Mkurugenzi Mtendaji wa tiba wa
hospitali ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, Dkt Emmanuel Nuwass
akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 64 ya hospitali hiyo ambapo
vifaa tiba vya shilingi bilioni 1.6 vilizinduliwa.
*******************************
HOSPITALI ya rufaa ya
Haydom Mkoani Manyara, imesherehekea maadhimisho ya miaka 64 tangu
ianzishwe kwa kuzindua vifaa tiba vya thamani ya shilingi bilioni 1.6
vya hospitali hiyo.
Hospitali ya rufaa ya
Haydom ya Kilutheri inayomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Mbulu ilianzishwa
mwaka 1955 na wamisionari wa Norway ina vitanda 420 baada ya
kupandishwa hadhi mwaka 2010.
Hospitali hiyo
inashirikiana na serikali ya Tanzania kupitia halmashauri ya wilaya ya
Mbulu, Mkoa wa Manyara na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto.
Maadhimisho hayo
yalitarajiwa kuwa na mgeni rasmi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu lakini akawakilishwa na Mkuu wa
Wilaya ya Mbulu, Chelestino Simbalimile Mofuga.
Mofuga alisema mzigo
mzito huwa anapewa mnyamwezi hivyo yeye amekasimiwa madaraka na Waziri
Wa Afya ili amwakilishe kwenye tukio hilo kubwa la kihistoria.
Alisema kila wakati
anaimwagia sifa hospitali hiyo kwani inabeba taswira nzuri ya wilaya
kutokana na huduma bora na nidhamu iliyopo.
“Hivi sasa mnazidi
kupiga hatua mnapaswa kuandika barua upya ili hospitali ipandishwe hadhi
kuwa ya kanda kwani inatoa huduma kwa watu wengi na walio na hali
duni,” alisema Mofuga.
Alisema uongozi wa
hospitali hiyo ni wabunifu kwani wamefanikisha ununuzi wa vifaa hivyo
kwa kuendesha harambee na kuchangiwa na wadau wa maendeleo.
Mkurugenzi wa tiba wa
hospitali ya rufaa ya Haydom, Dk Emmanuel Nuwass alisema vifaa tiba
hivyo vinne vipya vilivyozinduliwa vimegharimu shilingi bilioni 1.6.
Dk Nuwass alisema
vifaa hivyo ni CT scan, digital X-ray, mtambo wa kuzalisha hewa ya
oxsijeni kwa ajili ya wagonjwa na mashine ya kisasa ya kuteketeza taka
hatarishi.
Alisema mashine ya CT
Scan ya kampuni ya Siemens yenye thamani ya shilingi milioni 654.2
ikiwa imeshawahudumia zaidi ya wagonjwa 250, mashine ya pili ni Digital
X-ray ya kampuni ya GE Health care ya thamani ya shilingi milioni 320.2
mashine ya kuzalisha hewa ya oxsijeni ya kampuni ya Ozcan Kardelser ya
thamani ya shilingi milioni 372.9 imezalisha mitungi 1,665 imeokoa
shilingi milioni 72 zilizokuwa zimetumika na mashine ya kuteketeza taka
hatarishi (Incinerator) yenye uwezo wa kuchoma kilogramu 100 ya taka kwa
saa yenye thamani ya shilingi milioni 203.
Alisema hospitali ya
rufaa ya Haydom inahudumia wagonjwa 105,296 wa nje na 14,020 wa ndani
kwa mwaka kwenye mikoa ya Manyara, wilaya ya Karatu mkoani Arusha,
wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wilaya
za Mkalama na Iramba Mkoani Singida na wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Mwakilishi wa Balozi
wa Norway nchini, Britt Hilde Kjolas alisema kwa zaidi ya miaka 60 kabla
ya uhuru nchi yake ilikuwa na ushirikiano mkubwa na Tanzania hadi
sasa.
Mkurugenzi mkazi wa
Norwegian Church Aid (NCA) Gwen Bwerge aisema Serikali izidi kuweka
mkono wake kwa kuongeza watumishi kwani hivi sasa vifaa vipo.
Askofu wa KKKT
Dayosisi ya Mbulu, Nicolaus Nsangazelu alisema kuna baadhi ya wagonjwa
kutoka wilayani Meatu mkoani Simiyu ambao aliwauliza mbona wamekuja
kutibiwa mbali wakadai wamefuata huduma bora.
Mbunge wa jimbo la
Mbulu Vijijini, Flatei Maasay alisema aliwahi kuwakutanisha Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na
uongozi wa hospitali hiyo ili kuzungumzia changamoto zilizopo
hospitalini hapo.
No comments :
Post a Comment