Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Kangi Lugola (katikati), akipokea taarifa ya Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la
Magereza,
kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga,
katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma, leo. Lugola aliizindua
Bodi hiyo Mei 30, 2019 na kutoa miezi miwili Wajumbe wa Bodi hiyo kutembelea
miradi mbalimbali ya Magereza Tanzania Bara na kumletea taarifa iyakayoambatana
na maoni yao. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza
na Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, baada ya kupokea taarifa
ya Bodi hiyo, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma, leo.
Lugola aliifurahia taarifa hiyo na kuwataka Wajumbe hao wahakikishe Magereza
inajitosheleza kwa chakula kupitia miradi mbalimbali. Kulia meza kuu ni Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, na wapili kushoto ni Mwenyekiti
wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga. Na wapili kulia ni Kamishna
Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali
la Magereza, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga, akitoa ufafanuzi baada ya
kuwasilisha taarifa ya kipindi cha miezi miwili kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Kangi Lugola (wapili kushoto). Wapili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu. Kulia
ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepokea taarifa ya Bodi ya Shirika la
Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza, na kuwataka Wajumbe wa Bodi hiyo kufanya
kazi kwa bidii ili kuhakikisha Magereza inajitosheleza kwa chakula kupitia
miradi mbalimbali inayomilikiwa na Jeshi hilo.
Waziri
Lugola aliizindua Bodi hiyo Mei 30, 2019, na kutoa miezi miwili Wajumbe wa Bodi
hiyo, kutembelea miradi mbalimbali ya Jeshi hilo na kumletea taarifa ya awali
kuhusu miradi hiyo pamoja na maoni yao.
Akizungumza
na Wajumbe wa Bodi hiyo baada ya kupokea taarifa yao, katika ukumbi wa mikutano
wa Wizara hiyo, jijini Dodoma, leo, Waziri Lugola alisema taarifa
walioiwasilisha ameifurahia licha ya kuwa na mapungufu kadhaa ambayo yanahitaji
uboreshaji zaidi.
Alisema
Bodi hiyo inawataalamu mbaimbali ambao wanaweza wakaleta mabadiliko makubwa ya
uzalishaji mali na kuweza kufanikisha Jeshi hilo linajitosheleza kwa chakula
kupitia wafungwa mbalimbali waliopo magerezani.
“Nawapongeza
sana kwa kazi nzuri, ila nawataka mfanye kazi zaidi ambayo itatuwezesha kuona
mipango mizuri zaidi katika kulisimamia Shirika hili ambalo bodi yake
tuliizindua,”alisema Lugola.
Pia
Lugola aliwataka Magereza kutumia wataalamu wa Jeshi kupima viwanja vyao ili kufanikisha
maendeleo zaidi na siyo kushirikiana na makampuni binafsi.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga,
alisema Bodi yake kwa muda wa miezi miwili ilitembelea mradi wa ng’ombe wa
nyama Mbigiri, mradi wa maziwa Kingolwira, mradi wa Uhunzi, mradi wa Kilimo
Idete, mradi wa kilimo Kiberege na Mradi wa kilimo Isupilo ambapo Bodi hiyo
ilifanya tathmini ya mali zilizopo, mipaka pamoja na historia ya miradi hiyo.
“Pia
miradi mingine tuliyoitembelea ni mradi wa kilimo Ludewa, mradi wa kilimo na
mifugo Kitai, mradi wa kilimo Mkwaya, na pia Bodi itaendelea kutembelea miradi
mbalimbali ya Jeshi na kuendelea kutoa taarifa,” alisema Muhuga.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu aliitaka Bodi hiyo,
ifanye ukaguzi wa kina wa mali za Shirika hilo kiundani zaidi ili taarifa hizo
zije kiuhalisia zaidi na kuleta mikakati imara ya mafanikio.
Baadhi
ya maelekezo aliyoyatoa Waziri Lugola kwa Bodi hiyo mara baada ya kuizindua,
aliitaka kutekeleza maelekezo ya Rais John Magufuli kuhusu suala la Magereza kujitosheleza
kwa chakula na pia bodi ihakikishe maeneo ya magereza yanapimwa na kupata hati
miliki kwa kutumia wataalamu wa kupima ardhi wa Jeshi hilo.
Pia
aliielekeza Bodi hiyo itembelee Magereza yote yenye miradi ya Shirika, na
ifanye mkakati wa kutafuta wawekezaji kama vile wawekezaji kwenye mabwawa ya
ufugaji wa samaki, na pia bodi itoe mawazo mapya ili kuondoa kufanya biashara
kwa mazoea.
No comments :
Post a Comment