Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati akitangaza makusanyo ya
kodi ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20 ambapo amesema kwa
mara nyingine, TRA imevunja rekodi kwa kukusanya jumla ya kiasi cha sh.
trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019 sawa na ufanisi wa asilimia 100.20
kutoka katika lengo la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi
huo. Kulia kwake ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Msafiri
Mbibo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati akitangaza makusanyo ya
kodi ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20 ambapo amesema kwa
mara nyingine, TRA imevunja rekodi kwa kukusanya jumla ya kiasi cha sh.
trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019 sawa na ufanisi wa asilimia 100.20
kutoka katika lengo la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi
huo. Kulia kwake ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Msafiri
Mbibo na kushoto kwake ni Kamishna wa Idara ya Walipakodi Wakubwa Bw.
Alfred Mregi.
******************************
Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), kwa mara nyingine, imevunja rekodi kwa
kukusanya jumla ya kiasi cha sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019
ambayo ni rekodi ya kwanza kufikiwa tangu kuanzishwa kwake
ikilinganishwa na rekodi ya mwezi Septemba, 2019 iliyokuwa sh. trilioni
1.767.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka hiyo Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa, makusanyo hayo ya mwezi
Desemba 2019 ni sawa na ufanisi wa asilimia 100.20 kutoka katika lengo
la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi huo.
“Ni
kweli kwamba, kitaalam, miezi tofauti hailinganishiki moja kwa moja.
Hata hivyo, kwa makusanyo haya ya sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba
2019, TRA imevunja rekodi yake yenyewe iliyoiandika mwezi Septemba 2019
ambapo ilikusanya jumla ya sh. trilioni 1.767 ikiwa ni sawa na asilimia
97.20 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 1.817 katika kipindi hicho,”
alisema Dkt. Mhede.
Akizungumzia
makusanyo ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20 inayohusisha
mwezi Oktoba, Novemba, na Desemba yenyewe, Kamishna Mkuu Mhede amesema
kuwa, TRA imefanikiwa kukusanya jumla ya sh. trilioni 4.972 sawa na
ufanisi wa asilimia 97.49 ya lengo la kukusanya jumla ya sh. trilioni
5.100.
“Makusanyo
haya ya robo ya pili ya mwaka 2019/20 ni sawa na ukuaji wa asilimia
19.78 ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha Robo ya Pili ya mwaka
2018/19 ambapo Mamlaka ilikusanya sh. trilioni 4.151 ikiwa ni sawa na
ufanisi wa asilimia 87.59 kutokana na lengo la kukusanya mapato kiasi
cha sh. trilioni 4.739 katika kipindi hicho,” alifanunua Kamishna Mkuu
Mhede.
Ameeleza
kuwa, kwa upande wa makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi Oktoba
2019, TRA ilikusanya kiasi cha sh. trilioni 1.484 na Novemba 2019,
Mamlaka ilikusanya sh. trilioni 1.501 sawa na ufanisi wa asilimia 93.98
na asilimia 97.59 kutoka katika malengo ya kukusanya sh. trilioni 1.579
na sh. trilioni 1.538 kwa mwezi Oktoba na Novemba 2019.
Kamishna
Mkuu Mhede ameongeza kuwa, makusanyo hayo ni muendelezo wa kiashiria
cha wazi kwamba Walipakodi na Watanzania walio wengi wameendelea
kuelewa, kukubali, na kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano wa
kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya Taifa zima.
“Kwa
kuwa Walipakodi wengi wameitikia wito wa kulipa kodi kwa mujibu wa
Sheria, ni rai yangu kwamba asiwepo mlipakodi hata mmoja ambaye
atathubutu kubaki nyuma. Ni busara wafanyabiashara wote wakaungana na
kundi kubwa la Washindi, yaani, kundi kubwa la wanaolipa kodi kwa hiari,
kwa ukamilifu, na kwa wakati, alisisitiza Dkt. Mhede.
Pia,
amewashukuru walipakodi waliolipa kodi kwa wakati na hivyo kupelekea
kuongezeka kwa makusanyo ambayo yatapelekea utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
“Kwa
namna ya kipekee, napenda kuwashukuru Walipakodi wote waliolipa kodi ya
Serikali na kupelekea Mamlaka kufikia makusanyo haya ya kihistoria kwa
mwezi Desemba 2019. Pia, tunaishukuru sana Serikali ikiwa ni pamoja na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bodi ya Wakurugenzi ya TRA,
Taasisi za Maendeleo, na Sekta Binafsi kwa kuendelea kuipatia TRA
ushirikiano stahiki katika kutekeleza majukumu yake ya kukadiria,
kukusanya, na kuhasibu mapato ya Serikali,” Alisema Kamishna Mkuu Mhede.
Aidha,
ametoa wito kwa wamiliki wote wa majengo nchini kujitokeza kulipia kodi
za majengo ili kuepuka usumbufu wa kulipa mwishoni mwa mwaka wa fedha
2019/2020 ambapo amesema kuwa, kwa sasa viwango ni rafiki na vinalipika
kwa urahisi.
Amevitaja
viwango hivyo kwa mwaka kuwa ni sh. 10,000 kwa nyumba ya kawaida, sh.
50,000 kwa kila sakafu ya nyumba ya ghorofa katika Majiji, Manispaa, na
Halmashauri za Miji, na sh. 20,000 kwa jengo la ghorofa katika maeneo ya
Halmashauri za Wilaya.
No comments :
Post a Comment