Thursday, January 2, 2020

Mtoto mwenye uwezo mkubwa kiakili apata mfadhili.



Baraka Onyango Raphael (3)ambaye ana uwezo mkubwa kiakili wa kutaja Marais wa nchi 56 na mawaziri pamoja na manaibu waziri wa Tanzania bila ya kuangalia popote akiwa na mama yake Macelina Asango nyumbani kwao kwa mrombo Jana.(Happy Lazaro).
 Mfanyabiashara Philemon Mollel (Monaban)akiwa na mama na mtoto ambaye ameahidi kumsomesha kutokana na kuwa na kipaji kikubwa kiakili .
*********************************
Happy Lazaro,arusha
Arusha.Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha  Philemon Mollel maarufu kama Monaban amejitolea kumsomesha  mtoto mwenye uwezo mkubwa kiakili aitwaye Baraka  Onyango Raphael  (3) mkazi wa kwa mrombo kata ya Muriet jijini Arusha.
Aidha mtoto huyo ambaye aliwahi kuibuliwa na vyombo mbalimbali vya habari kutokana na uwezo mkubwa alionao ikiwemo kutaja mwenyewe idadi ya Marais wa nchi 56 pamoja na mawaziri na manaibu wa Tanzania  bila kusoma popote.
Akizungumzia namna mtoto huyo alivyo na uwezo wa kipekee ,mama wa mtoto huyo Macelina Asango  amesema kuwa,mtoto huyo alianza kuonyesha uwezo huo akiwa na miaka  2 na nusu,kutokana na wenzake aliokuwa akicheza nao kuona jinsi ambavyo anaongea mambo makubwa ambayo yaliwashangaza wao.
Amesema kuwa, mtoto huyo ambaye ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia hiyo baada ya wazazi wake kuona kipaji Cha mtoto huyo ndipo walipoanza kumwuliza maswali na kushangaa anajibu bila kusoma popote.
“kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa kutupa mtoto huyu kwani ana akili za kipekee sisi wenyewe tulishangaa Sana anavyowataja Marais wa nchi 56 kwa kichwa bila hata kusoma popote pamoja na mawaziri na manaibu waziri wa serikali ya Tanzania ,baada ya hapo ndipo  tulienda kwenye vyombo vya habari na kuelezea uwezo wa mtoto huyu ili aweze kusaidiwa kielimu kutokana na uwezo mdogo tulionao wa kumpeleka shule za mchepuo wa kiingireza”amesema mama.
Ameongeza kuwa,kutokana na uwezo mkubwa alionao mtoto huyo wanahitaji asome shule za mchepuo wa kiingireza ili kukuza kipaji chake kwani wao hawana uwezo wa kumpeleka shule binafsi .
Aidha baada taarifa za mtoto huyo kuripotiwa kwenye vyombo vya habari ndipo,Mfanyabiashara Philemon Mollel (Monaban)alipoguswa na kufika nyumbani kwa mtoto huyo ambaye ameahidi kumsomesha katika shule ya mchepuo wa kiingireza .
Akizungumza wakati alipomtembelea mtoto huyo,Mollel alisema kuwa,ameguswa Sana na kipaji alichonacho mtoto huyo na kuwa yupo tayari kumsomesha na atawashirikisha marafiki zake jambo hilo ili waweze kumsaidia mtoto huyo kufanikisha ndoto zake.
Mollel amesema kuwa,mtoto huyo ataanza rasmi shule Januari 6,mwaka huu katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya Pison iliyopo mjini hapa na kwa kuanzia atamlipia kiasi cha fedha  kwa ajili ya kuanzia .
Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Pison ,Gilbert Sarungi amesema kuwa,wapo tayari kumpokea mtoto huyo kutokana na uwezo mkubwa alionao wa kutambua mambo mkubwa bila hata ya kusoma popote.
Amesema kuwa, mtoto huyo atapewa kipaumbele maalumu kutokana na uwezo mkubwa alionao ambapo wapo tayari kumpokea Januari 6 shuleni hapo.
Mama wa mtoto huyo,Macelina ameshukuru Mfanyabiashara huyo kwa moyo wa huruma wa kumsaidia mtoto huyo ambaye walikuwa wakiwaza namna ya kumpeleka shule kwa ajili ya kuendeleza kipaji chake kutokana na uwezo mdogo walionao .
“Nashukuru Sana jamani vyombo vya habari kwa kunisaidia kumtangaza mtoto huyu na hatimaye ameweza kupata mfadhili wa kumsomesha shule ya mchepuo wa kiingireza na nimefarijika Sana kwani ataweza kuendeleza ndoto yake na kipaji chake cha tofauti alicho nacho”alisema mama wa mtoto huyo.

No comments :

Post a Comment