Saturday, September 28, 2019

WAZIRI MKUU MAJALIWA AMUAGIZA RC IRINGA KUFUATILIA UTENDAJI KAZI OFISI YA DC KILOLO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Iringa, Septemba 27, 2019.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happy na Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah (wa pili kushoto) kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kilolo , Septemba 27, 2019.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kilolo, Septemba 27, 2019. 
 Muonekano wa sehemu ya hospitali ya wilaya ya Kilolo ambayo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi huo  Septemba 27, 2019 na kusema kuwa amefurahishwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada kukagua na kufurahishwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kilolo, Septemba 27, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Ilula wilayani Kilolo, Septemba 27, 2019. Kushoto ni mkewe Mary, kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Jasephat Kandege, wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happy na wa pili kushoto ni Mbunge w Kilolo, Venance Mwamoto. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NA OWM, KILOLO
SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA WATENDAJI KATA 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya Watendaji Kata na askari nchini ambao wamekuwa wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu waliowapa ujauzito wanafunzi na amesema watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ameyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilula Sokoni, kata ya Nyalumbu wilayani Kilolo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.
“Wanafunzi bado wanaendelea kupewa ujauzito na kukatishwa masomo yao huku watu waliohusika na vitendo hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu baadhi ya watendaji na askari wamezikalia kesi zao na kushindwa kuwafikisha polisi.”
“Watoto wa kike lazima walindwe ili wamalize masomo yao waje kulitumikia Taifa lao. Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi.”
Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na adhabu iliyowekwa na Serikali ni kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayemuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi hususan waishio vijijini wasikubali kurubuniwa na kugawa ardhi yao kwa watu mbalimbali wanaofika kwenye maeneo yao na kutaka wauziwe ardhi bila ya kuzihusisha mamlaka husika. 
“Eneo lenu hili la Ilula ni zuri hivyo msikubali kurubuniwa kuuza ardhi yenu kwa sababau inathamani kubwa. Viongozi wa Kata na Vijiji hakikisheni mnaratibu vizuri na muandae mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro.”
Waziri Mkuu alisema wananchi hao wanatakiwa wawe makini na ardhi na mamlaka zinazohusika na ardhi lazima zihusishwe katika ugawaji wa ardhi kwa sababu wakigawa hovyo watasababisha vijana wao hapo baadaye wakose maeneo ya kilimo.
Akizungumzia kuhusu uboreshwaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu ameahidi ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Ilula ili kuwapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma hizo.
Alisema kituo kitakachojengwa kitakuwa na chumba cha kujifungulia, chumba cha maabara kwa ajili ya vipimo mbalimbali, huduma za mama na mtoto, mapasuaji, wodi ya wanaume na wanawake, aliwataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Waziri Mkuu alisema suala la kuboresha na kusogeza huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi zikiwemo za afya limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye anataka kuona wananchi wakiwa na afya nzuri ili waweze kushiriki ipasavyo katika shughuli zao za kimaendeleo.
Kabla ya kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa mradi wa maji Ilula na kuweka jiwe la msingi. Pia, Waziri Mkuu alikagua shughuli za ukarabati wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi  Ilula.
 Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege aliwahimiza wananchi hao wajiunge katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu ya bure wao na familia zao.
 Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi alisema kuwa awali eneo la Ilula lilikuwa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo yam ogogoro ya ardhi ambayo kwa kushirikiana na watendaji wenzake walifanikiwa kuitatua.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Ilula wilayani Kilolo, Septemba 27, 2019. Kushoto ni mkewe Mary, kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Jasephat Kandege, wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happy na wa nne kushoto ni Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Ilula wilayani Kilolo Septemba 27, 2019. Wa pili kulia ni mkewe Mary, wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Happy na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah. (Picha na Ofisi  ya Waziri Mkuu) 

