Sunday, September 29, 2019

HATIFUNGANI NI FURSA YA JAMII KUITIKIA WITO WA JPM KUJIKOMBOA KIUCHUMI


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa UTT AMIS, Simon Migangala.
Rais Dkt. John Magufuli Aakimkagua samaki na kumnunua kwa mfanyabiashara wa soko la Samaki Feri, jijini Dar es Salaam alipofany ziara ya kutembelea wafanyabiashara wadogo wanaotumia vitambulisho vya wajasiriamali ambao wanaweza kukuza mtaji wao kupitia uwekezaji kwenye Mfuko wa Hati Fungani.
……………………
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wengi wanatafuta mafanikio maishani mwao lakini bila kuwa na bidii,
ustahimilivu, nidhamu na shauku kubwa, huwezi kupata mafanikio ya kweli.
Kuna mbinu mbalimbali ambazo kila mwananchi anayetafuta mafanikio anaweza kuzitumia ili kufikisha lengo alilonalo.
Jambo la kwanza ni kujua unataka nini, ukijua unachotaka utakuwa na msimamo wa kutaka kufikia malengo yako.
Kama hujui unachotaka, jambo la msingi, chukua kalamu na karatasi kisha jiulize unataka kufanikiwa kitu gani?
Ni muhimu wakati unajiuliza, usifikirie mawazo hasi au mabaya ya kujiona kama utashindwa kufanikiwa bali kiajimi.
Ondoa wasiwasi wowote ambao utakuwa nao, orodhesha mambo yote unayotaka kufanikiwa, anza kupanga mipango kwa kujiwekea malengo, kutekeleza moja baada ya jingine.
Utajiri siyo fedha ambazo mtu anakusanya bali ni fedha ambazo huwekwa na kufanya kazi.
Tamaduni zetu zimeifanya jamii kubwa kuhifadhi fedha ndani kwenye vyungu, magodoro hata vibubu. Njia hizo zimekuwa zikibadilika taratibu sawa na ukuaji wa elimu na teknolojia.
Uwekaji akiba na uwekezaji ni dhana mbili tofauti. Uwekaji akiba ni tabia nzuri lakini bila kuziwekeza ni bure.
Ili uwe muwekaji akiba mzuri, unapaswa kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwani uwekezaji una uwiano mkubwa na muda. Muda unapozidi kuwa mrefu na uwekezaji wako unazidi kukuwa mkubwa. Mara zote pesa ndani ya uwekezaji UTT AMIS zinawekezwa katika mpango wa faida jumusihi ambapo muda huwa ni jambo la msingi kabisa.
UTT AMIS ni taasisi ya Serikali ambayo imepewa dhamana ya usimamizi wa mali kupitia Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.
Nchini Tanzania unaweza kuwekeza fedha zako katika masoko ya fedha, mitaji. Hatua hiyo inahusisha akaunti za muda maalum na zisizo za muda maalum katika benki za biashara.
Pia hati fungani za Serikali za muda mfupi, mrefu, kampuni na hisa zilizo orodheswa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ambazo zina nafasi kubwa ya kurejesha gawio zuri.
Uwekezaji unaofanywa na taasisi hiyo kupitia mifuko ambayo wanaisimamia ni fursa mbadala inayowezasha mtu, watu, vikundi, taasisi, kampuni kuwekeza pesa zao kwa Meneja wa UTT.
Meneja wa mfuko huzichukua fedha hizo, kuziwekeza kwenye masoko ya fedha na mitaji kulingana na waraka wa makubaliano. Waraka wa makubaliano ni maandiko ya kisheria yanayo zungumzia haki za pande zote mbili meneja na mwekezaji pia huanisha sehemu za kuwekeza na uwiano wa kuwekeza.
Faida inayopatikana hugawanywa kwa wawekezaji kulingana na uwiano wa uwekezaji uliofanyika kwenye mfuko husika. Awali UTT ilipewa dhamana ya usimamizi wa mifuko mitano.
Mifuko hiyo ni Mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha, Watoto, Mfuko wa Kujikimu na Mfuko wa Ukwasi. Hivi sasa taasisi hiyo imeongeza mfuko mwingine wa Hati Fungani.
