Serikali
imeitaka Benki ya TPB na Benki nyingine nchini kuboresha mifumo ya huduma na
bidhaa zao ili kuvutia Watumishi pamoja na Taasisi za Umma kutumia huduma zao.
Hayo
yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) (pichani) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti
Maalum, Mhe. Jacqueline Msongozi, aliyetaka kujua kwa nini Watumishi na
shughuli zote za Serikali zisitumie huduma za kibenki kupitia Benki ya Serikali
ya TPB.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, taratibu na
miongozo iliyopo ya uchumi huria, Serikali haina mamlaka ya kumlazimisha
Mtumishi au Taasisi ya Umma kutumia huduma za benki yoyote ikiwemo Benki ya TPB.
“Kwa
kuzingatia misingi ya nguvu ya soko, Benki ya TPB imefanikiwa kujitangaza na
kuimarisha huduma na hivyo kuvutia baadhi ya Taasisi za Serikali na Mashirika
ya Umma kutumia bidhaa zake”, alieleza Dkt. Kijaji.
Dkt.
Kijaji alisema huduma za Benki ya TPB zinazotumiwa na Taasisi za Serikali ni
pamoja na akaunti ya muda maalumu, akaunti ya biashara, malipo kwa njia ya
mtandao, kubadilisha fedha za kigeni, kukusanya mapato ya Serikali, kulipa
mishahara ya Watumishi, mikopo kwa Watumishi, kulipa pensheni za Wastaafu
pamoja na mikopo kwa Wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Serikali.
Alisema
kuwa baada ya biashara huria ya Sekta ya Fedha na kupitishwa kwa sheria ya
Benki ya Taasisi ya fedha kuanzia mwaka 1991, Wawekezaji mbalimbali walifungua
benki binafsi nchini na hivyo matumizi ya huduma na bidhaa za benki kuanza
kuamliwa na nguvu ya soko ikiwa ni pamoja na huduma na bidhaa za Benki za
Serikali.
Akijibu
swali la nyongeza la Mbunge wa Madaba Mhe. Joseph Mhagama, kuhusu wafanyabiashara
kushindwa kufanyabiashara kwa kukosa mitaji ili hali kuna Benki ya Serikali ya
TPB, Dkt. Kijaji alisema kuwa Benki hiyo ina mfumo wa kuwasaidia Wajasiriamali
kwa kuwapa mafunzo na mikopo iliyo na riba nafuu.
Aidha
Benki ya TPB kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo Tanzania imetoa mikopo ya
takribani Sh. bilioni 431 kwa Wakulima katika maeneo ambayo Benki ya Kilimo
haina matawi, hivyo kusadifu dhima ya Serikali ya kuwafikia Wananchi wake
katika kuwasaidia kukuza uchumi wao.
No comments :
Post a Comment