
Wawekezaji kutoka Misri wakikagua
ngozi iliyochakatwa katika kiwanda cha Ace Leather kilichopo Mjini
Morogoro mara baada ya kuwasili nchini kwa nia ya kuwekeza katika sekta
ya ngozi.

Bw.Hisham Gazar (kushoto)
Mkurugenzi Mtendaji kiwanda cha Piel Color,Bw.Mahmoud Sargy
(katikati),Mkurugenzi Mtendaji kiwanda cha Sargy Tannery na Mwenyekiti
bodi ya wakurugenzi kiwanda cha Cairo for Investment anda Development.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha
kutengeneza bidhaa za ngozi Woiso Original products Bw.Keneth Woiso (wa
kwanza kulia),Mkurugenzi wa uzalishaji na masoko Dkt.Felix Nandonde
(anayemfuata) wakiwa na wawekezaji kutoka Misri
………………………..
Na. Edward Kondela
Wawekezaji katika sekta ya ngozi
wamewasili hapa nchini wakitokea nchini Misri kufuatia
mwaliko wa Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya
ziara nchini humo kuanzia tarehe 8 hadi 10 Mwezi Julai Mwaka 2019 na
kukutana na wadau wa ngozi nchini humo.
Akizungumza kufuatia ugeni huo
uliowasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili katika Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix Nandonde, amesema umetokana na ziara ya
kikazi aliyofanya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa nchini Misri ambapo
alipokuwa nchini humo alitembelea mji wa viwanda vya ngozi Roubiki na
kuzungumza na wazalishaji wa bidhaa za ngozi nchini humo na kuwapa
mwaliko wa kuja nchini Tanzania kuwekeza katika sekta ya ngozi kutokana
na ubora wa bidhaa ya ngozi inayopatikana hapa nchini.
“Jambo moja kubwa tumeweza
kuwathibitishia hawa wawekezaji katika sekta ya ngozi kutoka nchini
Misri ni kwamba Tanzania ina bidhaa bora za ngozi na wenyewe wamejionea
bidhaa bora za ngozi na ngozi yenyewe ambayo inapatikana nchini,
wamekiri ni ngozi bora, tunaamini kwamba matunda ya ziara ya Waziri Mkuu
Mhe. Kassim Majaliwa imeweza kufungua mlango wa sekta ya ngozi
Tanzania.” Amesema Dkt. Nandonde
Kufuatia ugeni huo wa Bw. Mahmoud
Sargy Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Sargy Tannery,
Bw. Hisham Gazar Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Piel
Color na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Kiwanda cha kuchakata
ngozi Cairo for Investment and Development Mhandisi Yasser El Maghraby,
Dkt. Nandonde amefafanua kuwa anaamini wawekezaji hao watapanga mipango
ya muda mrefu na mfupi kuhakikisha wanashiriki kunyanyua sekta ya ngozi
nchini Tanzania.
Kuhusu ubora wa ngozi Mkurugenzi
huyo wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix
Nandonde amesema wizara imejipanga kuzidi kutoa elimu kwa wachunaji wa
ngozi ili wapate elimu sahihi ya uchunaji na kuwapatia mbinu bora ya
uchunaji wa ngozi kwa kuwa ngozi machinjioni imekuwa ikipoteza ubora
wake kwa asilimia 50 kutokana na uchunaji usiyo sahihi.
“Wizara kwa sasa imeanza
kutoa mafunzo kwa wachunaji mfano Mkoa wa Morogoro kwa kuwa ngozi
inapoteza ubora kutokana na kuharibiwa na visu wakati wa uchunaji hivyo
kuwa na matundu na kupunguza ubora wa ngozi.” Ameongeza Dkt. Nandonde
Licha ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
kutoa elimu ya ufugaji bora mkurugenzi huyo wa uzalishaji na masoko
amewaasa wafugaji kufuga ng’ombe kwa njia bora, kuhakikisa wanawaogesha
ili kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoharibu ngozi pamoja na wafugaji
kutowawekea alama mifugo yao sehemu zisizostahili ambazo zimekuwa
zikisababisha kupoteza ubora wa ngozi.
Awali wawekezaji hao kutoka Misri
mara baada ya kuwasili hapa nchini, waliambatana na maafisa kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kutembelea Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi
WOISO kilichopo eneo la Salasala jijini Dar es Salaam wakiwa na lengo la
kujionea namna ngozi inavyotumika kutengenezea bidhaa mbalimbali.
Wakiwa kiwandani hapo wameshuhudia
idadi kubwa ya vijana walioajiriwa wakiwa katika majukumu yao ya
kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu, mikanda na mabegi ambapo
walitaka kufahamu utendaji kazi wa kiwanda, teknolojia zinazotumika
kiwandani hapo pamoja na soko la bidhaa hizo ili kuangalia maeneo ambayo
wanaweza kushirikiana na wawekezaji waliopo hapa nchini katika sekta ya
ngozi.
Aidha wakiwa jijini Dar es Salaam
wawekezaji hao walipata fursa ya kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa
kiwanda cha kuchakata ngozi Ace Leather kilichopo mjini Morogoro Bw.
Onorato Garavaglia, ambapo walitaka kufahamu pia namna kiwanda hicho
kinavyopata ngozi na hatua inazopitia hadi kuchakata ngozi hiyo kabla ya
kuipeleka sokoni.
Bw. Garavaglia aliwafahamisha
umuhimu wa ujenzi wa kiwanda bora yakiwemo mazingira ambayo hayataathiri
ubora wa ngozi na namna kiwanda chake kinavyozidi kujiimarisha kwa
kufunga mitambo mipya ya kisasa zaidi ili kuchakata ngozi na kuiongezea
thamani zaidi katika soko la kimataifa.
Baada ya mazungumzo hayo
wawekezaji hao kutoka Misri Bw. Mahmoud Sargy Mkurugenzi Mtendaji wa
kiwanda cha kuchakata ngozi Sargy Tannery, Bw. Hisham Gazar Mkurugenzi
Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi Piel Color na Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi kutoka Kiwanda cha kuchakata ngozi Cairo for Investment
and Development Mhandisi Yasser El Maghraby ambao wameonesha nia ya
kuwekeza nchini katika sekta ya ngozi walifika katika kiwanda hicho cha
kuchakata ngozi Ace Leather mjini Morogoro na kujionea madaraja
mbalimbali ya ngozi iliyochakatwa kiwandani hapo na kusema kuwa
wamefurahishwa na ubora wa ngozi iliyopo hapa nchini.
No comments :
Post a Comment