Monday, September 30, 2019

DKT. ABBASI AWAPIGA MSASA MAAFISA MAWASILIANO MUHIMBILI, JKCI, MOI NA MUHAS



Mkurugenzi Mtendaji MNH Prof. Lawrence Museru akiongea na Maafisa Mawasiliano wa MNH, JKCI, MOI na MUHAS (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiongea na Maafisa Mawasiliano wa MNH, JKCI, MOI na MUHAS (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu ya maafisa mawasiliano
Baadhi ya Wakurugenzi MNH na mawasiliano wa MNH, JKCI, MOI na MUHAS wakifuatilia mada wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu ya maafisa mawasiliano.
Baadhi ya Wakurugenzi MNH na Maafisa Mawasiliano wa MNH, JKCI, MOI na MUHAS wakifuatilia mada wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (wa tatu toka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru (wa pili toka kushoto), baadhi ya Wakurugenzi MNH na Maafisa Mawasiliano wa MNH, JKCI, MOI na MUHAS.
……………….
Maafisa Mawasiliano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS), wametakiwa kutangaza maboresho makubwa ya uboreshaji huduma za
afya yaliofanywa na Serikali ya awamu ya tano.
Wito huo umetolewa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati akifungua mafunzo maalumu ya utumiaji sahihi wa mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma kuhusu taarifa mbalimbali katika taasisi hizo.
 “Suala la kutoa habari kwa umma kwa sasa si suala la kiutashi tena bali ni takwa la kisheria kwa mujibu wa sheria ya huduma za habari pamoja na sheria ya haki ya upatikanaji habari,” alisema Dkt. Abbasi
Aidha sekta ya afya imeboreshwa sana tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani na maboresho makubwa yamefanyika ikiwamo upatikanaji wa vipimo muhimu kama CT scan na MRI pamoja na uhakika wa upatikanaji wa dawa katika Hospitali mbalimbali nchini.
“Hivi karibuni nilitembelea Muhimbili na nilijionea mageuzi makubwa yaliyofanyika, nimekutana na wataalamu mbalimbali ambao wamenieleza mambo makubwa yanayoendelea hapa. Sasa mambo haya yote ni vizuri maafisa mawasiliano muyasemee ili wananchi waweze kuelewa,” alisema Dkt. Abbasi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru amesema uongozi umeamua kuitisha mafunzo hayo kwa watumishi wa kitengo cha habari na mawasiliano kwa kuwa hivi sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya upashanaji habari hivyo ni lazima wajifune mbinu mpya.
Mafunzo haya yamefunguliwa leo, yatatolewa kwa siku nne na wakufunzi kutoka Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali yanalenga kuwajengea uwezo watumishi wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano kutoka MNH, MOI, JKCI na MUHAS.

No comments :

Post a Comment