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akiwasalimia wananchi katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Uwanja wa Ilula Sokoni wilayani Kilolo, Septemba 27, 2019. Kulia ni Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto na wa pili kushoto ni Mwenyekititi wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Abel Nyamahanga.NA OWM, KILOLO
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi afuatilie utendaji kazi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo kufuatia watumishi 14 wa ofisi hiyo wakiwemo madereva 10 kuhamishwa baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo Asia Abdallah kudai kuwa hawafanyi kazi ipasavyo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ni mhuimu kwa viongozi wakatambua dhamana zao katika utekelezaji wa shughuli zao pamoja na kuwatambua, kuwajali na kuwathamini watumishi wa kada zote wakiwemo madereva, hivyo ni vizuri wawaandae kwa kuwapa maelekezo kwa wakati kwa kuwa nao ni binadamu na wanafamilia.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Kilolo, Halmashauri ya wilaya ya Kilolo pamoja na Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa. Amesisitiza umuhimu wa watumishi hao kushirikiana.
Waziri Mkuu amesema pamoja na shughuli za maendeleo wanazofanya katika wilaya hiyo lakini hawana mshikamano, hivyo amemtaka Mkuu wa Wilaya ahakikishe anashirikiana vizuri na wenzake kwa sababu watumishi wengi wamehamishwa tangu aingie katika ofisi hiyo na hata wanaoletwa wanalalamika na wanaomba wahamishwe.
Amesema watumishi wengi katika ofisi hiyo anawaona hawana uwezo wakiwemo wasaidizi wake kama madereva, watunza kumbukumbu na makatibu muhtasi. “Hata aliyekuwa Katibu Tawala wa wilaya hii alihamishwa kwa sababu na kutoelewana na DC, na hata huyu Katibu Tawala wa Wilaya aliyepo sasa hana raha anataka kuhama kwa sababu hizo hizo.”
“Lazima tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi, lazima kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya. Hapa tujue mbovu ni nani Mkuu wa Mkoa tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai?
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “ili mfanye kazi vizuri mnatakiwa mshikamane mfanye kazi kama timu moja kwani pamoja na shughuli mnazofanya hamna ushirikiano. DC (mkuu wa wilaya) sasa utabaki peke yako utakuwa unaandika mwenyewe, unaendesha gari mwenyewe maana wote hawafai. Mkuu Mkoa nakukabidhi majina ya watumishi hao ushughulikie suala hili. Na Katibu Tawala wa Mkoa usilete watumishi wengine hapa mpaka suala hili litakapopatiwa ufumbuzi”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga kiasi cha fedha katika makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati kwenye maeneo yao kama ujenzi wa vituo vya afya, barabara za halmashauri na masoko badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
Amesema wilaya ya Kilolo ambayo haina kituo cha mabasi inatakiwa itenge fedha kutoka kwenye makusanyo yao na kuanzisha mradi wa kituo hicho ambao utekelezaji wake utaboresha huduma kwa wananchi pia, mradi huo utasaidia katika kuongeza mapato ya halmashauri. Halmashauri ya wilaya ya Kilolo inakusanya sh. bilioni nne kwa mwaka.
Waziri Mkuu amesema watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani wananchi wanahitaji waone matokeo ya uwepo wao kutokana na dhamana waliyotewa na Serikali katika wilaya hiyo. “Madiwani nanyi simamieni halmashauri yenu vizuri kwa sababu nyie ndiyo wenye dhamana ya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri.”
Awali, Mbunge wa jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya yao ikiwemo ya umeme, ambapo kati ya vijiji 94 vilivyoko vijiji 54 vimeunganishiwa huduma hiyo na vilivyosalia vitakuwa viunganishiwa umeme ifikapo Desemba mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu miradi ya maji mbunge huyo alisema kati ya vijiji 94 vya wilaya hiyo vijiji 15 tu ndio bado havina maji ya uhakika lakini wanaendelea na mchakato wa ufuatiliaji ili kuhakikisha navyo vipata maji safi na salama.”Kuhusu sekta ya elimu tatizo tulilonalo ni madai ya walimu waliohama na waliopandishwa madaraja.” Waziri Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa kazi.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kupokea taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo ambapo alisema ameridhishwa na ujenzi huo uliogharimu sh. bilioni nne na alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mkurugenzi pamoja na mkandarasi anayenga.

No comments :

Post a Comment