
Na. Aron Msigwa – WMU, Dar es Salaam.
SERIKALI
imetoa muda wa mwezi mmoja (kuanzia Septemba 4 hadi Oktoba 4, 2019) kwa
wananchi wote wanaomiliki meno ya Tembo kinyume cha sheria, kuhakikisha
wanayasalimisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba
watakaofanya hivyo kabla ya kuisha kwa muda huo hawatashtakiwa.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa muda huo
alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam mara
baada Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya Ujangili (NTAP) kukamata watuhumiwa
8 wa ujangili, vipande 338 na meno mazima ya Tembo 75 pamoja na meno
mawili ya kiboko.
“Nimewaita
hapa ili mshuhudie kazi nzuri iliyofaywa na maafisa wa Serikali na
Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti ujagili, ninatoa huruma ya mwezi mmoja
kwa kila aliye na meno ya Tembo ayasalimishe kwenye chombo chochote cha
Serikali na atakayefanya hivyo ndani ya muda huo hatutamshtaki”
Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.
Dkt.
Kigwangalla amesema kukamatwa kwa majangili hao kumetokana na kazi ya
muda mrefu ambayo imezaa matunda na matokeo yake kuonekana kwa kukamatwa
kwa majangili sugu 8 (nane) akiwemo Bw. Hassan shaban maarufu kwa jina
la Nyoni aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa kujihusisha na mtandao
wa ukusanyaji wa meno ya Tembo kutoka Tanzania na Msumbiji.
Amesema
mtuhumiwa huyo wa ujangili amekamatwa na jumla ya vipande vya meno ya
Tembo 338 na memo mazima 75 pamoja pamoja na meno 2 ya Viboko ambapo kwa
mujibu wa Wataalam na Wanasayansi wa Uhifadhi wa Wanyamapori wanaeleza
kuwa meno hayo ni sawa na Tembo 117 waliouawa.
Amebainisha
kuwa meno hayo yalianza kutafutiwa soko mwaka 2015 wakati Serikali ya
Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ilipoingia madarakani,
hivyo hatua ya Serikali kuimarisha Ulinzi wa Rasilimali za Taifa na
kukiongezea uwezo Kikosi cha Kudhibiti Ujangili soko la meno hayo
liliharibika.
Dkt.
Kigwangalla amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya tano
Majangili wengi wamekamatwa na mitandao yao kusambaratishwa akisisitiza
kuwa yeyote atakayejihusisha na biashara hiyo kwa namna yoyote ile
atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
“Mtuhumiwa
huyu amehangaika na huu mzigo kwa zaidi ya miaka minne na hili nataka
watanzania wajue ya kwamba yeyote atakayejihusisha na biashara hii ya
kuuza nyara za Serikali tutamkamata tu maana, sababu ni moja wateja
tumebaki ni sisi wenyewe popote utakapojaribu kuuza tutakukamata tu”
Aidha,
ametoa onyo kwa wananchi wanaojihusisha au kushiriki kwa namna yoyote
ile na vitendo vya ujangili waache mara moja akibainisha kuwa kazi hiyo
kwa sasa haina nafasi nchini Tanzania.
Amesema
kuwa kuanzia mwaka huu Wizara yake itaweka Mkakati mpya wa kukomesha
vitendo vya ujangili nchini hadi kufikia mwaka 2014 akieleza kwamba
mkakati huo utaimarisha kikosi kazi cha kudhibiti ujangili, kuimarisha
ushirikiano na wizara nyingine, kuimarisha Jeshi USU na kuweka muundo
mzuri utakaozuia mauaji ya wanyama.
Aidha,
amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka 3 katika Ikolojia ya Selous
hakuna Tembo hata mmoja aliyeuawa na majangili akibainisha kuwa meno ya
Tembo yaliyokamatwa Agosti 31 mwaka huu ni yale ya ujangili uliofanyika
nyuma kabla ya kuingia kwa Serikali ya awamu ya tano.
Amesema
Kikosi Kazi hicho cha Serikali kimefanikiwa kuziba mianya yote ya
biashara haramu za nyara za Serikali kwa kupambana na uharifu kwa
kufuatilia na kusambaratisha mitandao yote ya ujangili ikiwemo mali na
silaha za majangili.
Amebainisha
kuwa kazi hiyo imefanikiwa kwa kuwa kinajumuisha maafisa kutoka Wizara
ya Maliasili na Utalii na vyombo vingine vya ulinzi na Usalama na
taasisi za kisheria na kimekuwa kikifanya kazi nzuri ya kuratibu ,
kusimamia na kuchukua hatua za kupambana na uhalifu wa rasilimali za
Wanyamapori na Mazao ya Misitu kwa kuendesha operesheni zinazoongozwa na
taarifa za Kiintelijensia.
Dkt.
Kigwangalla ameongeza kuwa Kikosi Kazi hicho kinafanya uchunguzi wa
wahalifu na mali zinazotokana na uhalifu, kukamata, kupekua na
kushikilia mali za wahalifu wanaojihusisha na ujangili.
“Sasa
hivi kupitia Kikosi Kazi chetu tumeziba mianya yote, anayefanya
biashara tutamkamata, aanayewinda kwenye maeneo ya hifadhi tutamkamata
na hata askari wote wanaoshirikiana na majangili tutawakamata kwa kuwa
tukimpata jangili mmoja tunahakikisha na mtandao wake wote tumeuvunja”
Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Dkt.
Kigwangalla ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019
Kikosi Kazi hicho kimefanikiwa kukamata watuhumiwa zaidi ya 1072 silaha
539 zikiwemo siala 85 za Kivita na jumla ya risasi 37,921.
Aidha,
nyara mbalimbali za Serikali zilikamatwa ikiwa ni pamoja na meno tembo,
pembe za faru, ngozi za Simba, Chui na Duma, meno ya Kiboko, Kobe
pamoja na mazao ya Misitu.
Pia
Dkt. Kigwangalla amebainisha kuwa Kikosi kazi hicho hadi sasa
kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wakubwa wa ujangili wakiwemo Aloyce
Francis Ayubu( Kamanda), Mateso Kassiani Albano (Mateso Chupi) na
Jayzan George Kuchar (China), Haruna Kassa, Frank Silagei na Ojugu
(Original).
Wengine
ni Haong Nghia Trung, MS. Yang Feng Glan (Queen of Ivory) ambaye
amekwishahukumiwa pamoja na Salvius Francis Matembo na Manase Julius
Philemon, Boniface Maringo, (shetani), Juma Maringo (Yesu), Godfrey
James Nyamicha (Papa), Haidari Omary Sharif, Oliva Lucas Mchua na
Mrangilwa Emanueli.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia na kupata maelezo ya vipande 338 na meno mazima ya Tembo 75 pamoja na meno mawili ya kiboko yaliyokamatwa kutoka kwa watuhumiwa 8 wa Ujangili na Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya Ujangili (NTAP). Picha na Aron Msigwa - WMU.


No comments :
Post a Comment