ukubwa wa kilometa 914
kuharakisha utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa mpaka sasa kazi hiyo
haijafanyika.
Aidha aliwaagiza (TFS) kuwatumia
watu wenye sifa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi hiyo kwa kasi na kiwango
cha hali ya juu, hata hivyo aliwashauri kufanya mazungumzo na Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) ili kutekeleza kazi hiyo kwa haraka.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani,
alitembelea eneo la ujenzi wa bwawa, madaraja, mitambo ya kusaga kokoto
na kuchanganya zege,na sehemu ya kujenga mitambo tisa( Turbine) ya
kufua umeme.
Dkt. Kalemani alisema kuwa
ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji ya mradi huo ambao katika kila
hatua ya Mpangokazi wa utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 95 kwa
kila kazi iliyopangwa, ambapo kwa ujumla katika hatua za awali za
utekelezaji wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 5 na kazi zinaendelea
vizuri, mradi huo unatarajiwa kukamilika Juni 14, 2022.
Katika utekelezaji wa ujenzi wa
mradi huo, tayari Mkandarasi alishalipwa kiasi cha shilingi Trilioni
moja nukta tano ikiwa ni malipo ya awali.
Mapema akiwa njiani kuelekea eneo
la mradi, Dkt. Kalemani alizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kisaki na
kuwaahidi kutatua malalamiko yao kuhusu utaratibu wa kuwapatia vijana
ajira ambao wengi wao walikuwa wakiulalamikia.
Hata hivyo aliwataka vijana
wanaopata kazi katika mradi huo, kufanya kazi kwa kujituma na kuzingatia
mikataba ya kazi, badala ya kutoroka na kuacha kufanya kazi walizopewa.
No comments :
Post a Comment