Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa
ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga akiongea na Wahariri wa vyombo
vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya mfuko huo, Leo 02/12/2019 Jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama
wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Christopher Mapunda
akiwasilisha mada kwa Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu masuala
mbalimbali ya mfuko na kuanzishwa kwa vifurushi via Bima ya Afya, Leo
02/12/2019 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa
ya Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga Akiwa katika picha ya Pamoja na
Wahariri wa vyombo vya habari, Leo 02/12/2019 Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari nchini wakisikiliza uwasilishaji wa mada
mbalimbali kuhusu Maendeleo ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na
uanzishwaji wa Vifurushi vya Bima ya Afya.
……………….
Na Mwandishi Wetu.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) umesema upo imara na unaweza kujiendesha na
kutoa huduma kwa
wanachama wake hadi mwaka 2024 bila kupokea michango yoyote kutoka kwa
wanachama
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu
wa NHIF, Bw. Bernard Konga kwenye mkutano kati ya Mfuko na Wahariri wa
vyombo mbalimbali vya habari uliofanyika Dar es Salaam leo, kuelezea
manufaa ya mpango wa vifurushi vipya
“Naomba niseme wazi kuwa Mfuko
haujayumba wala kutetereka kifedha kama inavyodaiwa, tathmini ya Uhai wa
Mfuko inaonesha tunao uwezo wa kuwahudumia wanachama wetu kuanzia sasa
mpaka mwaka 2024 bila kupokea michango yoyote kutoka kwa wanachama,
hivyo madai yanayoenezwa sio ya ukweli,” alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa madai ya
ucheleweshaji wa kulipa madai kwa baadhi ya watoa huduma hayatokani na
kukosa fedha za kulipa bali inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo
kujiridhisha kwa madai hayo.
“Kuna sababu nyingi za
kuchelewesha madai, yapo madai yanakuja na viashiria vya udanganyifu
hayo huwezi ukalipa mapema ni lazima uhakikishe umejiridhisha ili ulipe
fedha halali na ulinde fedha za wanachama zisitumike isivyo halali,”
alisisitiza Bw. Konga.
Akizungumzia uanzishwaji wa
vifurushi vipya, alisema kuwa vifurushi hivyo vina lengo la
kuwahakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu wananchi wote
watakaojiunga na mpango huo.
Alisema kuwa vifurushi hivyo
vimebeba huduma zote za matibabu ya msingi ambayo mwananchi aliyejiunga
na vifurushi hivyo ana uwezo wa kupata huduma za matibabu katika vituo
vyote vilivyosajiliwa na Mfuko Tanzania Bara na Zanzibar.
“Mfuko haujabuni vifurushi hivi
kwa lengo la kuongeza mapato ya Mfuko. Vifurushi ni kwa ajili ya kifikia
watanzania wengi walio katika sekta binafsi ambao hawana fursa yoyote
ya kupata bima binafsi hivyo niwatoe wasi wasi wananchi juu ya mpango
huu, ni mpango ambao una manufaa kwa ajili ya afya za wananchi,” alisema
Bw. Konga.
No comments :
Post a Comment