| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa anaingia katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Tokyo,Japan. August 26,2019. |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika moja ya Maktaba ya vitabu iliyopo katika Ubalozi wa Tanzania - Tokyo,Japan. August 26,2019. |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akikagua aina ya vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Japan. August,26,2019. |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika ofisi ya Balozi wa Tanzania Nchini Japan. August 26,2019. |
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi amewasili jijini Yokohama, Japan tarehe 26 Agosti kwa ajili
ya kushiriki Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya
Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD 7)
utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.
Mkutano
huu wa Saba utatanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo
Makatibu Wakuu na Mabalozi tarehe 25 na 26 Agosti 2019 ukifuatiwa na
kikao cha Mawaziri tarehe 27 Agosti, 2019 na utahitimiswa na Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019. Kauli mbiu ya
Mkutano huu ni “Kuendeleza Maendeleo ya Afrika kupitia Watu, Teknolojia
na Uvumbuzi”.
Mkutano
wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya
ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na
Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.
Agenda
za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na
kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia
kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na
kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda
za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika,
Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio
mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya
Hewa.
Kutokana
na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya kiuchumi barani Afrika,
Mkutano wa TICAD 7 umeandaa ratiba maalum itakayozishirikisha taasisi
binafsi na za umma kwenye majadiliano ya kibiashara yatakayofanyika
tarehe 29 Agosti 2019. Lengo la majadiliano hayo ni kuwaleta pamoja
wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Serikali wamiliki wa Kampuni,
wafanyabiashara na wawekezaji ili kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali
ya kukuza baishara, uwekezaji na utalii kati ya Japan na Afrika.
Kadhalika wakati
wa mkutano wa saba nchi zote za Afrika zimepatiwa nafasi ya kushiriki
katika shughuli mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za biashara,
uwekezaji na vivutio vya utalii za nchi husika. Tanzania kupitia Bodi ya
Utalii (TTB) imejipanga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini
wakati wa mkutano huo.
Mkutano
wa Saba wa TICAD utahitimishwa kwa Wakuu wa Nchi kupitisha Azimio la
Yokohama na Mpango Kazi wa utekelezaji wa Azimio hilo. Serikali ya Japan
ilianzisha jukwaa la majadiliano kati yake na nchi za Afrika mwaka 1993
kwa ajili ya kujadili maendeleo na nchi hizo.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa
ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo akimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
26 Agosti 2019

No comments :
Post a Comment