Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Ellen Mkondya
akizungumza katika mkutano wa tatu wa kisayansi kuhusu matumizi ya
teknolojia katika kutoa huduma za afya nchini. Mkutano huu
umewashirikisha wataalam kutoka hospitali mbalimbali nchini pamoja
taasisi nyingine.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mkutano huu leo.
Mkuu wa Idara ya Tehama Muhimbili,
Bw. Patrick Muro akitoa mada kwenye mkutano kuhusu matumizi ya
teknonolojia katika kutoa huduma za afya. Wengine ni watoa mada wakiwa
kwenye mkutano.
Washiriki wakisikiliza watoa mada kuhusu matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za afya nchini.
…………………
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
imefanya kongamano la tatu la kisayansi kujadili matumizi ya TEHAMA
katika kutoa huduma bora za afya katika zama za maendeleo ya
kidijitali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
kongamano hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Hedwiga Swai
amesema Muhimbili imefanya uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya TEHAMA na
imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali katika matumizi
ya teknolojia.
“Kongamano hili litahusisha
washiriki kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila
pamoja na washiriki kutoka nje ya Dar es Salaam ambapo watatoa uzoefu
wao na kujadili jinsi ya kutumia teknolojia ya kidijitali katika nyanja
mbalimbali za afya na kuona wapi tumefanikiwa na maeneo yapi tunahitaji
kufanya vizuri zaidi,” amesema Dkt. Swai.
Dkt. Swai amesema kongamano hili
litatoa fursa kwa washiriki kupata elimu ya teknolojia mbalimbali
zilizopo ambazo zinaweza kutumika katika maeneo mbalimbali ya utoaji
huduma za afya.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri MNH, Dkt. Ellen Mkondya amesema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
ndio hospitali kubwa nchini inapaswa kujizatiti kwenye eneo la
teknolojia katika utoaji wa huduma za afya ili kusaidia hospitali za
rufaa za kanda kujifunza kutoka muhimbili.
“Teknolojia na uvumbuzi vimekuwa
sehemu ya maisha ya kila siku, hivyo ni lazima tutumie fursa hiyo
kuhakikisha kuwa maendeleo haya ya kidijitali yanasaidia utoaji wa
huduma za afya kama tiba mtandao, utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa
pamoja na kuzuia magonjwa,”amesema Dkt. Mkondya
Kongamano hilo lilitanguliwa na na
mafunzo kwenye maeneo mbalimballi ikiwamo jinsi ya kufanya utafiti,
namna ya kuandika miradi ya maendeleo na namna ya kutumia TEHAMA katika
kufanya utafiti.
Katika kongamano hilo mada
mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa ikiwemo utunzaji wa kumbukumbu za
wagonjwa kieletroniki, sheria na kanuni zinazosimamia tiba mtandao,
uzoefu na changamoto za tiba mtandao, saikolojia ya mitandao ya kijamii
na mchango wa mitandao ya kijamii katika sekta ya afya.
No comments :
Post a Comment