Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Sekta
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inakabiliwa na changamoto mbalimbali
zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia
kupungua kwa uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na
rasilimali maji, teknolojia duni za kuhifadhi mazao baada ya mavuno,
uelewa mdogo wa wadau katika kukabiliana na upotevu wa mazao na uhaba wa
miundombinu ya masoko.
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameyasema hayo wakati akimkaribisha Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu
Hassan, kwa ajili ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima,
Nane Nane, yameanza leo tarehe 1-8 Julai 2019, katika Viwanja vya
Nyakabindi mkoani Simiyu.
Mhe
Hasunga amesema kuwa wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo watapata
fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ya bidhaa za kilimo ili kuona
hali halisi ya Maadhimisho pamoja na teknolojia za uzalishaji,
uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, zilivyoandaliwa.
Waoneshaji wengine wako njiani na tunatarajia uwanja huu wa Nyakabindi
utafurika kwa maonesho.
Alisema
kuwa ili kuweza kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo za upotevu wa
mazao baada ya kuvuna, Wizara ya Kilimo imetayarisha Mkakati wa Taifa wa
miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvunwa.
Alisema
kuwa Mkakati huo umeandaliwa ili kuendana na malengo endelevu ya dunia
ya kutokomeza njaa ifikapo 2030, kuhakikisha usalama wa chakula na lishe
na kukuza kilimo endelevu kama lengo la pili la Umoja wa Mataifa kati
ya Malengo 17.
“Katika
utafiti uliofanyika inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 watu watakuwa
bilioni tisa (9) na hivyo mahitaji ya chakula yatakuwa asilimia 60 zaidi
ya mahitaji ya sasa. Hivyo basi mkazo utakuwa kuzalisha chakula kati ya
asilimia 50 – 70 zaidi ya sasa. Hivyo, udhibiti wa upotevu wa mazao ya
chakula ni suala muhimu na la kipekee” Alikaririwa Mhe Hasunga na
kuongeza kuwa
Mkakati
huo utakuwa Mwongozo kwa Sekta za Umma na Binafsi katika kukabiliana na
changamoto ya upotevu wa Mazao baada ya mavuno. Aidha, Mkakati huo
umezingatia mabadiliko yanayoendelea ya Kitaasisi na Kisera.
Alisema,
suala la udhibiti wa upotevu wa mazao ya chakula ni suala muhimu na la
kipeee, linalopaswa kupewa kipaumbele na kila Mdau katika mnyororo wa
thamani na shabaha yetu ni kupunguza upotevu kwa asilimia 50 ya mazao ya
chakula ifikapo 2025.
Waziri
Hasunga ametaja Mkakati huo kuwa una malengo makuu tisa ambayo ni
Kujenga uelewa kuhusu usimamizi wa mazao baada ya kuvuna ili kuboresha
ufanisi na kupunguza upotevu wa mazao katika mnyororo wa thamani;
Kuhamasisha upatikanaji, ufikiaji, unafuu na utumiaji wa teknolojia na
mbinu zilizothibitishwa kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna;
Kuwezesha mifumo ya masoko ya kilimo, ili kuboresha upatikanaji wa soko
na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna; na Kuhamasisha tatifi na
uvumbuzi wa teknolojia mpya inayoendana na mazingira yetu pamoja na
mbinu za kupunguza upotevu wa mazao.
Mikakati
mingine ni Kupitia na kuweka sheria mpya ili kuhakikisha kuwa viwango
vya ubora vinazingatiwa kwa mujibu wa sheria ili kupunguza upotevu baada
ya kuvuna; Kuimarisha uwezo wa taasisi, uratibu, ushirikiano, ubia na
ushiriki wa Wadau wa usimamizi wa upotevu baada ya kuvuna katika
kuimarisha utekelezaji malengo ya kimkakati; Kutengeneza mifumo ya
usimamizi wa mazao baada ya kuvuna ili kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabia nchi; Kukabiliana na upungufu wa fedha katika
kugharamia usimamizi wa mazao baada ya kuvuna; na Kuwa na mbinu za
kiwango kinachokubalika za kukusanya taarifa za upotevu wa mazao baada
ya kuvuna nchini.
Wizara
ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine wameandaa mpango wa
kutekeleza Mkakati huo. Ili kutekeleza mpango na malengo hayo kwa
ufanisi ni vema kushirikikana Wadau wote kwenye mnyororo wa thamani.
No comments :
Post a Comment