Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni
ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud, akiongea na viongozi kutoka TIC, TCB,
TanTrade pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wakati walipokutana katika
mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya
kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo akiwaelezea jambo viongozi wa Kampuni
Alrifai juu ya upatikanaji wa zao la kahawa nchini
Meneja Viwango Bwn. Ahmed
Mohamed Bahie akikagua korosho zinazozalishwa hapa nchini, kulia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dkt. Anselm Moshi na
kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara TanTrade, Bi. Twilumba
Mlelwa
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni
ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud pamoja na Meneja wa Manunuzi Bwn.
Hussain wakikagua korosho zilizohifadhiwa kwenye moja ya ghala hapa
nchini, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dkt.
Anselm Moshi
……………….
Na Mwandishi wetu,
Kampuni ya Alrifai
inayojihusisha na biashara ya mazao mchanganyiko iko nchini kwa lengo la
kuangalia fursa za uwekezaji hususani kununua zao la korosho na kahawa
na kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanda cha kuchakata zao la korosho
nchini.
Ujumbe wa watu watatu (3)
ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo ya Alrifai, Bwn.
Abdellah Foaud, Meneja Viwango Bwn. Ahmed Mohamed Bahie pamoja na Meneja
wa Manunuzi Bwn. M. K Hussin uko nchini tangu tarehe 13 Januari, 2020
kwa lengo kuu la kuangalia uwezekano wa Kununua korosho zilizokwisha
chakatwa pamoja na kahawa zilizokobolewa na pia kuona maeneo ambayo
wanaweza kuwekeza katika kiwanda cha kuchakata korosho.
Ujumbe huo ulifanya kikako na
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Kahawa (TCB), Mamlaka ya
Maendeieo ya Biashara Tanzania (TanTrade) pamoja na Bodi ya Mazao
Mchanganyiko na kuweza kupata fursa ya kufahamu kwa undani juu ya
taratibu za ununuzi wa mazao hayo pamoja na taratibu za uwekezaji wa
kiwanda cha kuchakata korosho hapa nchini.
Akitoa maelezo juu ya
uzalishwaji wa zao la Korosho nchini, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za
Biashara wa TanTrade, Bi. Twilumba Mlelwa alisema kuwa korosho ghafi kwa
mwaka huzalishwa kati ya tani 250,000 na tani 300,000 ambapo kiasi
kikubwa huzalishwa Mtwara, Lindi, Ruvuma (Tunduru), Pwani (Mkuranga na
Kibaha) pamoja na Tanga.
“Naomba niwatoe shaka juu ya
zao la korosho kwani kwa sasa viwanda vya korosho ni 18 ambapo vinauwezo
wa huhifadhi tani 63,000 za korosho lakini kwa sasa vinavyofanya kazi
ni 13 na vina uwezo wa kubangua tani 43,000” Amesema Bi. Mlelwa
Kwa upande wake Afisa Mtendaji
Mkuu wa Kampuni hiyo ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud,ameushukuru Ubalozi
wa Tanzania nchini Kuwait kwa ushirikiano alioupata kutoka ubalozini
hadi kwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuweza kuratibu zoezi la
kukuagua zao la Korosho, kahawa pamoja na karafuu.
“Binafsi nashukuru kwa
ushirikiano nilioupata kwa viongozi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara, Bodi ya
Mazao Mchanganyiko, TIC, TanTrade, Bodi ya Kahawa pamoja na Balozi
Mhandisi Aisha Amour kwa namna alivyolisimamia jambo hili tangu likiwa
wazo mpaka sasa tunapoelekea kwenye utekelezaji niwaahidi tu kuwa
utekelezaji wa kununua mazao haya utaanza mara moja mara tu baada ya
kufanya maamuzi na mikataba itasainiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema
Bwn. Foaud
Aidha, mbali na maelezo ya
uzalishaji wa zao la Korosho nchini, ujumbe huo pia ulipata fursa ya
kuona zao la korosho lililohifadhiwa katika ghala la Serikali eneo la
Kurasini jijini Dar es Salaam na uliridhishwa na zao hilo na kuahidi
kuwekeza nchini kwani korosho zinzazalishwa ni nzuri na bora.
Meneja Viwango Bwn. Ahmed
Mohamed Bahie amesema “tumejionea wenyewe ubora wa korosho, kahawa na
karafuu kwa kweli ni nzuri sana na sote tumeridhika na ubora huo.
Tutajitahidi kukamilisha taratibu zote muhimu na kuanza mara moja
uagizaji wa korosho na baadae kujenga kiwanda cha kuchakata korosho hapa
Tanzania,”.
Ujumbe huo ulipata fursa ya
kutembelea maeneo kadhaa kwa lengo la kupata maelezo kuhusu taratibu na
fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini, maeneo hayo ni pamoja na mikoa
ya Lindi, Mtwara na Kilimanjaro pamoja na Zanzibar ambapo waliweza
kuona uzalishaji wa Karafuu.
Ujio wa kampuni hiyo ni matokeo
ya juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini Kuwait ambapo ulifanya
mazungumzo na Kampuni ya Alrifai inayojihusisha na biashara ya mazao
mchanganyiko kuhusu nia yao ya kununua zao la korosho na kahawa na
kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanda cha kuchakata zao la korosho
nchini Tanzania.
No comments :
Post a Comment