Watanzania wametakiwa kuyafanya
majukumu ya kitaifa wanayopewa na viongozi wa serikali kwa uzalendo
usiotiliwa mashaka,uamini na ufanisi kama walivyoelekezwa wakati wa
kukabidhiwa majukumu hayo kwa faida ya Nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John
Kabudi wakati akitoa Kongole kwa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed
Salim kufuatia kitendo cha kukabidhiwa Nishani ya Juu ya Urafiki ya
Jamhuri ya Watu wa China nishani ambayo inamfanya Dkt. Salim kuwa
mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya
China.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa
nishani aliyokabidhiwa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim
imeliletea heshima kubwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nay
eye mwenyewe kutokana na utendaji wake usiotiliwa mashaka baada ya
kuaminiwa na kukabidhwa majukumu hayo na Rais wa kwanza wa Tanzania
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuwataka Watanzania wote
hususani vijana kuiga mfano huo.
Amesema Dkt Salim Ahmed Salim
ni Mtumishi mwaminifu na mzalendo kwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye ameitumikia nchi katika nafasi mbalimbali kuanzia na
ukurugenzi katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika
Mashariki balozi katika nchi za Misri,India,China na Umoja wa Matifa
lakini pia ,Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Waziri wa Mambo
ya Nje,Naibu waziri Mkuu kisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na baadae Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Nishani hiyo iliyotolewa na
Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping ilipokelewa na
Bi. Maryam Salim, Binti ya Dk. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya Baba yake
kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za kiafya.
Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Mbelwa Kairuki.
Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya
kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na
Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Wang Qishan, Waziri
Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang, Spika wa Bunge Mheshimiwa Li Zhanshu na
Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza
la Taifa.
Nishani ya Juu ya Urafiki ya
Taifa la China imetolewa kwa Dkt. Salim kutokana na mchango wake wa
kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa
mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa.
Aidha, mchango wa Dk. Salim
katika kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania wakati
aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa
Nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk.Salim katika kujenga mahusiano
kati ya China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa
kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa Nishani.
Kwa upande wake Balozi wa
Tanzania nchini China Balozi Mbelwa Kairuki amesema mamilioni ya Wachina
hususani vijana wamepata fursa ya kufahamu nafasi na mchango wa
Tanzania na Bara la Afrika katika historia ya taifa lao.
Aidha, tukio la leo
limeifanya Tanzania kufahamika kwa watu wengi zaidi nchini China kupitia
tukio mara moja. Hatua hiyo itaamsha udadisi na hamasa miongoni mwa
Wachina wengi wa kizazi kipya kutaka kuifahamu zaidi Tanzania. Hali hii
yaweza kujitafsiri katika fursa kubwa ya kukua kwa utalii, biashara na
wawekezaji ikizingatiwa kuwa wananchi wa China hutoa mwitikio mkubwa
kwa nchi ambazo husemwa vizuri na kuthaminiwa na Serikali yao.
No comments :
Post a Comment