
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akijibu swali la Mbunge wa Rufiji Mhe.Mohamed
Mchengerwa aliyeuliza Je,ni lini Serikali itapeleka huduma za benki
katika wilaya ya Rufiji? bungeni leo jijini Dodoma katika mkutano wa 18
wa Bunge la 11
PICHA NA ALEX SONNA,FULLSHANGWEBLOG
…………………
Na Josephine Majula na Saidina Msangi
Serikali imeahidi
kuongeza jitihada za kuanzisha matawi ya benki ya uhakika katika Wilaya
ya Rufiji mkoani Pwani ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za
kifedha kwa
urahisi.
Hayo yameelezwa
bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed
Omary Mchengerwa aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka huduma za
benki katika Wilaya hiyo.
Mhe. Mchengerwa
alisema kuwa wananchi wa Jimbo kongwe nchini wamekuwa wakipata tabu ya
kupata huduma za kifedha hali inayowalazimu kusafiri umbali wa Kilometa
100 kufuata huduma hizo.
Akijibu swali
hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa wananchi wa Rufiji waendelee kutumia
huduma za fedha zilizopo wakati Serikali ikiendelea kuboresha
miundombinu muhimu pamoja na kufanya majadiliano na kuzishawishi benki
kuanzisha matawi yao katika Wilaya hiyo.
“Kufuatia
mabadiliko ya Sekta ya Fedha nchini ya mwaka 1991, Serikali ilitoa uhuru
kwa benki kufanya tafiti za kuamua kuhusu maeneo ya kupeleka huduma za
kibenki kulingana na taarifa za utafiti uliofanywa pamoja na vigezo vya
benki husika. Kwa kuwa benki zinajiendesha kibiashara maamuzi ya
kufungua tawi sehemu yoyote hapa nchini huzingatia vigezo
hivyo”,alisisitiza Dkt. Kijaji.
Alisema Serikali
inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kifedha hasa zile
zinazotolewa maeneo ya karibu na wananchi, itaongea na benki kuona namna
ya kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyoweza kusababisha gharama za
uendeshaji wa shughuli za benki wilayani hapo kuwa juu ili wananchi
waweze kupata huduma hizo kwa urahisi.
Alisema kwa sasa wananchi wa Wilaya hiyo wanapata huduma za kifedha kupitia Kituo cha Makusanyo ya Fedha cha NMB (Cash Collection Point – CCP) kilichopo katika Kata ya Utete pamoja na Mawakala wa Benki, hususan Benki ya NMB na CRDB waliopo katika Wilaya ya Rufiji
No comments :
Post a Comment