Mfuko wa Umoja, ulioanzishwa Mei 16, 2005 ukilenga kutimiza mahitaji tofauti ya wawekezaji. Awali bei ya kipande ilikuwa sh. 70, kwa sasa sh. 582.
Sifa zilizopo katika mfuko huo ni vipande kuuzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga). kiwango cha chini cha kujiunga ni vipande 10 tu, malipo ya mauzo hutozwa asilimia moja ya thamani halisi, pia ni rahisi kujiunga na  kutoka,  manunuzi na mauzo hufanyika kila siku ya kazi.
Mfuko wa Watoto una lengo la kuwasaidia watoto katika maendeleo yao nchini. Awali bei ya kipande ilikuwa sh. 100, mfuko ulianzishwa Oktoba 1, 2008.
Na  kwa sasa thamani ya kipande katika mfuko wa watoto ni shilingi 348 Sifa za mfuko huo ni uwekezaji kwa ajili ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 18. Kiwango cha chini cha uwekezaji sh. 10,000, unaruhusiwa kuwekeza kidogo kidogo kwa sh. 5,000.
Sifa nyingine ni vipande kuuzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga), mfuko hutoa mipango ya aina mbili, kwanza malipo ya ada, pili mpango wa kukuza mtaji.
Malipo ya ada na mauzo ya vipande yanaruhusiwa pale mtoto anapofikisha miaka 12. Mfuko huo ni miongoni mwa mifuko  inayotatua changamoto za kielimu hasa katika ulipaji ada kwa wanafunzi, kutoa mtaji baada ya ukomo wa shule kufikia.
Pia mfuko una mipango miwili mikubwa, mpango wa ada za shule na mtaji kwa mwanao. Ili mzazi aweze kuchangia kupitia mfuko huo, anapaswa kuweka sh. 10,000 kima cha chini na hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu. Mwekezaji anaweza kuwekeza mara kwa mara kadri anaweza.
Mfuko wa Jikimu una lengo la kukidhi mahitaji ya wawekezaji wanaohitaji uhakika wa mapato ya mara kwa mara, ulianzishwa  Novemba 3, 2008 ukiwa na sifa za mipango ya uwekezaji, kiwango cha uwekezaji, mpango wa gawio robo mwaka.
Kiwango cha chini kuwekeza  ili kupata gawio mara nne kwa mwaka yaani kila robo mwaka ni shilingi  milioni 2. Mpango wa gawio wa mwaka (kiwango cha chini cha uwekezaji sh. milioni moja), tatu mpango wa mwaka wa kukua (sh. 5,000).Vipande vinauzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga).
Mfuko wa Ukwasi unaotoa nafasi ya uwekezaji mbadala kwa wawekezaji wakubwa au taasisi ambao wangependa kuwekeza fedha zao za ziada kwa kipindi kifupi ama cha kati huku wakikuza mtaji wao.
Ulianzishwa Aprili 30, 2013, bei ya kipande ikiwa sh. 100.00, hivi sasa imepanda hadi zaidi ya sh. 219 hii ikiwa ina maana ya kuwa mfuko umekua mara 2.19 ndani ya miaka mitano au umekuwa kwa asilimia 119 huu ni ukuwaji mzuri sana kibiashara.  Sifa za mfuko huo ni rahisi mwekezaji kupata fedha zake za mauzo ya vipande ndani ya siku tatu za kazi baada ya maombi ya kuuza vipande kupokelewa Makao Makuu ya UTT AMIS.
Mfuko huo hauna ada ya kujitoa wala kujiunga, una unafuu wa gharama za uwekezaji, unafaa kwa wawekezaji mmoja mmoja au taasisi, kiwago cha chini cha kuwekeza sh. 5,000,000.00.
Kuongeza uwekezaji wako sh. 1,000,000.00, pia unaruhusu uhamishaji vipande kutoka kwa mwekezaji mmoja kwenda mwingine, kuruhuusu uhamishaji vipande kwenda kwenye mifuko mingine, kuviuza kwa thamani halisi.
Mfuko wa Wekeza Maisha unamwezesha mwekezaji kupata faida pacha (mapato mazuri pamoja na mafao ya bima).
