Wednesday, January 1, 2020

Masauni apiga marufuku Mawakili Nje ya Ofisi za NIDA




Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akifatilia Uingizwaji wa Taarifa za Wananchi waliotoka sehemu mbalimbali mkoani Morogoro na  kufika  Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA),zilizopo eneo la Tungi-Mfuruni mkoani hapo  ikiwa ni muendelezo wa zoezi la kujipatia kitambulisho hicho kwa wananchi nchini kote.Wapili kulia ni Afisa Usajili wa NIDA Mkoa wa Morogoro,James Malimo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) Mkoa wa Morogoro,James Malimo(aliyenyoosha mkono),akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia),aliyefika Ofisi ya NIDA zilizopo eneo la Tungi-Mfuruni kuona zoezi la uandikishaji na utolewaji wa vitambulisho linavyoendelea.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
********************************
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amepiga marufuku
watu wanaojiita mawakili na kuwatoza wananchi kiasi cha  fedha kinachozidi shilingi Elfu Kumi  wakidai ni ada ya kupewa nyaraka mbadala ya cheti cha kuzaliwa ikiwa ni hitajio la msingi kwa wananchi wanaofika ofisi mbalimbali nchini za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA)
Akizungumza baada ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Mkoa wa Morogoro walioitaka Serikali kuweka bayana kama kupata vitambulisho vya taifa lazima ulipe hela,Naibu Waziri Masauni alisema vitambulisho hutolewa bure hakuna haja ya kulipa gharama yoyote huku akipiga marufuku wananchi kutozwa fedha nje ya ofisi za NIDA
“Kuanzia sasa kila Ofisi ya NIDA itakuwa na mawakili wa serikali wataohusika na kuandaa pamoja kuhakiki nyaraka mbalimbali za wananchi wanaokuja kwa ajili ya vitambulisho vya taifa na ninatoa maelekezo kwa nchi nzima katika ofisi za NIDA kuwaondoa watu wanaowaandalia wananchi nyaraka hizo kwanza hatuwatambui kama ni maafisa sheria sahihi au la na wanaweza kuwathibitisha watu ambao sio raia wakapata vitambulisho kama raia” alisema Masauni
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema wao kama mkoa wako tayari kuleta mawakili wa serikali katika ofisi hizo za NIDA huku akiwaasa wananchi kwenda sehemu sahihi wanapofika kutafuta vitambulisho katika ofisi hizo.
“Serikali ipo kuhakikisha zoezi la utolewaji namba na vitambulisho vya taifa linamalizika ndani ya siku 20 zilizoongezwa na Rais Magufuli na kama mkoa tunayafanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri Masauni na kuanzia kesho mawakili wa serikali watakuwepo hapa kuhakiki na kutengeneza nyaraka za serikali kwa wananchi” alisema RC Sanare
Nae Afisa Usajili wa  NIDA Mkoa wa Morogoro,James Malimo amesema katika Mkoa wa Morogoro na Wilaya zake jumla ya vitambulisho 347,466 kati ya 849,436 vimezalishwa huku maombi 237.236 yakikwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo waombaji kukosa vigezo vya uraia,mihuri ya wadau na viambata.

No comments :

Post a Comment