Thursday, October 31, 2019

Dkt. Abbasi, Bosi PSSSF Watatua Kero ya Walimu Papo kwa Papo Simiyu



Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) jana mkoani Simiyu. Mkutano huo umewakutanisha walimu kutoka mikoa ya Kagera, Mwanza, Kigoma, Mara, Tabora, Shinyanga, Geita na wenyeji Simiyu.
******************************
Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali,  Dkt. Hassan Abbasi, jana jioni alilazimika  kumpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Hoseah Kashimba ili kutatua kero za walimu waliodai kuna wenzao wamestaafu hawajalipwa mafao yao.
Tukio hilo lilijitokeza wakati Dkt. Abbasi akijibu hoja za walimu mara baaya ya kuwasilisha mada wakati wa Mkutano ulioandaliwa  na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na walimu kutoka mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita, Mara, Tabora na Kagera 
Katika mkutano huo walimu walitaka kujua ni lini Serikali italipa pesheni kwa wastaafu ambao hawajalipwa kwa muda mrefu.
 Dkt. Abbasi alionesha kushangazwa na hali hiyo kwani aliwaeleza wanasemina hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, imeachana na utamaduni wa zamani wa kulimbikiza madeni yasiyo na sababu.
Alitoa mfano kuwa licha ya TZS Bilioni zaidi ya 40 zilozotolewa mwaka 2017 kulipa madeni ya wastaafu, Serikali ya Rais Magufuli pia ilihakikisha kati ya hizo TZS Bilioni 16 zinahusu walimu.
Akaongeza kuwa  hata mwaka huu kati ya Julai na Septemba Serikali imelipa madeni yanayofikia TZS Bilioni 85.62 ambapo kati ya hizo TZS Bilioni 50 ni madai ya pensheni, Bilioni 22 ni madai mbalimbali ya watumishi wa umma na nyingine ni wadai wa sekta binafsi.
Kutokana na madai ya kuwepo wastaafu wa kada ya elimu ambao hawajalipwa muda mrefu, baadhi wakidai kuwa ni mwaka mzima, Dkt. Abbasi alimpigia simu na kumuunganusha moja kwa moja kwenye kipaza sauti Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.
Akijibu  hoja hiyo,  Bw. Kashimba alisema kuwa Serikali kupitia PSSSF imeendelea kuwalipa pensheni wastaafu wote kwa wakati na kutoa ofa kwa mwalimu yeyote ambaye hajalipwa kwa muda mrefu alete vielelezo suala lake litafanyiwakazi haraka.
“Mmesikia wenyewe, kama nilivyosema, Serikali ya Rais Magufuli ni ya kisayansi. Hili sasa limekwisha, sio kulalamika tena lete ushahidi wa majina na namba ya malipo ya mishahara ya mtumishi husika, suala lake litatatuliwa haraka,” alisema Dkt. Abbasi kuwaeleza walimu hao waliokuwa na furaha tele baada ya ofa ya Mkurugenzi wa PSSSF.
Baadhi ya walimu hawakuwa na vielelezo husika lakini wachache waliwasilisha nyaraka zao na zinafanyiwa kazi.
Dkt.  Abbasi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Mkoa wa Simiyu,  ambapo awali aliudhuria hafla ya kufunga Kambi za Kitaaluma kwa Wanafunzi wa  Kidato cha Nne katika mwaka 2019.

No comments :

Post a Comment