
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Museveni kabla ya
kuanza mazungumzo yao Chato mkoani Geita mapema Julai 2019. PICHA NA
IKULU.
Na Mwandishi Wetu.
MTANZANIA
mwenzangu, najua unajua kuwa siku za karibuni nchi za Tanzania na
Uganda zinatarajia kufanya Kongamano la kibiashara la pamoja ambalo
litakuwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini kwetu.
Kwa
kukumbusha tu, kongamano hilo linatarajia kufanyika kuanzia Septemba 6
hadi Septemba 7 mwaka huu katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam.
Kongamano hilo baina ya Tanzania na Uganda linatarajia kuwashirikisha wafanyabiashara wa nchi hizo.
Kongamano
hilo kwa namna moja au nyingine itakuwa fursa nzuri kwa wafanyabiashara
wa nchi hizo kubadilisha uzoefu wa kibiashara na namna nzuri ya
kuendelea kushirikiana kwa maslahi ya pande zote mbili.
Serikali
ya Awamu ya Tano chini ya utawala wa Rais mzalendo na mwenye upendo kwa
nchi Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mambo mengine ameweka msingi
imara katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata soko
kwenye nchi nyingine zikiwemo za Afrika Mashariki.
Kauli
mbiu ya Tanzania ya viwanda ambayo imekuwa ikihimizwa na Rais wetu
imekuwa chachu kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa
viwanda sambamba na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora ambazo zinaweza
kushindana kwenye soko la Dunia, Afrika na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kabla
ya kuendelea kuzungumzia umuhimu wa kongamano hilo la kibiashara kati
ya Tanzania na Uganda naomba kutumia walau dakika moja ama mbili kutoa
pongezi zangu za dhati kwa Rais Dk. Magufuli kwa namna ambavyo ameamua
kufungua milango ya kuzikaribisha nchi mbalimbali kuja nchi kuwekeza.
Kwa
upendo mkubwa kwa nchi yake, amehakikisha anaweka mkazo katika ujenzi
wa miundombinu ya uwekezaji na kibiashara na matokeo yake muamko kwa
watanzania katika kuwekeza na kufanyabishara umekuwa mkubwa na wenye
tija. Hongera Rais wetu kwa kazi nzuri ambayo unaifanya kwa maendeleo ya
nchi yetu.
Hata
hivyo kupitia kongamano la biashara ambalo linahusisha nchi hizo mbili,
ni wazi Tanzania itatumia nafasi hiyo kama fursa ya kutangaza bidhaa
zake na wakati huo huo Uganda nayo itaonesha bidhaa zake.
Ni
kongamano ambalo kwangu naliona limekuja wakati muafaka hasa kwa
kuzingatia chini ya Rais Magufuli nchi yetu imekuwa na mazingira mazuri
ya kibiashara. Ni wakati muafaka kwa nchi zote mbili kutumia maonesho
hayo kujengeana ujuzi katika utengenezaji wa bidhaa bora na utafutaji
masoko.
Pamoja
na mambo mengine kupitia kongamano hilo la kibiashara itakuwa sehemu
sahihi ya kuweka mbinu na mikakati itakayofanikisha kuongeza thamani
kwa bidhaa zinazotokana na mazao.Sina shaka na hilo hata kidogo na
ukweli kwa Tanzania imedhamiria kuongeza thamani kwa bidhaa za mazao.
Katika
maisha ya kawaida najua unaweza kujiuliza hivi , je Tanzania tunauza
nini zaidi kwa nchi ya Uganda? Jibu vyovyote lakini hili ambalo
nitakueleza ni muhimu
zaidi. Iko hivi mpaka sasa Tanzania inauza bidhaa za mazao na bidhaa za viwandani nchini Uganda.
Takwimu
zilizopo zinaonesha kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita Tanzania
imeweza kuuza bidhaa za mazao ya chakula na viwandani zenye thamani ya
Sh. bilioni 300 kutoka Sh. bilioni 100. Hilo ni ongezeko mara mbili
zaidi ya fedha zilizopatikana huko nyuma.
Ninaposema
Rais Magufuli ameweka mazingira mazuri ya kibiashara naaminisha na
takwimu zinaeleza wazi namna ambavyo nchi yetu ilivyoweka mazingira
mazuri katika sekta ya biashara na viwanda.
Nikiri
kwa namna ambavyo Tanzania unauza bidhaa zake nchini Uganda na
kuingiza kiasi hicho cha fedha, kongamano litakalofanyika nchini
litaongeza wigo zaidi wa kibiashara.
Hata
hivyo kutokana na umuhimu wa kongamano hilo la kibiashara, Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga vema
kuhakikisha kongamano hilo linakuwa na tija na ushiriki wa Watanzania
unakuwa mkubwa zaidi.
Nakumbuka
wakati anazungumzia kongamano hilo Waziri wa Viwanda na Biashara
Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amesema kongamano hilo
litasaidia kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza wigo wa kujenga
viwanda zaidi nchini hasa vya usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani
ya mazao hayo.
Naomba
nitoe rai kwa wafanyabishara na wawekezaji na wote wanaojihusisha na
sekta ya biashara waliopo nchini Tanzania kuhakikisha wanashiriki
kikamilifu na kwa vitendo katika kongamano hilo. Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Rais Magufuli imejikita katika msingi wa kufanya kazi kwa
bidiii.
Hivyo
kwa wafanyabiashara kupitia kongamano hilo wataendelea kunoa vichwa ili
kujiimarisha zaidi kibiashara ana kiuwekezaji kwa maslahi ya nchi yetu
na watu wake kwa ujumla. Nihitimishe kwa kukumbusha tena kongamano la
kibiashara kati ya Tanzania na Uganda litafanyika Septemba 6 na Septemba
7 mwaka huu. Sote tushiriki bila kukosa.
No comments :
Post a Comment