Mhandisi wa wakala wa Barabara
mjni na vijijini(Tarura)Mji wa Mbinga Amos Agustine akieleza jambo juu
ya kuharibika kwa mifereji iliyojengwa katika mtaa wa Kipika kata ya
Matarawe Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,
Mitaro iliyojengwa katika Mtaa
wa Kipika kata ya Matarawe na Wakala wa Barabara mjini na
vijijini(Tarura) Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma ikiwa
imeharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika
wilaya hiyo,hata hivyo kuharibika kwa Mitaro hiyo kumetajwa na baadhi
ya wakazi wa Mbinga kunatokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango na
kukosa usimamizi makini wa Tarura ambapo imeanza kuharibika katika
kipindi cha miezi sita tu tangu mkandarasi akabidhi kazi hiyo.
********************************
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
MVUA zinazoendelea
kunyesha kwa wingi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,zimesababisha
kuharibika kwa miundombinu ya barabara katika mtaa wa Kipika kata ya
Matarawe wilayani humo na hivyo kutishia kukata mawasiliano kati ya mtaa
huo na maeneo mengine ya mji wa Mbinga.
Kutokana na uharibifu
uliotokea,baadhi ya wakazi wa mji wa Mbinga wameiomba Serikali
kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani makandarasi na
wahandisi wa wakala wa barabara vijijini na mijini Tanzania (TARURA) kwa
kushindwa kusimamia majukumu yao ikiwemo ujenzi wa mradi huo chini ya
kiwango.
Walisema, ni kawaida
baadhi ya barabara katika mji wa Mbinga kuharibika ndani ya muda mfupi
tangu zinapojengwa na hali hiyo inatokana na wahandisi kushindwa
kutumia taaluma zao wakati wa kutekeleza miradi ya Barabara katika
wilaya hiyo.
Wamesema, kupeana
kazi za ujenzi wa miradi ya barabara kwa misingi ya urafiki na kujuana
kwa kiasi kikubwa kumechangia miradi mingi ya barabara katika mji huo
kujengwa chini ya kiwango na hivyo kushindwa kuleta tija.
Aidha,wameiomba
taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mikataba
inayoingiwa kati ya Tarura na Makandarasi ili kufahamu juu ya uwezo wa
wakandarasi wanaopewa kazi katika Mji wa Mbinga.
Wakiongea kwa nyakati
tofauti,wakazi hao Antonia Komba,Daud Shija na Suzana Ndomba wamesema,
baadhi ya miradi inayojengwa haimalizi kero za wananchi licha ya
kutekelezwa kwa fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii.
Antonia Komba mkazi wa
mtaa huo, alitolea mfano ujenzi wa mifereji iliyojengwa katika barabara
ya Kipika mtaa wa Kipika imedumu kwa miezi saba tu tangu ilipojengwa
na sasa imeharibika kutokana na kusombwa na maji ya mvua na hivyo
kushindwa kumaliza kero ya muda mrefu ya wananchi wa kata ya Matarawe.
Alisema, mifereji hiyo
badala ya kuleta faraja kwa wananchi imeonekana sio salama hasa kwa
watoto wadogo wanaopita maeneo hayo wakati mvua zinaponyesha ambapo
maji kutoka maeneo ya milimani yanapita kwa wingi.
Mkazi mwingine Daud
Shija amesikitishwa kuona mifereji iliyojengwa kwa fedha nyingi imeanza
kuharibika kabla ya mvua hazijawa kubwa na hivyo kuwa na hofu kuhusu
uwezo wa mkandarasi aliyejenga mifereji hiyo.
Shija ambaye ni
Mchungaji wa Kanisa la TAG Mbinga, ameiomba Serikali kupitia taasisi na
idara zake kupima na kujiridhisha juu ya uwezo wa wakandarasi
wanaoomba kazi za ujenzi ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha za
Serikali.
“kwa kweli nilipoona
mifereji inajengwa katika eneo hili nilifurahi na kuipongeza sana
Serikali kwa hatua hii,lakini furaha yangu imepotea ghafla baada ya
kuona mifereji yote imeharibika kwa muda mfupi tangu ilipojengwa, mimi
kama Mtanzania naishauri Serikali lazima iwe makini na waandisi wake na
wakandarasi”alisema Mchungaji Shija.
Ditram Shabani
alisema, uwezo mdogo wa makandarasi ndiyo sababu ya mifereji hiyo
kuharibika kwa muda mfupi, tofauti na matarajio ya wakazi wa mtaa huo
kwani ni kama hakufanya kazi yoyote katika eneo hilo ambalo ni kiungo
muhimu kwa wakazi wa kata ya Matarawe na maeneo mengine ya Mji wa
Mbinga.
Suzana Ndomba alisema,
‘’kila mvua inaponyesha maji yanayopita katika eneo hilo yanakuwa na
kasi kubwa hali inayo hatarisha maisha ya watoto wadogo na hivyo
wanalazimika kuwafungia ndani kama hatua ya kuwaepusha kusombwa na
maji.
Meneja wa wakala wa
Barabara(Tarura)Mji wa Mbinga Ismail Mafita hakupatikana kutolea
ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kwa kuwa yuko nje ya wilaya ya
Mbinga na hata alipotafutwa kwa njia ya simu alikataa kujibu chochote
badala yake alituma ujumbe mfupi (sms) yuko Hospitali.
Hata hivyo,Kaimu
Meneja wa Tarura Amos Agustine alikiri kuharibika kwa mifereji
iliyojengwa katika eneo hilo,ambapo alisema hali hiyo imetokana na
athari za mvua zinazo endelea kunyesha kwa wingi katika wilaya ya
Mbinga.
Amos ameitaja kampuni
iliyojenga mifereji ni Stumack Engineering Co Ltd ya Dar es salaam huku
akitaja gharama za mradi huo ni shilingi Milioni 33.6.
Kwa mujibu wake,kazi
ya ujenzi wa mradi huo ilianza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2019
ambapo muda wa uangalizi umemalizika tangu tarehe 17 Novemba mwaka huu
na mkandarasi ameshakabidhi mradi kwa Tarura.
Aidha alieleza,mpango
uliopo kwa sasa ni kumpata mkandarasi mwingine ambaye atajenga upya
mifereji hiyo, hata hivyo alisisitiza kuwa, suluhisho la kudumu ni
kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika eneo hilo sambamba na
kuimarishwa kwa mifereji.
Alisema, eneo hilo ni
kati ya maeneo mengi katika Mji wa Mbinga ambapo barabara zake
zimeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa wingi
katika mji wa Mbinga.
Mkandarasi wa mradi
huo aliyefahamika kwa jina moja la Mwafyenga alipotafutwa kwa njia ya
simu alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sababu yuko Hospitalini
amelazwa.
No comments :
Post a Comment