Mfuko huo ulianzishwa Mei 16,2007, wawekezaji kati ya miaka 18 na 55 ndio wanaoruhusiwa kujiunga. Unatoa mipango ya aina mbili, kuchangia uwekezaji awamu ya kwanza, mkupuo mmoja.
Vipande vinauzwa kwa thamani halisi, hakuna gharama za kujiunga. Kujiunga ni sh. 8,340.00 tu kwa mwezi. Mafao ya bima yanayopatikana ni bima ya maisha, ulemavu wa kudumu na bima ya ajali.
Mfuko unamwezesha mwekezaji kuwekeza kwa mpangilio, kuchangia kwa mwezi, mara mbili kwa mwaka, mara moja kwa mwaka ambapo faida za uwekezaji katika Mifukoya Uwekezaji wa Pamoja ni kukuza mtaji kwa kutoa faida nzuri ukilinganisha na mifuko mingine kwenye masoko ya fedha.
Faida nyingine ni kutawanya hatari za uwekezaji, mwekezaji hupunguza athari za uwekezaji kwa kuwekeza katika uwekezaji anuai, wawekezaji kufaidika na unafuu wa gharama za uwekezaji.
Pia wawekezaji wanaweza kufuatilia maendeleo ya masoko ya fedha kwa kufuatilia maendeleo ya mifuko.
Mfuko mpya Hati Fungani unaojulikana kama ‘Bond Fund’ ni kati ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja inayoendeshwa na UTT AMIS ulioanzishwa kwa malengo maalum.
Malengo hayo ni kubuni, kuendeleza, kuanzisha na kusimamia Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja, kuwekeza, kununua, kumiliki na kuuza dhamana, kutimiza malengo, wajibu, haki na sheria.
Mengine ni kutoa huduma za usimamizi wa fedha kwa kampuni na wawekezaji binafsi, kutoa ushauri wa uwekezaji kwa taasisi na watu binafsi, kutunza taarifa za wawekezaji wa mifuko na kuhamasisha wananchi kujiwekea akiba.
Kuanzishwa kwa Mfuko wa Hati Fungani kumetokana na mahitaji ya wawekezaji na uchambuzi wa bidhaa za kifedha zilizoko kwenye soko la mitaji kwa sasa.
Mfuko utawawezesha wawekezaji wadogo na wa kati kuzifikia fursa za uwekezaji ambazo kwa hali ya kawaida ni wawekezaji wachache na wakubwa ndio wanaozifikia.
Pia utawekeza kwenye hati fungani zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa kwa asilimia 90 na asilimia 10 itakuwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.
Lengo ni kuwawezesha wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha kutokana na uwekezaji wao katika mfuko wafanye hivyo.
Mfuko umeundwa ili kumwezesha kila mwekezaji kuchagua kama anapenda kukuza mtaji au kupokea gawio kwa mwezi, kila miezi sita kutokana na mahitaji yake ya kifedha.
Sheria ya Masoko ya Mitaji inataka Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kuwa na Meneja, Mdhamini, Wakaguzi wa Mahesabu, Wanasheria na Msajili.
Mfuko huo utasimamiwa na UTT AMIS kama Meneja na Benki ya CRDB kama Mdhamini. Utakaguliwa na KPMG ambayo ni taasisi ya kimataifa ya ukaguzi wa mahesabu ya fedha.
Wanasheria watakuwa Kampuni ya Abenry and Company ambao wana uzoefu mkubwa katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja na Msajili atakuwa UTT AMIS.
Akiuzungumzia mfuko huo, Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga, alisemaumelenga  kuondoa changamoto ambazo wawekezaji wanakutana nazo.
Anasema soko la fedha lina bidhaa nyingi zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya watumiaji.
Baadhi ya bidhaa hizo zinaeleweka kirahisi hata namna ya kuzifikia na kuwekeza lakijni wakati mwingine hazitoi faida shindani kwa wawekezaji.
Anasema baadhi ya wawekezaji hasa wadogo ni vigumu kuwekeza kwenye baadhi ya bidhaa katika soko la fedha. Mfuko wa Hati Fungani umeratibiwa ili kuondoa changamoto hizo.
Mwekezaji anapata faida sawa na wawekezaji wakubwa, akihitaji fedha anauza baadhi ya umiliki wake kwenye mfuko kwa utaratibu rahisi bila kupoteza faida aliyoipata.
