Na. Josephine Majura na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa ongezeko
la idadi ya watu nchini ni fursa ya ukuaji wa uchumi kwa kuitumia kama
nguvu kazi ya kuzalisha mali, soko la bidhaa na huduma.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,
alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Bunda Vijijini , Mhe.
Boniface Getere, aliyetaka kujua faida ya ongezeko la idadi ya watu na
mikakati ya Serikali ya kudhibiti ongezeko hilo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, Taifa
la Tanzania bado lina rasilimali asili za kutosha kama ardhi ya
kulima, bahari, maziwa, mito, mabonde, madini, misitu, jiografia ya usafiri pamoja na fursa za utalii ambazo zikitumiwa kikamilifu, uzalishaji mali utaongezeka na kupunguza umasikini badala ya kuogopa ongezeko la watu.
kulima, bahari, maziwa, mito, mabonde, madini, misitu, jiografia ya usafiri pamoja na fursa za utalii ambazo zikitumiwa kikamilifu, uzalishaji mali utaongezeka na kupunguza umasikini badala ya kuogopa ongezeko la watu.
“Si jambo baya kudhibiti
ongezeko la idadi ya watu kama familia au Taifa limefikia kiwango cha
mwisho cha kutumia rasilimali zake za asili pamoja mikakati mingine
mbadala”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa, kwa sasa Serikali
imejielekeza zaidi katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na
kufanya biashara ili kutumia kikamilifu nguvu kazi iliyopo nchini kukuza
uchumi.
Dkt. Kijaji alisema utafiti wa
idadi ya watu Duniani unaonesha idadi kubwa ya watu ni fursa iwapo
kutakuwa na maboresho katika maisha ya watoto, elimu na uwezeshaji kwa
wanawake na kuimarisha uwekezaji katika afya ili kuwa na nguvu kazi
bora na yenye tija.
Maeneo mengine ni kuimarisha
uwekezaji katika elimu ya juu ili kuwa na nguvu kazi yenye elimu, ujuzi
na ubunifu, kufanya mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuharakisha ukuaji
wa uchumi na upatikanaji wa kazi kwa ajili ya nguvu kazi iliyopo na
mageuzi ya sera ili kuvutia wawekezaji wa kigeni na kuhakikisha
uwajibikaji hasa katika rasilimali za umma.
Aidha alieleza kuwa dhima ya
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 hadi 20220/ 2021
ni kujenga uchumi wa viwanda ili kufungamanisha ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya watu.
Alisema Mpango huo wa pili
umejikita zaidi katika uwekezaji wa kimkakati katika Sekta ya viwanda,
kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kusambaza umeme
mijini na vijijini, kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakati na kutatua
changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujenga
Bwawa la kufua umeme katika mto rufiji.
Alibainisha kuwa Mpango wa Pili
wa Maendeleo wa Miaka Mitano unalenga kuimarisha huduma za jamii kwa
kujenga na kukarabati miundombinu ya maji, shule, hospitali vituo vya
Afya vya umma, pamoja na kutekeleza kwa ufanisi sera ya Elimu bila
malipo.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa,
miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inalengo la
kufungamanisha fursa za kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu.
Matokeo chanya ya ongezeko la
watu nchini yataonekana iwapo kila Mtanzania atashiriki kikamilifu
katika uzalishaji mali na huduma za jamii kuanzia ngazi ya Kaya hadi
Taifa.
No comments :
Post a Comment