
…………………………………………………………………………………………………………
Na. Josephine Majura na Peter Haule WFM, Dodoma
Serikali imeeleza
kuwa haina mpango wa kuingilia taaluma ya ukaguzi wa hesabu nchini kwa
kuondoa kipengele cha Hati inayoridhisha kwenye Ukaguzi wa Hesabu kwa
kuwa ni matakwa ya Viwango vya kimataifa vya uandaaji wa Taarifa za
Fedha.
Hayo yamesemwa
Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bunda Mhe.
Mwita Boniface, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaondoa kipengele
cha Hati safi kwenye taarifa za ukaguzi wa Hesabu za Fedha kwa kuwa ni
dalili za kuficha ubadhirifu katika Mashirika na Taasisi za Umma.
Akijibu swali
hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Kijaji, alisema kuwa kutoa
utaratibu mwingine wa taarifa za kikaguzi za fedha itakua ni kukiuka
Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Fedha (IPSAS) katika
Sekta ya Umma na pia Viwango vya Kimataifa vya Ukaguzi (ISSAI) ambavyo
Serikali imeviridhia.
“Dhana ya kuwa
Hati inayoridhisha inatoa tafsiri ya kuwepo kwa kila aina ya ubadhirifu
siyo sahihi kwa sababu maoni ya ukaguzi yanatolewa kwa malengo maalum ya
kuwafahamisha watumiaji wa taarifa za fedha kama taarifa hizo
zinaonyesha ukweli na hali halisi ya hesabu za mizania kwa taarifa za
mapato na matumizi pamoja na taarifa ya mtiririko wa fedha kwa kipindi
kilichokaguliwa”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa Hati
inayoridhisha hutolewa kwa Taarifa za Fedha zinazowasilishwa na
kukaguliwa zinapozingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu
katika Sekta ya Umma na Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.
Dkt. Kijaji
aliongeza kuwa dhana ya ukaguzi wa Hesabu inajikita katika masuala
ambayo wakaguzi wanaamini kuwa ni mazito na yanaathari kubwa kwenye
taarifa za fedha za Taasisi husika.
“ Lengo Kuu la
ukaguzi wa Hesabu ni kutoa maoni kama Hesabu zinazokaguliwa zinaonesha
hali halisi ya mapato na matumizi ya Serikali kwa kuzingatia viwango vya
kimataifa vya uandaaji wa taarifa za fedha”, alifafanua Dkt. Kijaji.
Alifafanua kuwa
Maoni hutolewa kwa njia ya hati za ukaguzi ambazo zimegawanyika katika
makundi manne ambayo ni Hati inayoridhisha, Hati yenye shaka, Hati
isiyoridhisha na Hati Mbaya.
Sheria ya Ukaguzi
wa Umma ya Mwaka 2008 inampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali kufanya kaguzi mbalimbali ambazo ni Ukaguzi wa Hesabu
(Financial Audits, Ukaguzi wa Kiuchunguzi (Forensic Audits), Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Audtis) na Ukaguzi Maalum (Special Audits) ili kujua hali halisi ya Mapato na Matumizi.
No comments :
Post a Comment