Pia mfuko huo unawafaa wawekezaji wakubwa kwa sababu ya faida shindani, gharama ndogo za kuwekeza, ukwasi wa kutosha, usalama wa mtaji, hatari ndogo za uwekezaji.
Mfuko unatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza, kushiriki katika masoko ya mitaji, kufaidika na uwekezaji huo.
Kwa mantiki hiyo, mfuko umeandaliwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa kipato cha chini, kati na kipato cha juu ambapo watu binafsi, kampuni, taasisi na vikundi rasmi wanaweza kushiriki katika uwekezaji kwenye mfuko huo.
Lengo kuu la mfuko ni kuwawezesha wawekezaji katika ushiriki mpana kupitia uwekezaji wa vipande na kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba kupitia hati fungani, masoko ya fedha.
Mfuko huo hutoa fursa ya uwekezaji rahisi wa muda mrefu kwa wawekezaji ambao wangependa kuwekeza ili kukuza mtaji wao, kupata gawio kila mwezi au kila baada ya miezi sita kama mwekezaji anavyohitaji.
Mbaga anasema, mfuko una mipango miwili ya uwekezaji ili kukidhi matakwa tofauti ya wawekezaji. Kuna mpango wa kukuza mtaji, gawio kila mwezi na gawio kila miezi sita, mpango wa kukuza mtaji.
Gawio la mara kwa mara halitatolewa kwa wawekezaji badala yake faida iliyopatikana itarudishwa kwenye uwekezaji wa awali kwa kununua vipande vitakavyonunuliwa kwa bei ya wakati huo.
Mpango huo utawafaa wawekezaji wanaohitaji kuweka akiba kwa malengo maalum mfano kujenga nyumba au wafanyakazi wenye kipato kama wangependa kuwa na fedha ya akiba.
Wawekezaji katika mpango huo wanaweza kuuza kiasi chochote cha uwekezaji wakiwa wamekidhi vigezo vinavyohusu uuzwaji wa vipande. 
Wawekezaji wanaohitaji kuchukua faida kila mwezi kama  wastaafu wanaopata fedha zao za mkupuo, kuwekeza kwenye mfuko, wanashauriwa kuchagua kupokea gawio kila mwezi ili wapate kipato cha kuishi bila kupoteza fedha walizopata.
Mbaga anasema wawekezaji wengine wanaopata fedha nyingi mara moja mfano wachimba madini, wanaweza kuchagua gawio kila mwezi ili wafanye shughuli zao bila kuathiri mtaji wao.
Pia wawekezaji watakao jiunga na mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vyote ili mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko vinavyohusu uuzwaji vipande.
Mpango wa gawio kila miezi sita, Mbaga alisema hutegemea na mahitaji ya fedha ya mwekezaji na anavyochagua kwenye fomu ya maombi ya kuwekeza kwenye mfuko.
Kwa wawekezaji ambao wanahitaji kuchukua faida kila miezi sita mfano wafanyakazi wanaohitaji kuweka kiasi cha fedha ili faida inayopatikana itumike kulipa ada kusomesha watoto, wanaweza kuchagua kupokea gawio kila miezi sita.
Pia kuna wawekezaji wanaopata fedha nyingi mara moja kama wakulima wa mazao mbalimbali ya msimu, wanaweza kuchagua kupata gawio kila miezi sita.
Lengo ni kupata fedha wakati wa kutayarisha, kulima mashamba na wakati wa kuvuna ili waweze kuendesha shughuli zao kwa kufuata msimu bila kupoteza mtaji walio nao. Pia hawa wanahitaji pesa wakati wote huku kilimo kikiwa ni cha msimu mpka msimu. Wakati wanasubiri msimu mpya wana chukuwa pesa za kwa mwezi ili kukidhi mahitaji ya kila siku.
Wawekezaji watakao kujitoa kutoka  mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vipande vyote ili mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko.
Akizungumzia sera ya uwekezaji, Mbaga anasema muundo wa mgawanyo katika mfuko wa Hati Fungani unatoa mapato ya muda mrefu ikijumuisha hati fungani zinazotolewa na Serikali.
