
****************************************
NA MWAMVUA MWINYI, Bagamoyo
Nov 27
Baadhi ya wakazi wa
kitongoji cha Mtambani Kimarang’ombe Kata ya Nianjema Bagamoyo mkoani
Pwani, wanaodai kutapeliwa ardhi yao ya hekari 34 ,wamemtaka Waziri wa
ardhi William Lukuvi ,serikali ya mkoa na wilaya kuwasaidia kurejeshewa
eneo lililovamiwa ili waishi kwa amani.
Wakizungumza kwa
niaba ya wenzao na Waandishi wa habari katika eneo hilo Fatuma
Ramadhani, Hussein Temo, Isdory Mwepong’we na Makolega Turuka,
walielezea masikitiko yao ya kutakiwa kuondoka katika eneo waliloishi
miaka 40 sasa.
Fatuma alisema
,walifika kwenye eneo hilo mwaka 1974 wakianza kulima, kabla ya Mkuu wa
wilaya miaka hiyo Shaaban Kandoro kufika katika eneo hilo, akimtaka
mmiliki na kukuta pori kubwa.
“Alipofika alituuliza
mmiliki, na alitoa miezi mitatu kwa viongozi wamtafute mmiliki, kama
hajajitokeza eneo hilo ataligawa kwa wananchi waliokuwepo, huku
akiwataka viongozi wa kijiji wakati huo na kata kumfatuta,” alisema
Fatuma.
Nae Hussein Temo
alieleza baada ya muda aliouweka Mkuu huyo wa wilaya wakati huo
kumalizika pasipo kupatikana mmiliki, akaamua kuwagawia eka mojamoja
kila mtu akaanza kuyaendeleza kwa kilimo, huku wengine wakijenga nyumba
za muda.
“Tulishangazwa
ulipofika mwaka 2010 kuwaona watu wakiwa na darubini wanapima maeneo
hayo pasipokujulishwa, tuliitana na kukubaliana kwenda kwa viongozi wa
Kijiji, ambapo Mwenyekiti akatuambia hata yeye hana taarifa ya zoezi
hilo,” alisema Temo.
Kwa upande wake
Makolega Turuka alihoji uhalali wa Omary Sud ambaye kwa sasa ni
marehemu, ambaye ni mkazi wa Bagamoyo alikuwa wapi kwa zaidi ya miaka
40, na kusema kuna mchezo mchafu wa kutaka kuwaondoa wananchi hao kisha
wapige bei.
“Kesi ilifunguliwa
mahakamani na kufikia 2010 Sud alikiri eneo hilo si lake ,na kesi
ilifutwa kisha kusema walionunua kupitia yeye warudishe fedha ama
kuwalipa fidia wazee hao”
Akizungumzia sakata
hilo,ofisa ardhi wilayani hapa Wendeline Izana alisema kuwa, taarifa
hizo alipatiwa na Ofisa Mtendaji Kata kwamba eneo hilo ni la Omari Sud.
Mwenyekiti wa
Kitongoji hicho Yussuph Mgala alisema kwamba analitambua eneo hilo miaka
mingi kabla hajashika wadhifa huo, na kwamba linamilikiwa na Sud kabla
ya kuwapatia wananchi hao walime mazao ya muda mfupi, na kwamba 2010
alifika kwa ajili ya kupima viwanja.
Mtendaji Kata wa
Nianjema Sezary Madasha alifafanua, anatambua eneo hilo ni la Sud, hivyo
aliwashauri wananchi hao wakafungue mashitaka katika mahakama ambayo
ndio yenye maamuzi kisheria.
No comments :
Post a Comment