
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani (Ocean Road), Dkt.Julius
Mwaiselage, akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani), kuhusu
mafanikio ya Taasisi hiyo kwa miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam.
*****************************************
SERIKALI kupitia Taasisi ya
Saratani Ocean Road (ORCI) imenunua na kusimika mashine mbili za kisasa
za huduma ya uchunguzi na tiba za kutibu saratani aina ya LINA na CT
Simulator zenye thamani ya Tsh Bilioni 9.5/- hatua inayolenga kupunguza
muda wa kusubiri
tiba mionzi kutoka wiki sita hadi kufikia wiki mbili.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu
(Desemba 2, 2019) Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI,
Dkt. Julius Mwaiselage wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari
kuhusu mafanikio ya ORCI katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Tano unaoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.
Dkt. Mwaiselage alisema mashine
hizo za kisasa zinazotumia teknolojia ya 3D zinapatikana katika
hospitali yoyote kubwa ya saratani duniani kama India, Ulaya na
Marekani, ambapo tangu mashine hizo zianze kutoa huduma za uchunguzi na
tiba mwezi Septemba 2018 tayari wagonjwa 1,141 wamepatiwa matibabu.
‘’Kwa wagonjwa 1,141 waliotibiwa
kwa kipindi hicho, takribani wagonjwa 208 wangepelekwa nje ya nchi
kama mashine hizi zisingekuwepo na hivyo Serikali imeweza kuokoa Tsh.
Bilioni 10.4 ambazo zingetumika kutibu wagonjwa hao nje ya nchi ambapo
mgonjwa mmoja hugharimu Tsh Milioni 50’’ alisema Dkt. Mwaiselage.
Dkt. Mwaiselage alisema mshine ya
CT Simulator imesaidia kuanzisha huduma za kupima CT Scan katika taasisi
hiyo ambapo hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, jumla ya wagonjwa
1,430 walikuwa wamepata kipimo cha CT Scan, hivyo kupunguza usumbufu kwa
wagonjwa ambao walitakiwa kwenda hospitali nyingine kupata huduma hiyo.
Kuhusu rufaa za wagonjwa kwenda
nje ya nchi, Dkt. Mwaiselage alisema katiks mwaka 2015, jumla wagonjwa
164 wa saratani walipatiwa rufaa kwenda nje ya nchi, lakini baada ya
kuboresha huduma za saratani nchini, kuanzia mwaka 2018 hadi 2019 ni
wagonjwa 39 pekee waliosafirishwa nje ya nchi, ambapo wagonjwa hao wengi
walikuwa wakienda nje kwa upasuaji na tiba mionzi ya kisasa.
Akibainisha mafanikio mengine,
Dkt. Mwaiselage alisema ORCI pia imekarabati wodi mbili za kutolea tiba
kemia ikiwemo kufungwa viyoyozi na kununua vitanda maalum vya kutolea
tiba kemia hivyo kuongeza utoaji wa tiba kemia kutoka wagonjwa 40 kwa
mara moja hadi wagonjwa 100 kwa mara moja, ambapo awali huduma hiyo
ilikuwa inatolewa katika wodi 1 pekee.
‘’Kuongezeka kwa wodi na vitanda
imesaidia kupunguza muda wa kuanza tiba kemia kutka siku 10 hadi tatu
pekee, ikimaanisha mgonjwa anaweza kuanza tiba ndani ya siku tatu kama
majibu ya vipimo vyake vyote vitakuwa sawa kupata tiba hiyo’’ alisema
Mwaiselage.
Aidha Dkt. Mwaiselage anasema
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia na Wazee na
Watoto imewezesha kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa dawa kutoka
asilimia 4 mwaka 2014/15 hadi kufikia asilimia 95 mwaka 2018/19, na
upatikanaji wa dawa upo kwa asilimia 100 kwa wagonjwa wenye saratani za
mlango wa kizazi, matiti, Kaposi sarcoma, tezi dume, njia ya chakula,
kooni, damu, matezi, ngozi na kibofu cha mkojo.
Akifafanua zaidi Dkt. Mwaiselage
alisema asilimia 5 ya dawa zinazopungua, hupatikana katika Duka la Dawa
la Jamii la Taasisi ililolianzisha ili kuimarisha upatikanaji wa dawa
za saratani na dawa zake hupatikana kwa bei nafuu sana ulikinganisha na
maduka mengine ya binafsi.
Dkt. Mwaiselage alisema kuwa
kutokana na kuimarika kwa huduma za saratani katika taasisi hiyo,
wagonjwa kutoka nchi jirani za Kenya, Comoro, Malawi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, na Burundi wameongezeka kuja kupata huduma za
tiba saratani na hivyo kuongeza mapato ya Taasisi kwani wananchi wasio
raia wanalipia huduma hizo.
No comments :
Post a Comment