Uwekezaji kwenye hati fungani ili mfuko uwe na mapato ya kudumu utakuwa si chini ya asilimia 90 ya thamani ya mfuko, asilimia 10 itawekezwa kwenye rasilimali zenye ukwasi ili wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha wafanye hivyo.
Meneja atawekeza kwenye rasilimali zenye ukwasi ili kuhakikisha uwezo wa kulipa wawekezaji pale fedha zao zitakapohitajika unakuwa imara.
Mbaga anasema wawekezaji wote wa ndani, nje ya Tanzania kama Sheria ya Soko la Mitaji na Dhamana inavyoruhusu wanaweza kuwekeza kwenye mfuko huo.
Kuhusu ununuzi wa vipande, alisema vinanunuliwa siku yoyote ya kazi isipokuwa kipindi cha kufunga vitabu ambacho hakitazidi siku saba za kazi.
Kuanzia Septemba 16 hadi Oktoba 16, mwaka huu itakuwa kipindi cha mauzo ya awali hivyo Watanzania wachangamkea fursa hiyo kwani kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000 na thamani halisi ya kipande itakuwa sh. 100.
Maombi ya kununua vipande yanaweza kuwakilishwa katika tawi lolote la Benki ya CRDB, ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam; Ofisi za Shirika la Posta; Wakala yoyote atakayeteuliwa na UTT AMIS.
Wawekezaji walio nje ya Tanzania anayetaka kuwekeza katika mfuko huo awasiliane na ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au kuwasiliana moja kwa moja na Ofisi za UTT AMIS ili kupata taarifa na muongozo zaidi.
Anaongeza kuwa, thamani ya mwanzo ya kipande itakuwa sh.  100. Thamani ya kuuza na kununua kipande itakuwa sawa na thamani halisi ya kipande bila gharama yoyote.
Kiwango cha chini kitakuwa sh. 50,000, hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu ambapo hiyo ni fursa kwa kila Mtanzania.
Baada ya muda wa mauzo ya awali, mwekezaji anaweza kuwekeza kuanzia sh. 5,000, mara nyingi kadri awezavyo.
Malipo ya mauzo ya vipande yanaweza kufanywa kwa fedha taslimu au hundi ya benki itakayolipwa kwenye akaunti ya ‘Mfuko wa Hati Fungani’ iliyopo Benki ya CRDB.
Wawekezaji wanaweza kwenda kwenye tawi lolote la Benki ya CRDB na kufanya malipo. Pia malipo yanaweza kufanyika kwa kupitia M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money.
Kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa Kukuza Mtaji ni vipande 500. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 50,000.
Unaposema Mfuko wa Kukuza Mtaji maana yake mwekezaji atakuwa anawekeza mara kwa mara kwa malengo Fulani ili kutimiza azima fulani huko mbele. Na kila anacho wekeza kitakuwa kinakuwa kutokana na mwenendo wa soko
Kuhusu mpango wa gawio kila mwezi, kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa mpango wa gawio kila mwezi ni vipande 100,000. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 10,000,000.
Mpango wa gawio kila miezi sita, kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa mpango wa gawio kila miezi sita ni vipande 50,000. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 5,000,000. Kuhusu ununuzi na mauzo ya baadaye yatakayoanza Oktoba Mosi, mwaka huu, idadi ya chini ya vipande inayoweza kuuzwa ni vipande vyenye thamani ya sh. 5,000, vitaonekana katika mgawanyo wa desimali nne.
Maombi ya mauzo, manunuzi ya vipande yatapokelewa na kukubalika siku za kazi tu.
Mauzo ya vipande yatafanyiwa kazi baada ya kupokelewa kwa fomu ya kuuza vipande ambayo itakuwa imeambatanishwa na taarifa ya akaunti, nakala ya kitambulisho, kielelezo kingine kitakachohitajika na Meneja wa Mfuko.
Malipo ya mauzo ya vipande kwenda kwa mwekezaji yatafanyika kwa njia ya benki au kupitia Shirika la Posta ndani ya siku 10 za kazi tangu kupokelewa maombi yaliyo kamili.
Lazima mwekezaji ajaze fomu ya maombi ya kujiunga ili aweze kununua vipande na kuwekeza, fomu hiyo ipelekwe kwa wakala yeyote aliyeteuliwa na Meneja wa Mfuko.

No comments :

Post a Comment